Unaweza kusema ni umri wa mtoto aliyezaliwa hadi kuhitimu elimu
ya msingi kwani ni takribani miaka 12 bila mkoa wa Tabora kuwa na timu
inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya Mirambo kushuka mwaka 2001.
Ilikuwa timu iliyoleta changamoto kwenye ligi kuu zamani
iliitwa daraja la kwanza na kuweza kuwakilisha Tanzania bara kwenye kombe la
Muungano mwaka 1993 lakini baada ya kushuka mkoa wa Tabora ulisahaulika kabisa
kwenye ramani ya soka na kufanya mashabiki wa mkoa huo kukosa burudani.
Kutokana na Mirambo kushuka ilibaki historia ya majina ya
wachezaji waliowahi kuwika wakiwa na timu hiyo kama Quresh Ufunguo, Wastara
Baribari, Jobe Ayoub, Dionis Paul, Said Swed “Scud”, Douglas Muhani, Daddy
Phares na akina marehemu Said John, Abbas Mchemba na wengine wengi.
Leo sipo kukuletea historia ya Mirambo ila nimekukumbusha
kidogo ili kukuleta karibu uvute kumbukumbu ya mkoa wa Tabora kisoka ulivyowahi
kuwika. Msimu wa 2013 utakaoanza
Septemba kiu ya mashabiki imekatwa na Rhino Rangers, timu inayomilikiwa na
Jeshi la Wanachi kambi ya Tabora (JWTZ).
Rhino Rangers ilisajiliwa mwaka 1987 na ilianza kushiriki
ligi daraja la nne wilaya ya Tabora mjini na baadae Ligi ya mkoa wa Tabora
kipindi hicho ilichukulia michezo kama burudani kwa wafanyakazi baada ya kazi
za kutwa.
Mwaka 2008 JWTZ kambi ya Tabora
iliona kuna umuhimu wa kuhakikisha kuwa timu inapata mafanikio na kuona siku
moja inashiriki ligi kuu ili kutoa burudani kwa wana Tabora pia ajira kwa
vijana wenye uwezo wa kusakata kabumbu la uhakika.
Kuhakikisha lengo linafikiwa iliundwa kamati ya watu tisa wa
kusimamia na kuhakikisha Rhino Rangers inafanya vizuri na inafika mbali.
Kamati hiyo
ilikuwa inaundwa na
Meja Prosper
Masawe- Mwenyekiti,
Captain
Samwel Mwaila- Makamu Mwenyekiti,
Clarence Kambona-
Katibu,
Grayson
Kawele - Katibu Msaidizi,
Haji Kubeja -
Mweka Hazina
Osward
Mlaponi, Issa Habibu, Gift Emanuel na Steven Luziga ni wajumbe.
Baada ya
kamati kupatikana na kuanza kazi 2008 Rhino Rangers ilichukuwa Ubingwa wa
wilaya ya Tabora Mjini na Mkoa wa Tabora pia kwenye mwaka huo na kufanikiwa
kuwakilisha mkoa wa Tabora kwenye mashindano ya kanda yaliyofanyika Shinyanga.
Mashabiki wa Rhino wakifuatilia kwa makini mpambano wa timu yao kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora |
Ikiwa kwenye
kituo cha Shinyanga 2009 ilipata nafasi ya kuwa miongoni mwa timu zilizokwenda
kwenye kituo cha Dar es salaam 2010 ambacho kilikuwa kinaundwa na washindi toka
kila kanda.
Ikiwa kwenye
kituo cha Dar es Salaam Rhino Rangers ilifanikiwa kupanda daraja la kwanza na
kwenda kwenye kituo cha tisa bora kilichofanyika Tanga 2011, kituo ambacho ili
uweze kuwa mwenyeji lazima ulipe milioni 25 kwa shirikisho la soka nchini (TFF)
Wakiwa
kwenye kituo cha Tanga, timu za JKT Oljoro, Moro United na Coastal Union
zilipata nafasi ya kucheza ligi Kuu, Rhino Rangers ikishindwa kupata nafasi
ikarudi kujipanga tena kwani ilibaki kwenye daraja la kwanza.
Mwaka
2012 tisa bora ilichezwa Morogoro, timu
za Polisi Moro, JKT Mgambo ya Tanga na Tanzania Prison ya Mbeya ndizo
zilizofanikiwa kupenya na kufanikiwa kuingia ligi Kuu.
Uongozi wa
Rhino Rangers haukukata tamaa bali walichukulia kama changamoto na kurudi
kujipanga na hapa wanasema ligi kuchezwa kwa kituo ndio ilikuwa inasababisha
timu zenye uwezo kupokwa nafasi kauli
ambayo inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (TAREFA)
Yusuph Kitumbo.
