LONDON, England
HARAKATI za Arsenal kumshawishi Luis Suarez juzi zilichukua sura mpya, baada ya kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger, kuweka wazi kuwa anataka kuvunja rekodi ya usajili ndani ya timu hiyo ya Gunners, ili kuhakikisha anamnasa nyota huyo wa Liverpool.
Mbali na kuvunja rekodi ya usajili ndani ya klabu yake, kocha wa klabu hiyo ya Emirates, alitangaza kuvunja rekodi ya usajili nchini humo kwa kupanda hadi kufikia dau la pauni milioni 51, ili kuhakikisha anatimiza azma yake.
Hadi sasa rekodi ya usajili ndani ya Arsenal ni pauni milioni 15, ambazo ilizitoa kumsajili, Andrey Arshavin mwaka 2009, lakini kwa sasa Arsenal inaripotiwa kudhamiria kuondokana na rekodi hiyo kwa kumnyakua Suarez.
Hadi sasa Arsenal imeshapeleka ofa karibia mara tatu ikiomba kumsajili mshambuliaji huyo raia wa Uruguay, lakini inavyoonekana Liverpool haijaonesha dhamira yoyote ya kupokea ofa hizo kutoka kwenye klabu hiyo ya Kaskazini mwa jiji la London.
Inaelezwa kuwa Arsenal, safari hii imedhamiria kuweka mezani dau la pauni milioni 51 kumchukua Suarez kutoka Liverpool, kiasi ambacho kitakuwa kimezidi cha pauni milioni 50 ambazo klabu hiyo ililipwa na Chelsea wakati ikimsajili Fernando Torres mwaka 2011.
Endapo Arsenal itaipiku rekodi ya Torres, itakuwa imemfanya Suarez kuwapiku nyota wengine kumi ambao walisajiliwa kwa bei mbaya miaka ya nyuma.
Ifuatayo ni orodha ya wachezaji hao ambao wamewahi kutikisa rekodi ya usajili nchini England, ambao kama dili la Suarez litafanikiwa atakuwa amewabwaga.
10. Andriy Shevchenko: AC Milan kwenda Chelsea:
pauni milioni 30.
Abramovich inadaiwa ndiye aliyewabembeleza mno mashabiki wa AC Milan hadi akafanikiwa kumnasa.
Hata hivyo Shevchenko, hakuweza kufunga mabao kama alivyofanya akiwa kwenye klabu hiyo ya San Siro na nyota huyo anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji walionunuliwa kwa bei mbaya na Abramovich, lakini wakashindwa kuleta manufaa kwa Chelsea.
Katika kipindi alichokipiga kwenye klabu hiyo mchezaji huyo wa timu ya Taifa Ukraini alijikuta akiziona nyavu mara 22 katika mechi 77 alizoshuka uwanjani kuchezea Chelsea, kabla ya kumwaga mbio kwenye Klabu hiyo ya Magharibi mwa jiji London na kwenda kukipiga Dynamo Kyiv, ikiwa ni baada ya kuitumikia miaka mitatu tu.
9. Rio Ferdinand: Leeds kwenda Manchester United kwa pauni milioni 30
Ferdinand
Rio Ferdinand aliingia kwenye historia ya wachezaji waliosajiliwa kwa bei mbaya katika usajili wa Uingereza alipojiunga na Manchester United akitokea Leeds wakati wa usajili wa majira ya joto ya mwaka 2002.
Hata hivyo, beki huyo wakati huo alishaweka rekodi nyingine alipotoka West Ham kwenda Leeds miaka miwili kabla ya kujionesha mwenyewe kuwa ni kinda bora kwenye klabu hiyo ya Upton Park.Ferdinand alishashuka uwanjani mara 430 katika kipindi cha miaka 11 alichoitumikia Manchester United akiwa kama mchezaji na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara sita na ubingwa mara moja wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
8. Dimitar Berbatov: Tottenham kwenda Manchester United –kwa pauni milioni 30.8
Kabla ya kuitema Tottenhm, Berbatov alishafunga mabao 46 katika mechi 102 alizoichezea Spurs.
