.
“KIPAJI
pekee hakiwezi kukufikisha kwenye mafanikio ila kujituma ndio kutakufanya
ufanikiwe”, haya ni maneno aliyosema mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abeid
Ayew Pele ambaye pia ni Balozi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA)
alipotembelea Tanzania hivi karibuni.
Pele ambaye
alikuwa mshambuliaji wa zamani wa
kimataifa wa timu ya taifa la Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya
Ufaransa, aliwaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kwamba, hakuna njia ya
mkato katika kutafuta mafanikio na kuwataka kufanya jitihada ili watimize ndoto
zao, ikiwa ni pamoja na Serengeti Boys kuhakikisha inafuzu kucheza fainali za
Afrika mwakani.
Pele, ambaye
aliiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao
dhidi ya AC Milan ya Italia, aliwaambia wachezaji chipukizi wakati
alipotembelea kituo cha mafunzo kilicho chini ya Shirikisho la Soka Nchini cha
Karume, na kushuhudia programu ya
mazoezi ya vijana wadogo inayofanyika kila mwishoni mwa wiki, ambako watoto wa kuanzia
umri wa miaka minne hadi 17 hufundishwa mbinu za kucheza soka.
"Katika
kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye alifanya
ziara ya siku tatu nchini ambayo ilikuwa imeandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka Ulimwenguni (FIFA) kuangalia shughuli
mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Hakuna
ambaye atabisha juu ya kauli ya Pele kwani tunaona wachezaji wenye vipaji
vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze kucheza kwa kiwango cha juu
kwani bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria hawawezi kufanikiwa.
Wachezaji wetu waliobahatika kuonana na Pele basi iwe
chachu kwao ya kufikia mafanikio kama yake isiwe ilikuwa ni kupiga picha naye
tu ikaishia hapo, bali watumie falsafa yake ya kuwa kipaji vikubwa haviwezi kuleta mafanikio bali
wafanye jitihada. Jitihada inayotakiwa hapa ni kufanya mazoezi kwa bidii tena
kwa muda mrefu na kusikiliza makocha maana nidhamu pia hujenga na ikachangia
mafanikio.
Mfano mzuri
ambao wachezaji wa Tanzania wanaweza kujifunza juu ya kujituma na kufanya
mazoezi muda mrefu ni Nonda Shaban raia ya Congo ambaye aliwahi kuichezea Yanga
ya Dar es Salaam, Nonda wakati kocha anapanga program yake inaanza saa kumi
jioni yeye saa nane mchana anakuwa uwanja akifanya mazoezi lakini kocha akifika
anaendelea na programu yake na ndio maana aliweza kupata mafanikio ambayo
yamemwezesha kucheza nje ya nchi.
Pele baada
ya kuonana na wachezaji Karume na timu ya Taifa ya vijana waliochini ya miaka
17 “Serengeti boys” alitembelea kituo cha soka cha Azam kilichopo Chamazi
ambapo pia ni makao makuu ya klabu ya Azam, maarufu kama Azam Complex, jijini Dar es Salaam.
Akiwa Azam
kwanza kabisa kabla hajasaini kitabu cha wageni alifanyiwa surprise ya kuimbiwa
happy birthday na kukabidhiwa keki kubwa iliyopambwa uwanja wa soka ambapo siku
hiyo alitimiza miaka 48.
Akiwa Chamazi alijionea mambo mbalimbali ikiwemo
mradi wa maendeleo ya soka ya vijana “ Academy” aliusifia sana na kusema
utaleta matunda makubwa Tanzania baadaye, pia alitumia fursa hiyo kuelezea
namna alivyoiona ligi kuu ya Tanzania kwani jana yake alihudhuria Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Yanga na
Azam.
Pel>Pele ambayo
pia anamiliki shule ya soka, alisema
Azam miaka kadhaa ijayo itakuwa klabu kubwa sawa na za Uingereza
kutokana na uwekezaji wake mzuri. Pia alisema akademi ya Azam ni nzuri na bora
kuliko hata akademi yake.
“Kwetu kuna shule za soka nyingi, lakini
nyingi ni za wawekezaji wa nje (klabu za Ulaya), lakini hii ya Azam ni nzuri
kuliko shule yangu ambayo ni ndogo tu, haifikii hii kwa ubora, nami nina ndoto
za kuwa na akademi kubwa kama hii, na nimejifunza mengi kutoka kwa
Azam,”alisema Pele.
Pia Pele
aliishauri Azam na vilabu vya Tanzania kuachana na desturi ya kuchukua
wachezaji wa nje ya nchi, kwani kama wataitumia vizuri fedha wanazonunulia
wachezaji wakawekeza kusaka vipaji zaidi
nchi mzima watapata wachezaji bora.
“Nawaahidi
tutakuwa tunabadilishana uzoefu na kama
una akademi nzuri kama hii hakuna sasabu ya kuchukua mchezaji kutoka Ghana, hii nchi yenu
ina watu zaidi ya Milioni 40, mnaweza kutengeneza wachezaji wengi wazuri na
nyinyi mkauza Ulaya,”alisema Pele.
