Ndugu wana
habari,
KUMEKUWAPO na taarifa za kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa
Wanachama wa Simba uliopangwa kufanyika Kesho (Machi 17, 2013) jijini Dar es
Salaam kujadili mustakabali wa klabu.
Ikumbukwe kwamba
Mkutano Mkuu wa Wanachama ndiyo chombo cha juu kabisa cha maamuzi kwa klabu
yetu. Katiba ya Simba SC imeupa Mkutano Mkuu hadhi ya juu mno na ndiyo maana
imeweka utaratibu wa kufanyika kwake.
Miongoni mwa
utaratibu ni kwamba ni lazima uitishwe na Mwenyekiti aliye madarakani wa klabu.
Kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji, ndiye atakayepanga ajenda, mahali na
wakati wa kufanyika kwa mkutano wenyewe.
Katika miaka ya
nyuma, zilikuwepo nyakati ambapo klabu ilikaa hadi miaka mitatu pasipo kuitishwa
kwa Mkutano Mkuu wowote wa wanachama. Hakuna mwanachama au kikundi chochote
kilichojitokeza kudai mkutano wa dharura wakati huo ingawa ilikuwa ikifahamika
kwamba huo ulikuwa ni ukiukwaji mkubwa wa katiba ya klabu.
Tangu uongozi huu
uingie madarakani takribani miaka mitatu iliyopita, mikutano mikuu miwili ya
wanachama imefanyika kwa mujibu wa KATIBA. Mungu akijaalia, uongozi huu utafanya
mkutano mwingine wa kawaida wa wanachama baadaye mwaka huu.
Hata hivyo, kwa
kuzingatia hali halisi ya klabu, Mwenyekiti wa Simba, Alhaji Ismail Aden Rage
(Mb), mwezi uliopita alitangaza dhamira yake ya kuitisha Mkutano Mkuu wa Dharura
wakati wowote kuanzia sasa.
Rage alisema
mkutano huo ungekuwa na ajenda moja tu; Kujadili Mwenendo wa Klabu kwenye
mashindano inayoshiriki msimu huu.
Kwa bahati mbaya,
Mwenyekiti alishikwa na maradhi na akapelekwa India kwa matibabu na yuko huko
hadi Mola atakapomjalia afya njema na kurejea. Kuna uwezekano mkubwa, Inshallah,
akarejea mwishoni mwa wiki ijayo.
Hii maana yake ni
kwamba uongozi umeridhia kufanyika kwa Mkutano wa wanachama. Kimsingi, kama
uongozi umeridhia, hakuna mwanachama mwingine anayeweza kuitisha mkutano mkuu
mwingine.
Mwenyekiti ameruhusiwa kuitisha Mkutano Mkuu kwa sababu
alichaguliwa na wanachama na hivyo ana nguvu ya kisheria (locus standi)
kufanya hivyo. Hawa wengine wanaoitisha mkutano wana nguvu gani ya kisheria
kufanya hivyo? Walichaguliwa na nani kuwakilisha wanachama? Lini na wapi?
No comments:
Post a Comment