LIGI Kuu England msimu wa 2013-14, inaanza kutimua
vumbi kesho kwenye viwanja mbalimbali nchini humo.
Kila klabu inahaha kuimarisha kikosi chake kwa ajili
ya msimu mpya na kutengeneza mazingira mazuri ya kupata mafanikio.
LENZI YA MICHEZO inakuletea uchambuzi wa kina kuhusu klabu
zote 20 zitakazoshiriki ligi hiyo msimu huu.
Arsenal:
Msimu uliopita; 4, matarajio: Top 4, utabiri; 4
The Gunners wamekuwa kimya kwenye dirisha la
usajili, licha ya taarifa fedha ipo, wana pauni milioni 80 mfukoni, Arsene
Wenger mpaka sasa amemnasa Yaya Sanogo pekee, tena bure. Amewakosa kina Gonzalo
Higuain na Stevan Jovetic kutokana na ubahili wake. Kwa sasa wanahaha kumsaka
Luis Suarez.
Hakuna mbadala wengi sokoni, wanatakiwa kutoa pauni
milioni 50 kumnasa Suarez, swali je, Wenger atatoa? Wanakila kitu kinachoweza
kuwapa mafanikio kwenye ligi, lakini wanakosa straika wa kufunga mabao zaidi ya
25 kwa msimu. Wameitema mizigo kama kina Marouane Chamakh, Gervinho, Denilson,
Sebastien Squillaci na Andre Santos na
kuna wengine wanafuata.
Mchezaji
muhimu: Santi Cazorla ndiyo injini kwenye kiungo cha timu
hiyo na mchezeshaji wa mastraika.
Aston
Villa; Msimu uliopita: 15, matarajio: Kuepuka kushuka daraja, utabiri: 13
Kocha Paul Lambert alitegemea zaidi vijana kuikoa
timu kushuka na alifanikiwa, sasa baada ya kupata uzoefu wa mwaka mmoja,
wanatarajiwa kufanya vizuri msimu ujao. Kumbakiza Christian Benteke ilikuwa
lazima. Beki yao inatakiwa kuboreshwa wamesajili beki kutoka Sevilla Antonio
Luna na Jores Okore, wakiungana na Nathan Baker na Matt Lowton watakuwa vizuri
zaidi.
Mchezaji
muhimu: Christian Benteke, ndiye ataongeza mashambulizi
yao.
Cardiff
City: Msimu uliopita: Wamepanda, matarajio: Kuepuka kushuka daraja; Utabiri: 18
Malky Mackay amefanya jambo la busara kutambua
sehemu za kuimarisha kwenye timu yake, kubaki ligi kuu kutategemea vitu viwili,
kiwango cha nyumbani na rekodi ya mabeki. Kumsajili Steven Caulker kutoka
Tottenham, kutawasaidia kuwa na beki nzuri. Ujio wa John Brayford kutoka Derby,
utaongeza nguvu nyuma. Mabao yanahitajika na uwepo wa Frazier Campbell na Nicky
Maynard utawabeba idara hiyo, pia usajili wa Andreas Cornellius kutoka
Copenhagen ni biashara nzuri.
Mchezaji
muhimu: Kombinesheni ya Peter Whittingham na Craig Bellamy
itakuwa muhimu.
Chelsea;
Msimu uliopita: 3, matarajio: Ubingwa, utabiri; 1
Mpaka sasa Chelsea ndio timu bora ligi kuu, The
Blues kwa sasa wameungana tena na Jose Mourinho ambaye ataifanya timu yake iwe
tayari kwa mapambano toka siku ya kwanza. Hawajafanya usajili mkubwa sana,
lakini wanakikosi kikubwa. Wamemnasa Andre Schurrle kutoka Bayer Leverkusen na
Marco van Ginkel kutoka Uholanzi.
Fernando Torres na Demba Ba kidogo uwezo wao unatia
shaka, Mourinho atasajili straika mwingine. Wayne Rooney atawapa kitu wanataka.
Utatu mtakatifu wa Juan Mata, Oscar na Eden Hazard utatisha na wakiwa na
Mourinho wapinzani watakoma.
Mchezaji
muhimu: Romelu Lukaku ndiye anaweza kuwa straika namba moja
Chelsea kwa sasa.