“Mkoa
ulikuwa unanunua kituo kwa milioni 25 ambazo zilikuwa zinalipwa kwenye ofisi za
Shirikisho la Soka nchini (TFF) na zilikuwa hazirudishi hivyo mkoa uliakikisha
timu yake inapanda daraja hata kama uwezo wake ni mdogo, hivyo waliwatumia
waamuzi” alisema Clarence Kambona.
Pia anasema
ushahidi wa timu zilizopanda daraja wakati huo na kushuka msimu huo ni Moro
United na msimu huu kuna Polisi Moro ambayo ipo kwenye hatihati ya kushuka na
kushukuru ligi kuchezwa nyumbani na ugenini.
“Mfumo wa
kituo ulikuwa wa ukandamizaji kwani timu zilikuwa zinabebwa pasipo kuwa na
uwezo akatolea pia mfano kituo cha Kigoma kuwa na uzalendo kwani JKT Kanembwa
ilibebwa lakini ilipokuja kucheza nyumbani na ugenini ikashindwa kuchomoza
zaidi ya kushinda michezo ya nyumbani ikajikuta inafungwa michezo ya ugenini”
alitabainisha Clarence Kambona ambaye ni Katibu wa Rhino Rangers.
Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) baada ya kuona na kujiridhirisha
kuwa mfumo wa ligi uliokuwepo haukidhi haja ilibadilisha mfumo wa ligi na kuondoa
ligi za vituo na kurudisha madaraja na kuamua ligi zichezwe kwa mfumo wa
nyumbani na ugenini lakini wakaweka mikoa kwenye kanda ili kupunguza ukali wa
gharama kwani ligi haina mfadhili.
Rhino
Rangers ambayo ilikuwa Kundi C linalohusisha timu za mikoa ya kanda za
magharibi, ziwa kati na kaskazini ilifanikiwa kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu
kuu baada ya kujikusanyia pointi 32 kwenye michezo 14 iliyocheza.
Pia Kambona
anasema wameweka mikakati ya kuhakikisha kuwa Rhino Rangers inafanya vizuri
kwenye ligi Kuu ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya ufundi itakayoshirikisha
uongozi wa chama cha Soka Tabora na uongozi wa serikali wa mkoa huo kwani umoja
ndio utakaweza kusaidia timu kufanya vema.
“Tunatoa
kipaumbele kwa wazawa wa Tabora kwani wametupa ushirikiano wa hali ya juu na
hamasa ya soka Tabora imerejea na kwa kushirikia na wadau na serikali naamini
tutaweza kuipeleka Rhino Rangers tunapotarajia”, alisema.
Kambona
anasema kwa sasa kambi imevunjwa lakini baadae wataita wachezaji wote wenye uwezo
waje wacheze ili kamati ya ufundi itakayotajwa baadae ipate kuchagua wale wenye
uwezo na baadae kuwasajili ili kuunda Rhino Rangers bora kama zilivyo timu
zingine za majeshi ambazo zinaleta changamoto kwenye ligi.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tabora (TAREFA) Yusuph Kitumbo anasema kuwa
wapenzi wa soka wa Tabora ili Rhino Rangers ipate mafanikio na waweze kuziona
Simba na Yanga zinakuja kucheza kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi wanatakiwa
waweke mbele Rhino Rangers kwanza na Tabora kwanza.
“Wanatakiwa
waweke Rhino Rangers kwanza na Tabora kwanza mbele kwani kwa kipindi cha miaka
14 inametosha kujifunza hivyo ushirikiano wao ndio utasaidia timu ifanye vizuri
siyo Simba na Yanga zinakuja halafu wanaanza kuzishangilia na kuicha Rhino
Rangers” alisema Kitumbo
Kitumbo
alisema Usimba na Uyanga wanatakiwa waweke kwenye mechi zingine ambazo Rhino
Rangers haichez, ikiwezekana ziwe zile za
kimataifa.
Pia Kitumbo
anasema uongozi wa Rhino Rangers unatakiwa uendelee kuwa karibu na wao kama
walivyofanya na kwa sababu timu yao mashabiki wa Tabora wanaona kama mali yao
kwani haina zile tabaka za kijeshi itakuwa rahisi kuendelea kufanya vizuri.
Uongozi wa
Chama cha Soka Mkoa wa Tabora (TAREFA) umeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha
unaipandisha Tabora kwenye medani ya soka kama ilivyowahi ikiwa ni pamoja na
kuanzisha kozi za waamuzi, makocha na utawala ili kuhakikisha mchezo wa soka
unaendeshwa na wataalamu.
Kwa kuwa
Rhino Rangers itatumia uwanja wa Ally Hassan Mwinyi katika michezo yake ya
nyumbani TAREFA imesema imewasiliana na wamiliki wa uwanja huo chama cha
Mapinduzi ili kuufanyia ukarabati ikiwa ni pamoja na kuweka vyoo vya nje kwani
hakuna vyoo zaidi ya vilivyopo kwenye vyumba vya wachezaji.
No comments:
Post a Comment