KIUNGO mkabaji wa Simba, Salum Kinje amesema kuwa Yanga
wasitegemee mteremko katika mpambano wao wa funga dimba unaotarajiwa kuchezwa
Mei 18, katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam kabla ya kuondoka Zanzibar, Kinje alisema
kuwa licha ya timu yao kuundwa na vijana wengi, lakini wanategemea kuonyesha
ushindani wa hali ya juu na kuibuka na ushindi.
“Yanga wanaweza wakaidharau Simba kutokana na timu yetu
kuundwa na vijana wengi, lakini wanaweza wasiamini kitakachowatokea siku hiyo
kwani Simba inacheza kitimu zaidi kuliko wao,” alisema.
Alisema kuwa baada ya kupoteza ubingwa msimu huu kilichobaki
ni kuwafunga Yanga siku hiyo ambapo amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa
wingi kuishangilia timu yao.
Katika hatua nyingine, alisema kuwa anatarajia kuendelea
kuitumikia Simba msimu ujao kwani lengo lake ni kutaka kurudisha heshima yake
kwa wapenzi wa timu hiyo ambao hawakuridhishwa na kiwango chake msimu huu.
“Msimu huu haukuwa mzuri kwangu, hivyo nitahakikisha msimu
ujao ninafanya kila linalowezekana ili kuwafurahisha mashabiki, bado nina
mkataba na Simba hivyo nawaomba waendelee kunipa muda wataona wenyewe.
“Simba walinisajili baada ya kuona kiwango changu
kilivyokuwa Kenya, nimekuja hali haikuwa nzuri sana ni kama ilivyo kwa
wachezaji wa Ulaya kama Torres alivyokuwa Liverpool alikuwa mzuri, lakini
alivyokwenda Chelsea hajaonyesha kiwango kizuri lakini mashabiki wanaendelea
kumsapoti,” alisema.
No comments:
Post a Comment