Crystal
Palace: Msimu uliopita: Wamepanda, matarajio: Kuepuka kushuka daraja, utabiri:
20.
Pamoja na kwamba Ian Holloway ni bonge la kocha,
kikosi chake hakina ubora wa kubaki ligi kuu, kitendo cha kushindwa kumbakiza
Wilfried Zaha kwa mkopo tena kutoka Manchester United, kutaathiri safu yao ya
ushambuliaji. Usajili Dwight Gayle kutoka Peterborough, hauwezi kuziba pengo
lake.
Mchezaji
muhimu: Yannick Bolasie atalazimika kuongeza ufundi ambao
umepotea baada ya kuondoka kwa Zaha.
Everton:
Msimu uliopita: 6, matarajio: Top 6, utabiri: 8
Everton ilipokuwa chini ya David Moyes ilikuwa
haitetereki, lakini sasa ameondoka na mikoba yake imechukuliwa na Roberto
Martinez, ambaye wachambuzi wa soka wanahofu kama anaweza kuipaisha timu hiyo.
Hawajapoteza wachezaji wengi wakati huu wa kiangazi zaidi ya kumuongeza Arouna
Kone ambaye atacheza sambamba na Nikica Jelavic na kuiongeza nguvu safu ya
ushambuliaji ya timu hiyo.
Usajili wa mkopo wa Gerard Deulofeu kutoka
Barcelona, watu wanasubiri kuona akikomaa atakuaje kwa sababu ni mmoja kati ya
vipaji vya kweli kutoka La Masia, atapata nafasi ya kucheza. Ni winga anayeweza
kucheza kulia na kushoto.
Mchezaji
muhimu: Marouane Fellaini na Leighton Baines, ndio watakuwa
injini ya timu.
Fulham:
Msimu uliopita: 12, matarajio: Top 10, utabiri: 16
Fulham hawatakuwa na msimu mzuri na wanahati hati ya
kuwa miongoni mwa timu zitakazokuwa zinapigana kuepuka kushuka daraja. Licha ya
kufanya usajili mpya kwa kuwaleta watu kama kina Fernando Amorebieta, Derek
Boateng na Maarten Stekelenberg, umri mkubwa wa wachezaji wake unaweza kuwafanya
wakachemka, pia hawana mbadala kwenye safu yake ya ushambuliaji. Adel Taarabt
ataongeza ubunifu baada ya kutua kwenye timu hiyo kwa mkopo.
Mchezaji
muhimu: Dimitar Berbatov anahitaji kuendelea kufunga msimu
huu na mabao 15 yatatosha kuwaokoa wasishuke daraja.
Hull
City: Msimu uliopita: Wamepanda, matarajio: Kuepuka kushuka daraja, utabiri: 19
Steve Bruce ameiongoza Hull kupanda daraja msimu
uliopita, timu hii inaweza kuwa nzuri nyuma na kucheza mechi kadhaa bila
kuruhusu bao, lakini kitakachoiharibia ni kukosa safu kali ya ushambuliaji.
Danny Graham anawapa nafasi ya kupambana, usajili mpya Yannick Sagbo bado
hajathibitisha uwezo wake.
Mchezaji
muhimu: Sone Aluko na Ahmed Elmohamady, wanahitaji kuwalisha
Sagbo na Graham kama wanataka kubaki Ligi Kuu.
Liverpool:
Msimu uliopita: 7, matarajio: Top 6, utabiri: 7
Brendan Rodgers anajitahidi kutengeneza timu ya
ushindi Liverpool. Usajili wake wa Januari, Phillipe Coutinho ulikuwa bora.
Wakati huu Luis Suarez akitarajiwa kuondoka, majukumu ya kufunga yako mikononi kwa
Daniel Sturridge na Fabio Borini, wachezaji wapya pia Iago Aspas na Luis
Alberto, wanahitaji kufanya makubwa kwenye msimu wao wa kwanza klabuni, Kolo
Toure ametua bure kuchukua mikoba ya Jamie Carragher.
Mchezaji
muhimu: Phillipe Coutinho anahitaji kuwa kwenye kiwango cha
juu sana ili timu ifanye vizuri.
Manchester
City: Msimu uliopita: 2, matarajio: Ubingwa, utabiri: 2
Kocha mpya Manuel Pellegrini anahitaji kuvaa viatu
vya Roberto Mancini mapema, baada ya kutumia zaidi ya pauni milioni 100 kwenye
usajili wakati huu wa kiangazi, matarajio ya wengi ni City kuwa mabingwa na
kufika mbali Ulaya. Kuchukua nafasi ya Carlos Tevez, amesajiliwa Stevan Jovetic
na Jesus Navas, anatarajia kuongeza ubunifu kwenye kiungo cha timu hiyo.
David Silva alionekana kuchoka msimu uliopita, ujio
wa Navas utamuibua upya. Fernandinho atacheza sambamba na Yaya Toure na
kuimarisha kiungo cha timu. City wanahitaji kuimarisha beki yao.
Mchezaji
muhimu: Sergio Aguero anahitaji kurudi kwenye fomu msimu huu
na kufunga mara kwa mara kama kweli City inataka kufanya vizuri msimu huu.
Manchester
United: Msimu uliopita: 1, matarajio: Mabingwa, utabiri: 3
Kocha mpya, David Moyes ameshindwa kufanya usajili
wa mchezaji mwenye jina kubwa mpaka sasa, kukosekana kwa wachezaji wapya
kunaweza kuwanyima ubingwa. Wapinzani wao wakubwa mbio za ubingwa ni Manchester
City na Chelsea na wote wamefanya usajili mkubwa hasa kwenye eneo la kiungo,
ili kuivua United ubingwa. Ukiangalia vikosi vyao na kulinganisha na Man
United, unaona kwamba United hawana kiungo kikubwa. Michael Carrack ndiye bora
eneo hilo.
Wanakosa ubunifu na waliwakosa mafundi Lucas Moura
na Eden Hazard katika miaka ya karibuni. Beki na safu yao ya ushambuliaji,
inaweza kuchuana na City na Chelsea, sasa wanahitaji kuvunja benki kwa ajili ya
kiungo wa kiwango cha kimataifa, mtu kama David Silva au Juan Mata, na kama
wakimpata mtu watachuana nao.
Mchezaji
muhimu: Robin van Persie ataongoza mashambulizi ya Man
United.
Newcastle
United: Msimu uliopita: 16, matarajio: Top 10, utabiri: 9
Lengo lao kuu wakati huu wa kiangazi ilikuwa ni
kutafuta mtu wa kuchukua nafasi ya Demba Ba, ambaye Januari wamefanya hilo kwa
kumnasa Loic Remy kwa mkopo kutoka QPR, Remy ni chaguo sahihi la kumuongezea
nguvu Papiss Cisse. Msimu uliopita kilichowaharibia ni kukosa kikosi kikubwa.
Mchezaji
muhimu: Hatem Ben Arfa kama akiwa fiti kwa sehemu kubwa ya
msimu, timu hiyo itafika mbali.
Norwich
City: Msimu uliopita: 11, matarajio: Katikati, utabiri: 11
Chris Hughton anajua nini anatakiwa kufanya msimu
huu ili Norwich wasonge mbele na ameshawaleta wachezaji wenye vipaji kama kina
Ricky van Wolfswinkel na Gary Hooper, pia kumsajili moja kwa moja Javier
Garrido ni jambo sahihi alikuwa beki wao bora msimu uliopita na ujio wa Leroy
Fer kwenye kiungo umeongeza nguvu kwenye timu.
Mchezaji
muhimu: Gary Hooper ndiye muhimu zaidi Norwich.
Southampton:
Msimu uliopita: 14, matarajio: Katikati, utabiri: 12
Mauricio Pochettino ataifundisha Southampton toka
mwanzo wa msimu na ameshasajili aina ya wachezaji anaowapenda, amewaleta kina
Victor Wanyama na Dejan Lovren. Hawa wote ni viungo wa ulinzi, Wanyama anaweza
kucheza pia kama beki wa kati.
Wanahitaji kusajili mshambuliaji mwingine
kumuongezea nguvu, Ricky Lambert na Jay Rodriguez.
Mchezaji
muhimu: Gaston Ramirez bado hajathibitisha ubora wake tangu
alipotua kwenye timu hiyo kutoka Bologna.
Stoke
City: Msimu uliopita: 13, matarajio: Katikati, utabiri 17
Stoke wako hatarini kushuka daraja, wameshindwa
kusajili wachezaji wa ukweli. Kuondoka kwa Tony Pulis ni pigo kubwa kutokana na
kocha huyo kuwa ameshatengeneza timu yake na anaijua vilivyo. Stoke itakutwa na
majanga kama yaliyowakuta Charlton, baada ya kuondoka Alan Curbishley. Mark
Hughes ameingia kwenye timu na hajafanya usajili wa maana zaidi ya kumleta Erik
Pieters kutoka PSV.
Mchezaji
muhimu: Charlie Adam anatakiwa kutawala kiungo cha timu
hiyo na kumlisha Peter Crouch zaidi.
Sunderland:
Msimu uliopita: 17, matarajio: Katikati, utabiri: 14
Paolo Di Canio amekuwa akifanya biashara zake kimya
kimya, akimleta Jozy Altidore kutoka AZ Alkmaar, wakati huu wa kiangazi acheze
sambamba na Steven Fletcher. Sunderland walikuwa wabovu nyuma hivyo wamesajili
Modibo Diakite bure kutoka Lazio. Pia usajili wa Emanuele Giaccherini kutoka
Juventus utaongeza ubunifu.
Mchezaji
muhimu: Jozy Altidore anahitaji kufunga kila wiki kuipa
matumaini ya kufanya vizuri timu hiyo.
Swansea
City: Msimu uliopita: 9, matarajio: Top 8, utabiri: 6
Michael Laudrup anatengeneza kikosi kikali Swansea
kwa ajili ya michuano ya Ulaya. Kuchukua Kombe la Ligi na kumaliza nafasi ya
tisa siyo jambo la kubeza. Hawajapoteza wachezaji wao muhimu, wamembakiza Michu
na jeshi lake. Wamesajili wachezaji wengine wakali mapema.
Wilfried Bony alikuwa balaa msimu uliopita Uholanzi,
akifunga mabao 31 msimu uliopita, amesajiliwa kwa dau la pauni milioni 12.
Michu anaweza kucheza nyuma ya Bony. Jonjo Shelvey yuko vizuri pia.
Mchezaji
muhimu: Kombinesheni ya Michu na Bony itakuwa ndiyo siri ya
mafanikio ya klabu msimu ujao.
Tottenham
Hotspur: Msimu uliopita: 5, matarajio: Top 4, utabiri: 5
Spurs wamekosa kidogo tu kushiriki ligi ya mabingwa
kwa misimu miwili nyuma. Kutetereka nusu ya pili ya msimu ndiyo tatizo lao
kubwa. Wamefanya bonge la usajili wakati wa kiangazi, Paulinho ameongeza nguvu
kwenye kiungo na atacheza sambamba na Sandro, Nacer Chadli ataongeza nguvu kwa
Gareth Bale kama akibaki. Bale wakibaki wana nafasi ya kumaliza Top 4, lakini
bahati mbaya ni lazima aondoke, Roberto Soldado ni bonge la straika anayeweza
kufunga mabao zaidi ya 30 kwa msimu.
Mchezaji
muhimu: Roberto Soldado atahitaji kufunga kila wiki kama
wanataka kumaliza Top 4.
West
Brom: Msimu uliopita; 8, matarajio: Katikati, utabiri: 15
Jamaa msimu uliopita walivuka malengo na kumaliza
nafasi ya nane, lakini kuondoka kwa Romelu Lukaku aliyerudi Chelsea ni pigo,
Nicolas Anelka amekuja, lakini ubora wake unatia shaka kama uko kama zamani,
usajili wa Diego Lugano utaongeza nguvu kwenye beki ya timu hiyo.
Mchezaji
muhimu: Shane Long anahitaji kuwa fiti na kuziba pengo la
Lukaku.
West
Ham: Msimu uliopita: 10, matarajio Top
10, matarajio: 10
Sam Allardyce amehakikisha mastaa wake wote
wamebaki, Mohamed Diame, Mark Noble na James Tomkins wamebaki klabuni.
Wamemleta Andy Carroll kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, baada ya
kuichezea kwa mkopo timu hiyo msimu uliopita, usajili wa Stewart Downing
utaongeza nguvu pembeni.
Mchezaji
muhimu: Andy Carroll amesajili kwa pauni milioni 15 na
atatakiwa kuthibitisha thamani yake kwa kucheka na nyavu.
No comments:
Post a Comment