LONDON, England
HADI sasa ni takribani wiki mbili tangu michuano ya ligi mbalimbali duniani ianze kutimua vumbi.
Licha ya kuwa ni siku chache tangu michuano hiyo ianze, lakini kwa baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wameshaanza kubaini mwelekeo na mwenendo wa kila timu utakavyokuwa kwenye michuano hiyo.
Katika mtazamo wa wachambuzi hao wa soka, wameshaona hali ambayo kila timu itakumbana nayo, mafanikio ya makocha na wachezaji.
Kupitia mtazamo wameshabaini kuna makocha ambao msimu huu utakuwa mbaya kwao na huku wengine wakionekana watapata mafanikio zaidi baada ya kukabidhiwa majukumu ya kuzinoa timu hizo.
Na hii ndivyo ilivyo kupitia utabiri ambao umefanywa na mtandao unaojihusisha na utabiri wa masuala ya soka nchini England kwa kutumia njia ya kompyuta uitwao Football Manager.
Katika utabiri wao, kundi hilo la wataalam wa masuala ya soka limejaribu kuangalia hali itakayozikuta timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya England ambazo ni kongwe na zile ambazo ndiyo kwanza zimepanda ligi.
Kupitia utabiri huo wa kompyuta, inaonekana kuwa baada ya Jose Mourinho kurejea Chelsea ataipa ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu tangu mwaka 2010, huku Tottenham ikimaliza ligi ikiwa juu ya Arsenal kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1995, wakati Kocha Martin Jol atafukuzwa na Fulham kabla ya Krismasi na timu mpya kwenye ligi hiyo, Cardiff, Hull City na Crystal Palace, zikiporomoka daraja.
Mtandao huo ambao tangu utengane na gazeti la Evening Standard la jijini London nchini England umekuwa ukijihusisha na masuala ya utabiri wa mambo ya siku zijazo, unaeleza kuwa ujio wa Mourinho katika Ligi Kuu hiyo ni wa mafanikio, wakati Arsenal pamoja na kujikamua pauni milioni 42.4 kumsajili Mesut Ozil, haitaizuia kuzidiwa na Spurs kwenye nafasi ya nne ambayo itafuzu kutinga michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Mtandao huo ambao kwa jina jingine unafahamika kama Championship Manager, umekuwa ukijihusisha na masula hayo tangu mwaka 1992 na umejijengea umaarufu kwenye soka na una watu wapatao 1,000 makocha na wachezaji 500,000 ulimwengu mzima.
Ukiachilia mbali na nafasi za timu zitakavyokuwa kwenye ligi na mambo yatakayowakumba makocha, kwa upande wa wachezaji inaonekana kuwa mshambuliaji mpya, Samuel Eto'o ndiye atakayekuwa mfungaji bora wa Chelsea, akiwa na jumla ya mabao 21 atakayovuna kwenye mechi 33.
Hata hivyo pamoja na kufunga mabao hayo, lakini Eden Hazard ndiye atakayevuna sifa nyingi akiwa na mabao 15 na kusaidia kupatikana mengine 17, yatakayoifanya Blues kutwaa ubingwa wa ligi ikiwa na pointi nne zaidi dhidi ya timu itakayoshika nafasi ya pili, Manchester United.
Utabiri huo unaeleza, licha ya Ozil kupachika mabao saba na kusaidia kupatikana mengine 15 kutoka kwenye mechi 32 atakazocheza na pia Olivier Giroud kufunga mabao 16, Arsenal ambayo itakuwa nafasi ya nne ifikapo Aprili, itapoteza nafasi ya kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya kwa majirani zao, Spurs.
Hatua hiyo itakuja baada ya timu hiyo kufanya vizuri msimu mzima, lakini itajikuta ikipoteza pointi kwa timu za Everton, Hull, Newcastle na Norwich.
Kwa upande wao Fulham, ambao watakuwa wakivurunda katika kipindi hicho, itashuhudiwa wakitengana na Jol ifikapo Desemba na huku baada ya kushikilia mkia kwa muda mrefu kwenye msimamo wa ligi, kocha mpya, Harry Redknapp atafanikiwa kuinusuru baada ya kukusanya pointi kwenye mechi tatu za mwisho.
Inaelezwa kuwa licha ya utabiri huo utaonekana huenda ukawa ni wa kipuuzi, hususani kwa mashabiki wa Arsenal, Kocha wa Spurs, Andre Villas-Boas, amekuwa akiukubali kutokana na kwamba amekuwa akidai kuwa akiwatengeneza wachezaji kwa njia ya gemu na wengine kama vile Ole Gunnar Solskjær na Paul Pogba wakicheza mchezo huo.
Hata hivyo mtandao huo unasema kuwa matokeo ya utabiri huo wa kompyuta yanategemea jinsi gani utakavyouchezesha ili kuweza kupata matokeo ambayo pengine yanaweza kuwa ya kweli.
Kwa ujumla matokeo kamili jinsi msimamo wa ligi utakavyokuwa hadi msimu utakapofikia tamati Mei mwakani ni kama ifuatavyo.
Timu Pointi
1. Chelsea 81
2. Man Utd 77
3. Man City 70
4. Spurs 68
5. Arsenal 65
6. Liverpool 63
7. Swansea 56
8. Norwich 54
9. West Brom 53
10. West Ham 52
11. Southampton 49
12. Aston Villa 48
13. Everton 47
14. Newcastle 47
15. Stoke 47
16. Sunderland 45
17. Fulham 41
18. Cardiff 33
19. Hull 31
20. Palace 31
Hii ni mara ya pili kwa mtandao huo kuitabiria ubingwa Chelsea baada ya kufanya hivyo mapema mwaka huu.
Hata hivyo wakati wataalam hao wa kutumia kompyuta wakitoa utabiri wao, kundi jingine la wachambuzi linapingana nao, likitoa sababu tano ambazo Tottenham haitaipiku Arsenal kwenye orodha ya timu hizo nne bora.
Wanazitaja sababu hizo kuwa ni:
Wanasema kuwa sababu ya kwanza ni kwamba Spurs msimu huu imepoteza mchezaji wake nyota, Gareth Bale ambaye msimu uliopita aliwafungia mabao 21.
Wakosoaji hao wa masuala ya soka wanasema unaweza ukasajili vizuri, lakini huwezi kuziba kwa haraka pengo ambalo utakuwa nalo baada ya kupoteza mchezaji ambaye alikuwa roho ya timu.
Wanasema kuwa sababu ya pili itakayoifanya Arsenal kuibuka kidedea dhidi ya Spurs ni kwamba timu hiyo imesajili mchezaji bora wakati wa usajili wa mwaka huu, Mesut Ozil.
Wanaeleza kuwa kwa kumsajili nyota huyo, Arsenal imefanya jambo la maana mno kutokana na kwamba Mjerumani huyo kwa sasa yupo kwenye orodha ya wachezaji bora 10 wanaotamba kwenye ligi mbalimbali ulimwenguni.
Wanataja sababu ya tatu, kuwa ni kwamba wachezaji wote ambao wamesajiliwa na Tottenham wanahitaji kwanza muda ili kuweza kuzoea mazingira ya ligi hiyo, ikilinganishwa na Arsenal ambaye mchezaji ambaye atakuwa tegemo lao ni mmoja tu, Ozil.
Sababu nyingine ambayo wanaitaja ni uzoefu wa makocha Arsene Wenger na Andre Villas-Boas.
Wanasema katika masuala ya soka sula la uzoefu kwa makocha nalo pia huwa likiangaliwa, hivyo ukiwalinganisha makocha hao utaweza kuona kwa haraka nani mzoefu kwenye ligi hiyo ambapo moja kwa moja jibu litakuwa ni Wenger.
Sababu ya mwisho inayotajwa ni kuhusu michuano ya Ulaya ambapo wanasema kwa msimu huu Tottenham itaikabili Anzhi, Tromso ya Norway na timu ya Sheriff kutoka nchini Moldova kwenye michuano ya Ligi ya Europa hatua ya makundi.
Wanasema kuwa ili iweze kucheza mechi hiyo, itailazimu Spurs kusafiri maili 5039 ikilinganishwa na Arsenal ambayo itaikabili Borussia Dortmund, Marseille na Napoli, umbali ambao utakuwa wa maili 1948 kwa Gunners.
Wanasema umbali huo ni karibia na nusu ya umbali waliokuwa nao mahasimu wao.
No comments:
Post a Comment