Hata hivyo hadi anaondoka kwenye klabu hiyo ya Old Trafford, raia huyo Bulgaria hakuweza kulipa kile ambacho, Sir Alex Ferguson alikitarajia kwani baada ya miaka minne aliyoichezea Manchester United na kisha kwenda kujiunga na Fulham, aliuzwa kwa pauni milioni 25, jambo ambalo lilikuwa ni hasara kwa mashetani hao wekundu.
7. Eden Hazard: Lille kwenda Chelsea –kwa pauni milioni 32
Hazard
Hata hivyo ilikuwa ni Chelsea ambayo ilishinda mbio za kumfukuzia mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Ubelgiji baada ya mchezaji mwenyewe kuamua kujiunga na klabu hiyo wakati timu mbili za Manchester nazo kuwa zimeshakubaliana ada na timu ya Lille ili ziweze kunasa saini yake.
Katika msimu wake wa kwanza, Hazard ameshaanza kufurahia maisha ndani ya klabu hiyo ya jijini London, baada ya kufunga mabao 13 na kutoa msaada wa kupatikana mengine 25 yaliyoisaidia pia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa mbele ya Benfica.
6.
Robinho: Real Madrid kwenda Manchester
City – kwa pauni milioni 32
Baada ya kutua katika timu hiyo, Mbrazil huyo alianza vyema maisha yake na Manchester City, lakini muda mfupi akaanza kuonekana hatayaweza kuyamudu maisha ya michuano ya Ligi Kuu.
Baada ya kutokea hali hiyo, Robinho alipelekwa kukipiga kwa mkopo kwenye timu ya Santos, ikiwa ni msimu mmoja tu tangu aishi na timu hiyo ya Sky Blues, kabla ya mwaka 2010 kupata kibarua cha kudumu kwenye timu ya AC Milan.
5. Fernandinho: Shakhtar Donetsk kwenda Manchester City – kwa pauni milioni 34
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye pia anakipiga kwenye timu ya Taifa ya Brazil, msimu uliopita alifanya vizuri akiwa na timu ya Shakhtar Donetsk, wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya ya msimu uliopita na hivyo Man City wana matumaini ataendelea na moto huo.
Hadi anaondoka katika timu hiyo ya Shakhtar Donetsk, Fernandinho ameichezea mechi 284 ndani ya kipindi cha miaka nane aliyoishi Donetsk, na katika kipindi hicho aliweza kupachika mabao kwenye misimu sita.
4. Andy Carroll: Newcastle kwenda Liverpool –kwa pauni 35
Tangu alipojiunga na timu hiyo, Carroll aliweza kufunga mabao 11 katika mechi 58 alizoichezea Liverpool, kabla ya kujiunga kwa mkopo na timu ya West Ham ambako amepewa mkataba wa kudumu wa kuitumikia klabu hiyo ya Upton Park.
3. Sergio Aguero: Atletico Madrid kwenda Manchester City kwa pauni milioni 38
Msimu huo wa kwanza ulikuwa wa manufaa kwa Aguero, ambapo ilishuhudiwa akiumaliza kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Manchester City.
Katika msimu wake wa kwanza, Aguero aliweza kufunga mabao 30 katika mashindano yote na msimu wa 2012-2013 akaongeza mengine 17.
2. Carlos Tevez: Manchester United kwenda Manchester City kwa pauni milioni 47
Tevez alijiunga na Manchester United akitokea West Ham na akaiwezesha kutwaa ubingwa mara mbili katika kipindi cha miaka miwili aliyoitumikia klabu hiyo ya Old Trafford.
Mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Brazil vilevile aliweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Manchester City, baada ya kutoka kwenye mgomo kabla ya kuondoka na kujiunga na vinara wa soka Italia timu ya Juventus.
1. Fernando Torres: Liverpool kwenda Chelsea – kwa pauni milioni 50
Torres aliwahi kufunga mabao ya haraka 50 kuliko mchezaji yoyote katika historia ya Liverpool jambo ambalo lilimfanya aingizwe kwenye vitabu vya kumbukumbu za klabu hiyo.
Hata hivyo, hadi sasa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ameshafunga mabao 15 katika Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment