Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa pongezi kwa uongozi mpya wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha (ARFA) uliochaguliwa katika
uchaguzi uliofanyika Oktoba 7 mwaka huu.
Ushindi
waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ARFA walivyo na imani kubwa kwao katika
kusimamia mchezo huo mkoani Arusha.
TFF
inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya ARFA
chini ya uenyekiti wa Khalifa Mgonja ambaye amechaguliwa tena kuongoza
chama hicho.
Uongozi
huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha
shughuli za mpira wa miguu mkoani Arusha kwa kuzingatia katiba ya ARFA
pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia
tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya ARFA na Kamati ya Uchaguzi ya
TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za
uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi
waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Khalifa Mgonja (Mwenyekiti), Seif
Banka (Makamu Mwenyekiti), Adam Brown (Katibu), Peter Temu (Mjumbe wa
Mkutano Mkuu TFF), Omari Walii (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Mwalizo
Nassoro (Mhazini).
Waliochaguliwa
kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi huo uliofanyika
Leganga, Usa River ni Hamisi Issa, Athuman Mhando na Eliwanga Mjema.
Nafasi ya Katibu Msaidizi iko wazi na itajazwa katika uchaguzi mdogo
utakayofanyika baadaye.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment