Baadhi ya waamuzi wa daraja la kwanza wakiwa kwenye semina jijini Dar es salaam hivi karibuni |
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Waamuzi Taifa (FRAT) waliokuwa wamekutana Dodoma kuanzia Octoba 6-7 mwaka huu wameshindwa kufanya mkutano mkuu wa kuwachagua viongozi wapya kutokana na kamati ya uchaguzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuondoa baadhi ya wagombea.
Wagombea waliondolewa ni Omary Abdukadir aliyekuwa anagombea nafasi ya Mwenyekiti, Sudi Abdi aliyekuwa anagombea nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Ruvu Kiwanga aliyekuwa anagombea nafasi ya mjumbe wa kamati ya utendaji ya chama cha waamuzi Taifa (FRAT).
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati inayosimamia uchaguzi huo Alhaj Muhindin Ndolanga alisema kuwa sababu iliyofanya wagombea hao kuondolewa na kamati ya uchaguzi ya TFF ni fomu zao kujazwa na watu wengine na wao kuweka saini tu.
"Wagombea walioondolewa wameondolewa kwa sababu fomu zao zilijazwa na watu wengine hivyo kulingana na kanuni hilo ni kosa, na sisi tunaheshimu maamuzi ya wajumbe tunakwenda kuandaa mchakato mwingine wa uchaguzi", alisema Ndolanga.
Wajumbe wanalalamikia kitendo cha uchaguzi huo kutofanyika kwani wamekuwa wakijigharamia kila kitu kuhudhuria mkutano huo.
Hii ni mara ya tatu kwa uchaguzi wa FRAT kukwama baada ya 2010, FRAT kutakiwa na shitikisho la soka nchini kuwa na katiba mpya, hivyo kuanza mchakato wa katiba mpya na 2011 kukwama tena baada ya katiba hiyo mpya kutokidhi matakwa kwani ilikuwa haiwatambui wanachama wa wilaya ambao ndipo cha kinapoanzia.
No comments:
Post a Comment