Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, August 30, 2013

11 HAWA WAKIWA CHINI YA MOURIHNO



LONDON, England

NI jambo la kawaida kwenye kizazi cha soka karne hadi karne kuwa na wachezaji nyota wanaotamba katika kipindi hicho.
Kutokana na hali hiyo, imekuwa ikishuhudiwa zikiundwa timu mbalimbali kuanzia mabara hadi dunia zinazowahusisha wachezaji nyota wanaotamba katika kipindi hicho. Katika makala  haya,  tutaangalia wachezaji ambao wanaweza kuunda kikosi cha sasa cha timu ya dunia,  baada ya kung’ara misimu kadhaa iliyopita.

KOCHA: Jose Mourinho.
Huyo anatajwa kuwa kocha bora kwa sasa, baada ya kocha, Alex Ferguson kustaafu na mfumo wake wa 4-3-3 unadaiwa utaifaa timu hii endapo atakabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo.

1.   Mlinda mlango: Manuel Neuer
Mlinda mlango huyo wa timu ya Bayern Munich na timu ya Taifa ya Ujerumani, amekuwa na kiwango kizuri misimu michache iliyopita.
Inaelezwa kwamba baada ya Iker Casillas kuzitumia siku nyingi za msimu uliopita akisugua benchi na huku Petr Cech msimu uliopita akiwa hakufanya vizuri, Neuer  ndiye mlinda mlango pekee ambaye anaweza kuwania nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho cha kwanza.

2. Beki wa kulia: Philipp Lahm
Huyo ni mchezaji mwingine wa timu ya Taifa ya Ujerumani ambaye ana kiwango cha kutosha kuingizwa kwenye orodha hii.
Lahm anaweza kucheza nafasi yoyote ya ulinzi lakini nafasi anayoonekana kuimudu ni ya beki wa kulia.
Jambo hili limeonekana dhahiri, baada ya kocha Pep  Guardiola alipotaka kujaribu  kumtumia kwenye nafasi ya kiungo wa kati lakini nafasi  hiyo ikaonekana kumshinda na hivyo ikabainika dhahiri nafasi ya  beki wa kulia ndiyo mbadala kwake zaidi.


3.  Beki wa kati: Thiago Silva
Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya  Brazil na timu ya  PSG, kwa sasa ndiye anayetajwa kuwa beki  bora wa kati duniani.
Nyota huyo ndiye aliyetoa mchango mkubwa kwenye timu ya Taifa ya Brazil wakati wa michuano ya Kombe la Mabara na ndiye aliyekuwa kizingiti cha safu ya washambuliaji wa Hispania wakati wa mechi ya fainali.
Kutokana na  umahiri huo, nyota pangapangua kama ukitangaza kikosi cha dunia cha karne hii bila jina lake kuonekana utakuwa umefanya makosa makubwa mno.

4.Beki wa Kati: Giorgio Chiellini
Muitaliano huyo anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaozibeba timu za Juventus na timu ya Taifa ya Italia kwa miaka kadhaa iliyopita.
Nyota huyo  ana uwezo wa kukaba, akili ya kimchezo, uwezo wa kutoa pasi, vitu ambavyo anatakiwa kuwa navyo beki wa kati.

5. Beki wa kushoto: Ashley Cole
Cole amekuwa msaada mkubwa kwa klabu yake ya Chelsea  na timu ya taifa ya England.
Inaelezwa kuwa licha ya nyota huyo kuwa na umri wa miaka 32, lakini bado amekuwa akikumbana na upinzani mdogo kutoka kwa wachezaji wengine wanaowania nafasi hiyo.
Baadhi ya wachezaji wanaofukuzia nafasi hiyo ni  kama vile  David Alaba na Jordi Alba.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa ni lazima wakaze buti kwanza kwa  miaka kadhaa kabla ya kumpora namba hiyo Cole.

6.Kiungo wa kati: Xavi Hernandez
Huyo ni kiungo wa kati ambaye kwa miaka mingi ameonekana  kuimudu mno nafasi hiyo.
Inaelezwa kuwa uwezo wake wa kudhibiti mpira  ndilo jambo la pili ambalo linamfanya aingizwe kwenye kikosi hiki.Inaelezwa kuwa  licha ya umri wake kuanza  kumtupa mkono kwenye kibarua chake, bado nyota huyo anaweza kuishikilia nafasi hiyo kwa miaka kadhaa bila kutetereka.


7. Kiungo wa Kati: Bastian Schweinsteiger
Huyu ni mchezaji ambaye amekuwa kivutio cha mashabiki kwa miaka mingi iliyopita.
Hata hivyo nyota huyo anaonekana kutakata zaidi katika kipindi cha miaka miwili ama mitatu iliyopita.
Licha ya msimu uliopita kuikosa penalti kwenye mechi ya fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, lakini uwezo wake katika sehemu hiyo unadaiwa kuwa moto wa kuotea mbali kwenye mechi za kimataifa na za ligi ya ndani.

8. Kiungo mshambuliaji: Andres Iniesta
Mwaka hadi mwaka mwanamume huyo wa shoka  amekuwa akitakata zaidi.
Hali hiyo imejidhihirisha katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kumfanya kupata heshima kubwa katika tasnia hiyo ya soka.
Wachezaji kama  Juan Mata, Mesut Ozil na Mario Gotze wanaonekana kufukuzia nafasi hiyo  miaka michache ijayo, lakini kwa sasa Andres Iniesta yupo kwenye kiwango tofauti.


9. Wingi ya kulia: Lionel Messi
Katika nafasi hii anasimama mchezaji bora wa dunia.
Licha ya kucheza kama mshambuliaji wa pembeni, Messi ana uwezo mkubwa wa  kucheza pia  nafasi ya mshambuliaji wa kati bila kutetereka tofauti na ambavyo inaweza kuleta madhara endapo utaamua kumchezesha kama beki wa kushoto.

 10. Mshambuliaji wa Kati: Robin van Persie
Licha  ya  wachezaji wachache kama  Radamel Falcao, Robert Lewandowski na  Mandzukic kuonesha dhamira ya kunyakua nafasi hiyo, lakini  Robin van Persie ndiye anaonekana kuwa mkali zaidi katika kipindi cha miaka kadhaa aliyokuwa akikipiga  Arsenal na kisha  Manchester United.

Mbali na kipindi cha siku za nyuma, pia msimu huu tayari ameshaanza kuonesha uwezo wake, baada ya kufunga mabao manne katika mechi mbili alizokwishacheza.

11. Mshambuliaji wa  kushoto:  Cristiano Ronaldo
Katika nafasi hii hakuna mjadala mrefu kutokana na kwamba, Ronaldo ndiye amekuwa kinara katika nafasi hiyo kwa muda mrefu.
Umahiri wake umeshajidhihirisha kwenye mechi mbalimbali alizocheza tangu aanze kusakata kandanda.
Umahiri wa nyota huyo ulijidhihirisha tangu akikipiga FC Porto, kabla ya kutua Manchester United na hatimaye Real Madrid.
 Hakuna ubishi wowote kwa sasa kwamba Ronaldo ndiye mchezaji anayeweza kusimama kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo kabla ya kufikiriwa mchezaji yeyote.

No comments:

Post a Comment