KIUNGO
mshambuliaji wa Azam, Abdi Kassim 'Babi' ni miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa
kuivusha timu hiyo katika michuano ya Kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani
Afrika, inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Babi
aliyeandika historia ya kufunga bao la kwanza kwenye Uwanja mpya wa Taifa, Dar
es Salaam katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya
Uganda ‘The Cranes’ uliochezwa Septemba Mosi, 2007, wakati ikishinda bao 1-0.
Hata hivyo,
amevunja rekodi nyingine baada ya kuifungia Azam bao la kwanza katika mchezo wa
Kimataifa dhidi ya Al Nasri ya Sudan Kusini, wakati ikishinda mabao 3-1, uliochezwa
Februari mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Babi ndiye
aliyefungua ukurasa mpya kwa timu hiyo kuiwezesha kupata ushindi katika mechi
za kimataifa, iliyoanza kushiriki kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo
mikubwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Kutokana na
uwezo wake wa kucheza mechi nyingi za kimataifa akiwa na timu kama Mlandege ya
Zanzibar, Mtibwa Sugar, Yanga, DT Long ya Vietnam na Taifa Stars, ilimjengea uzoefu
mkubwa wa kucheza soka kwa mafanikio.
Hata hivyo,
kutokana na umuhimu wake ndani ya kikosi hicho, kiungo huyo anaweza kuwa
mchezaji tegemezi katika mchezo wao kesho dhidi ya Barrick Young Controllers ya
Liberia utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchango wake
unatarajiwa kuonekana kama alivyofanya katika mchezo wa kwanza dhidi ya Al
Nasri, iliyotolewa katika michuano hiyo baada ya kufungwa jumla ya mabao 8-1
ikiwa ni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini.
Abdi Kassim akipongezwa na wachezaji wenzake baada ya kufunga bao la kwanza kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la shirikisho kwa timu ya Azam dhidi ya Al Nasir ya Sudan, uwanja wa Taifa |
Katika
mchezo uliofuata Azam ilianzia ugenini ambako iliibuka na ushindi wa mabao 2-0,
hivyo inahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili iweze kujiweka mazingira
bora zaidi ya kusonga mbele katika michuano hiyo.
Babi anasema
akipewa nafasi ya kucheza na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Stewart Hall atahakikisha
anaitumia vizuri, lakini Watanzania wanatakiwa kuwapa hamasa na waondokane na
kasumba ya Uyanga na Usimba wa kushangilia timu zao.
Anasema Azam
ni timu pekee iliyobakia katika michuano hiyo kwa timu za Afrika Mashariki,
baada ya zingine kutolewa katika hatua ya awali.
Historia yake
Alianza
kucheza soka akiwa Shule ya Msingi ya Haile Sellasie iliyoko visiwani Zanzibar,
wakati huo akiwa na umri wa miaka mitano, lakini soka lilikuwa kwenye damu ya
familia yao kutokana na baba yake alikuwa mchezaji wa soka.
Baadaye alijiunga na timu ya Vikokotoni FC
mwaka 1995, iliyokuwa ikishiriki ligi daraja la pili, Zanzibar, lakini soka lake
lilianza kung'ara mwaka 1999, baada ya kujiunga na timu ya Mlandege iliyokuwa
ikishiriki Ligi Kuu, Zanzibar.
Kama ilivyo
kwa wachezaji wengi kila mtu anatafuta maslahi zaidi, Babi aliipiga kisogo timu
hiyo na kujiunga na Mtibwa Sugar ya Manungu Turiani Morogoro mwaka 2004, ambaye
alidumu kwa miaka mitatu na baadaye kujiunga na Yanga mwaka 2007.
“Yanga
ilivutiwa na kiwango changu na uongozi wa klabu hiyo uliamua kunisajili,”
anasema Babi.
Kiungo huyu mwenye nguvu za misuli ya kupiga
mashuti makali anasema jina la 'Babi' lilitokana na kaka yake aitwaye Shaban
kushindwa kumwita kwa kutamka Abdi na kujikuta akimwita Babi.
Jina la Babi
liliendelea kuzoeleka na hadi leo watu wengi wamezoea kuita hivyo.
Babi anasema
kamwe hawezi kumsahau Kocha wa zamani wa
Yanga, Simba na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, SylleSaid Mziray (marehemu) ambaye
aliwahi kumwita kwenye kikosi cha Stars baada ya kuona kipaji chake akiwa na
timu ya Mlandege ya Zanzibar.
Kwa mara ya
kwanza aliitwa Taifa Stars 1999 akiwa Mlandege na alidumu kwenye kikosi hicho kwa
miaka 13 mfululizo na hakuwahi kuachwa hadi alipokuja Kim Poulsen aliyechukua
mikoba ya Jan Poulsen.
Anasema falsafa
ya Kim ya soka la vijana ndiyo iliyomfanya atemwe kwenye kikosi cha Stars, japo
anaamini bado ana uwezo na nguvu za kuitumikia timu hiyo.
Hata hivyo
anasema baada ya kuichezea Yanga miaka mitatu, mwaka 2010 alipata nafasi ya
kujiunga na DT Long ya Vietnam, timu ambayo anasema aliunganishiwa na aliyewahi
kuwa mshambuliaji wa Simba na Taifa Stars, Danny Mrwanda.
Babi anasema
alifanikiwa kucheza mechi 11 na kati ya michezo hizo alifunga mabao saba, mabao
manne akifunga kwa mipira ya faulo na matatu kwa mashuti akiwa nje ya eneo la
penalti.
Anasema soka
ya Vietnam lipo tofauti na Tanzania kwani kila timu inamiliki uwanja wake
binafsi vyenye viwango vinavyotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa na Soka
(Fifa), huku vikiwa vimezungushwa fremu za maduka.
Hata hivyo,
anasema waamuzi wa Vietnam ni tofauti na wa kwetu Tanzania, kwani akigundulika
amepokea rushwa kwa ajili ya kubeba timu fulani na kupindisha sheria 17 za soka
anawekwa rumande.
Babi anasema
timu aliyokuwa akichezea ilimfunga mwamuzi miezi sita, kwani ilibainika kupokea
rushwa kwenye mchezo wao.
“Chama cha
Soka nchini humo, kimejiwekea utaratibu suala la ubingwa ni timu yenye uwezo,
ndiyo itakayotwaa ubingwa na ushindani ni mkali tofauti na hapa kwetu unaweza
kujua matokeo ya mchezo kabla timu hazijacheza,” alisema Babi.
Anatabainisha
kuwa kwenye mishahara Vietnam wanalipa vizuri wapo makini na unaanzia dola
5,000 za Marekani na timu ikishinda kila
mchezaji anapata motisha ya dola 1000 na
ikitoka sare walikuwa wanapata dola 100 na ikifungwa hampewi.
Ubaguzi wa rangi
ni tatizo la kudumu Vietnam, anasema alisaini mkataba wa miaka miwili kuchezea DT
Long, lakini alidumu kwa miezi minane tu, kwani wakiwa katikati ya msimu
uongozi ulileta kocha mpya ambaye ni raia wa Ujerumani alikuwa akibagua
wachezaji weusi.
Anasema
alipoona mazingira magumu aliamua kufanya mawasiliano na uongozi wa Azam, ili
aweze kujiunga na timu hiyo.
Alijiunga na
timu hiyo katika msimu wa mwaka juzi kwa mkataba wa miaka miwili, lakini
anajivunia historia ya kufunga bao katika uzinduzi wa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Babi anasema alifunga bao hilo kipindi cha
pili kwa shuti kali la mguu wa kushoto akiwa mita zipatazo 35.
Abdi Kassim kwenye mchezo dhidi ya Al Nasir ya Sudan |
"Nakumbuka pasi alinipa Haruna Moshi 'Boban' nilituliza mpira na kuusogeza mbele kidogo na kupiga shuti kali ambalo lilimshinda kudaka kipa wa The Cranes, ” alisema.
Hata hivyo,
anasema ili mchezaji aweze kudumu kwa muda mrefu kwenye timu anatakiwa anafanya mazoezi kwa kufuata programu
ya kocha wake na kuwa programu yake binafsi.
Anasema yeye
anatenga muda wa saa moja na dakika 15, kwa ajili ya mazoezi yake binafsi na
dakika 30 huzitumia kwa 'sprint' nyingine kuruka kamba na 15 mazoezi ya viungo,
kwani mazoezi hayo yanamjengea stamina, kasi na wepesi uwanjani.
Kiungo huyu anasema, Ramadhan Hamsa Kidilu wa Zanzibar, ambaye alichezea Mlandege na Mtibwa Sugar ndiye mchezaji aliyemvutia lakini kwa sasa amestaafu kwani alimwona enzi zake akicheza soka.
Anasema
viungo wengi wametawaliwa na papara ndio maana wanaonekana hawana msaada na
timu zao ila anasema anamkubali zaidi, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam lakini
si kama ilivyokuwa kwa Kidilu.
“Salum anajitahidi lakini bado ana kazi kubwa
ya kufanya kumfikia Kidilu ambaye alikuwa na vitu vya ziada kuweza kuisaidia
timu ikapata matokeo mazuri,” anasema
No comments:
Post a Comment