USHINDI wa
mabao 4-1 ya Simba waliyoifunga Sports Club Villa ya Uganda kwenye mchezo wa maadhimisho
ya tamasha la Simba Day, linalofanyika kila mwaka huwezi kusema kuwa ni kipimo
cha Simba kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania bara inayotarajiwa kuanza
Agosti 24, mwaka huu.
Mchezo huo
uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ulihudhuriwa na mashabiki wengi wa
Simba pia watani wao wa jadi wakiwepo kujionea uhondo wa siku hiyo maalum kwa
watani wao uliosindikizwa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya.
Simba ambayo
iliialika SC Villa kwa ajili ya kunogesha sherehe hizo, ambazo zinafanyika kwa
mwaka wa tano sasa ilianza kwa kuwatambulisha wachezaji wake wote waliosajiliwa
kwa msimu wa 2013/14 akiwepo mshambuliaji Mrisho Ngassa ambaye pia amesajiliwa
na Yanga.
Simba dakika
45 za kipindi cha kwanza haikufanya mashambilizi ya kutisha kiasi cha kusema
kuwa kombinesheni iliyoanza inaweza kuwa kikosi cha kwanza japo ilikuwa na
wakongwe kipa Abel Dhaira, Nassor Massoud, “Cholo”, Ramadhan Chombo “Redondo”
Amri Kiemba, Jonas Mkude, Abdulmalik Humud aliyesajiliwa toka Azam FC na Betram
Mwombeki.
Pia kuna
uchoyo wa pasi pale wanapokuwa karibu na goli, hii sishangai kwani baadhi ya
wachezaji wetu wanapenda waonekane ndio wamefunga wakisahau kuwa mchezo wa soka
ni wa kusaidia na ndio maana wapo 11 uwanjani na kila mtu ana dakika nne za
kuuchezea mpira.
Bao la Simba
la kusawazisha ambalo walilipata dakika ya 43, kupitia kwa Jonas Mkude, ambaye
aliachia shuti akiwa nje ya eneo la
penati, lilipita katikati ya mabeki wa Sports Club Villa na kujaa moja kwa moja
wavuni na kufanya matokeo kuwa 1-1 na kwenda mapumziko wakiwa wameshusha presha
lilikuwa juhudi binafsi baada ya kuona wanapoa pasi mbele lakini ama zinakwenda
nje au kuishia mikononi mwa golikipa.
Kipindi cha pili Simba ilibadilika na kuanza
kushambulia baada ya kufanyika
mabadiliko kadhaa ya kuwatoa Ramadhan Chombo na nafasi yake kuchukuliwa na
Wiliam Lucian, Joseph Owino na kuingia Hassan Isihaka na Amri Kiemba akaingia
Abdallah Seseme na kufanya mchezo kubadilika.
Kikosi cha
wachezaji chipukizi waliokuwepo awali na waliosajiliwa msimu huu ndicho
kilichoonyesha mchezo wa kuvutia na kushambulia kwa nguvu muda wote na
kuwafanya mashabiki kushangilia muda wote wa kipindi cha pili.
Kuingia kwa Wiliam
Lucian kulifanya mchezo uonekane wenye ladha kwani alikuwa akisaidiwa
mashambulizi na beki kinda Issa Rashid
maarufu kama “Baba Ubaya” ambaye ana uwezo wa kupanda na kushuka
kutokana na mbio alizonazo na uwezo wa mapafu yake.
Simba
imejitahidi kufanya usajili mzuri kwa wachezaji chipukizi lakini kwa Abdulhalim Humud na golikipa Andrew
Ntalla unaweza kusema imepotea kwani uchezaji wao hauna tija kwa timu. Pia mshambuliaji
Betram Mwombeki anahitaji kupata
mchezaji ambaye ana uwezo wa kumlisha mipira kwani anaweza kuwamudu mabeki na kuwa “goal getter” kwa vile mwili wake ulivyojengeka kiuchezaji
ukinakshiwa na urefu wake.
Simba
mwishoni ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Mwombeki na nafasi yake kuchukua
Ramadhani Singano 'Messi' na Marcel Kaheza akamrithi Haroun Chanongo walicheza
kandanda safi lakini bado kocha Abdallah
Kibaden anakazi ya kurekebisha kikosi chake ili kicheze kitimu na
kufanya mashambulizi yanayofika mwisho siyo timu ifanye shambulizi ikifika
karibu na eneo la penalti inarudisha mpira kwenye kiwanja chake.
Kwa vile
soka ni mchezo wa kupokezana na ndio maana wana kuwa 11 uwanjani wachezaji wanatakiwa wasiwe wachoyo kupeana
pasi pindi anapoona yeye hayupo kwenye nafasi nzuri ya kufunga kuliko kupiga ili
uonekane bora umepiga.
Pia
mashabiki wakubali kuwa timu inavyocheza michezo mingi ndivyo wachezaji
wanavyozidi kuzoeana na kucheza vizuri hivyo mashabiki wanatakiwa kukubaliana
na matokeo yoyote kwa kipindi cha mwanzo hasa kwa kikosi kilichobadilika kama
cha Simba.
No comments:
Post a Comment