KOCHA Jose Mourinho,
amefanya uamuzi wa kumsajili mshambuliaji Mcameroon, Samwel Etoo kutoka
klabu ya Anzhi Makhachkala, baada ya jaribio la kumnasa Wayne Rooney kutoka
Manchester United kushindikana.
Pengine watu wanajiuliza je, Mourinho hasa anahitaji
nini kwani anawashambuliaji mahiri kama vile Fernando Torres, Demba Ba Romelu
Lukaku?
Hili ni swali gumu lakini ni la msingi sana, kwani
wote ni washambuliaji na sasa kufika kwa Eto’o kutaifanya Chelsea kuwa na
washambuliaji wanne katika namba moja.
Jibu ya swali hili ni rahisi kwa Mourinho, pamoja na
kwamba Torres na Lukaku ni wafungaji wazuri, Ba ni mpiganaji na mfungaji pia
lakini kilichomvuta zaidi Mourinho kumsaka Rooney na hata kumnasa Eto’o ni
kutafuta mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufunga, kukaba na kutengeneza nafasi kwa
wengine.
Ni wazi kwamba, Mourinho aliwasoma washambuliaji
wake wote watatu na kuona kwamba kuna upungufu ndiyo maana amehitaji huduma ya
Eto’o kwenye kikosi chake ili kuwa na mbadala wa Torres, Demba Ba.
Kwa aina ya ufundishaji ya kocha huyo kutoka Ureno,
isingekuwa rahisi kumtumia mtu kama Torres kwenye kikosi cha kwanza hasa katika
mechi ngumu, kwani anahitaji washambuliaji wanaoweza kujipanga na kupanga
wenzao na wenye uwezo wa kutengeneza nafasi zao binafsi na kuwatengenezea
wengine jambo ambalo Etoo ni mtaalamu zaidi ya Demba na Torres.
Lukaku bado hajaaminiwa sana kushika mikoba ndani ya
Stanford Bridge, hii inamuweka pembeni katika vita ya namba ingawa pia suala la
uzoefu huwezi kumlinganisha na Etoo.
Msenegal Ba aliifungia Chelsea mabao mawili kwenye
ligi baada ya kununuliwa katika msimu wa
dirisha dogo, huku Mhispania akizidi kupoteza makali yake ya ufungaji kama
alivyokuwa Liverpool.
Wengi wameshapoteza imani na Torres, kwa sasa si
mmoja wa washambuliaji wenye madhara tena kama ambayo ilikuwa ikifahamika.
Torres aliwika sana akiwa Liverpool, iliyokuwa na
aina yake ya uchezaji huku Xabi Alonso akipewa jukumu ya kummegea na kumtengea
mapande mazuri yaliyomuwezesha kucheka na nyavu mara kwa mara.
Wakati Demba Ba akishangaika kufuta ukame wa mabao
uliomkumba tangu Januari, Torres ameshindwa kufikia matarajio ya wadau wa Stamford
Bridge na Lukaku bado kinda ambaye anatakiwa kuanzia benchi.
Mourinho amekosa mfungaji hasa wa mabao licha ya
kuwa na wapishi mahiri na viungo imara, amefanya uamuzi mgumu kumchukua Etoo,
mtu anayemfahamu vyema kwa kuwa alikuwa naye katika kikosi kilichotwaa Klabu Bingwa
Ulaya akiwa na Inter Milan ya Italia.
Pengine Etoo anaweza asiwe suluhisho la muda mrefu
kwa Chelsea, kutokana na umri kuanza kumkimbia, lakini mchezaji huyo aliyetwaa
klabu bingwa Ulaya mara tatu ataleta faraja darajani.
No comments:
Post a Comment