Akizungumzia
Ligi Kuu ya Tanzania baada ya kuona mechi ya Yanga na Azam, Pele alisema ina
ubora sawa na ligi nyingine kubwa Afrika na akasema sasa kinachotakiwa ni
kuongeza maboresho pia wachezaji kulingana na alivyoona mchezo alioshuhudia wa
Azam na Yanga alisema kwamba wana uwezo sawa na wachezaji wengi duniani ili watimize ndoto za kucheza Ulaya,
wanatakiwa kuongeza juhudi
"Soka
barani Afrika lina mazingira yanayofanana, hakuna mtoto wa waziri, mwanasheria au
wa mfanyakazi wa benki ambaye anacheza soka. Soka inachezwa na watoto wanaotoka
kwenye familia ambazo hazina maisha mazuri hivyo wana nafasi sawa na wengine
wote. Mnachotakiwa kufanya ni kujituma, kudhamiria na kufanya jitihada ili
mfungue milango ya mafanikio” , alisema Pele, ambaye watoto wake wawili wanaichezea
Marseille.
Pia
aliwataka wachezaji wa timu ya Taifa ya Vijana walio na umri china ya miaka 17
kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika
nchini Morocco, Machi mwakani. "Mkifuzu
mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu", alisema gwiji huyo
ambaye anaiwakilisha FIFA katika kukagua na kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo ya soka
nchini Tanzania.
“Nilivyowaangalia
naona mna uwezo wa kuwaondoa wapinzani
wenu DRC na nitafuatilia mechi yenu.
Mkifuzu tutakuwa wote na nitawaunga mkono”, aliwaambia Serengeti boys. Pele ambaye kwa sasa anamiliki shule ya mpira
wa miguu (academi) alikuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya soka wa FIFA
kwa nchini za Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na Emmanuel Maradas mjumbe wa
Idara ya Mawasiano ya FIFA , walikaa nchini
kwa siku tatu ambazo walizitumia kupata taarifa za shughuli mbalimbali za
maendeleo, zikiwemo za soka la watoto (grassroots), soka la vijana, soka la
wanawake na miradi ya viwanja vinavyokarabatiwa na FIFA kama ule wa Nyamagana
Mwanza na Zanzibar.
Shirikisho
la Soka nchini kupitia idara ya ufundi linatakiwa kuwekeza zaidi kwenye shule
za soka ili kuwapa fursa zaidi vijana
wadogo kuonyesha vipaji vyao ili viweze kuendelezwa. Nasema hivi kwa sababu TFF
wana uwezo wa kuamuru kila chama cha soka cha mkoa nchini kiwe na darasa la
shule za soka kila jumamosi na jumapili na kwa sababu karibu mikoa yote ina
viwanja na makocha wataweza kufanya hivyo. Pamoja yote pia ligi za vijana
viwepo siyo mpaka Copa cocacola tu ambayo pia vile vipaji vinavyopatika
vinapotea tu kwa sababu hakuna mahali
maalumu pa kuwaweka ili kuendeleza vipaji hivyo.
Pia
wasisitize timu zinazocheza ligi kuu zianzishe shule za soka ili kupunguza
fedha wanazotumia kununua wachezaji wa kigeni wawekeze kwenye shule za soka.
Kwa kufanya hivyo wanaweza kuuza wachezaji nje baadaye na watakuwa na vipaji na
wachezaji wanaoujua mpira kisawasawa.
Wachezaji wa
kitanzania ambao mnajua mna kipaji cha kucheza soka mjitume na nidhamu pia iwe
ndio ngao yenu ili mfike kwenye
mafanikio muweze kujisaidia wenyewe, familia zenu na nchi yetu. Najua kwa sasa
upo mfano mzuri wa kuiga ambao ni Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu vijana
wadogo wanaochezea TP Mazembe ambao utajiri unawanukia kabla ya kufikisha miaka
20. Mlikuwa mnawaona wakicheza mpira wakiwa uwanja wa Karume wakati kuna ile
shule ambayo Shirikisho la Soka nchini lilikuwa na mkataba na Bolton Wonderus
ya Uingereza mkataba ambao hata hivyo ulivunjika na kila mchezaji kurudi kwenye
timu zao za awali na wengine kusajiliwa na Yanga, Mtibwa, African Lyon na
Simba. Baadhi ya wachezaji waliotoka kwenye shule hiyo ambayo makao yake makuu
yalikuwa kwenye hostel zinazomilikiwa na TFF zilizopo Karume ni Mbwana Samata,
Thomas Ulimwengu, Simon Msuva, Issa
Rashid “baba ubaya”, Omega Seme, Jamal Mroki, Barwany Khomein, Jerome Lambele,
Leonard Muyingwa na wengine wengi.
Tuache
kulalamika tujitume wenyewe mafanikio yatafuata nyuma ili ziara ya Pele isiwe
alikuja tupige naye picha za kutundika ukutani au kuweka kwenye albamu tu bali
iwe ni kumbukumbu ya kutusukuma tufikie mafanikio kama yake na pengine zaidi
yake. Natoa hoja.
No comments:
Post a Comment