MELI YAPAMIA MWAMBA BISMARCK ZIWA VICTORIA
Meli kubwa ya abiria na mizigo ya MV New Mwanza imepata changamoto na kugonga Mwamba wa Bismarck katika Ziwa Victoria majira ya asubuhi wakati ikiwa katika utaratibu wa kawaida wa majaribio ya maandalizi ya kuanza safari zake rasmi za kibiashara.
Tukio hili limetokea wakati chombo hicho kikiwa kimebeba wadau na viongozi wa sekta ya usafirishaji waliokuwa jijini Mwanza kwa ajili ya Mkutano wa 19 wa Kila Mwaka wa Tathmini ya Sekta ya Uchukuzi.
Meli hiyo ilikuwa imepaki kwa muda mrefu katika gati lake na Serikali kupitia Shirika la Huduma za Meli (TASHCO) ilikuwa katika maandalizi ya awali ya kuanzisha safari zake za kiutendaji kulingana na ratiba wakati kisa hicho cha kugonga mwamba kikijitokeza.
Taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda zikiwemo za shuhuda Bakari Mwigela zinaeleza kuwa tukio hilo lilichochewa na hatua ya ghafla ya kukwepa kivuko cha abiria kilichokuwa kikitokea Sengerema ambacho kilikuwa hatarini kugongana uso kwa uso na MV New Mwanza.
Hata hivyo, imeelezwa katika juhudi hizo za kubadili njia katikati ya mkondo wa maji, meli hiyo ilijikuta ikipoteza mwelekeo wa kawaida wa chombo kikubwa na kuishia kugonga sehemu ya Mwamba wa Bismarck.
Maelezo ya awali yanaonesha kuwa hatua hiyo ya haraka ya nahodha ilisaidia kuzuia maafa makubwa zaidi ambayo yangejitokeza iwapo vyombo hivyo vingegongana .
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Salum Hamdun amewahakikishia wananchi na wadau wa usafirishaji kuwa uchunguzi wa awali wa wataalamu unaonyesha kuwa meli iko salama na hakuna sababu ya kuingia hofu.
Aidha amesema Mkoa umefanya mawasiliano ya moja kwa moja na Wizara ya Uchukuzi pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuunda timu ya pamoja ya kiufundi itakayochunguza chanzo halisi na kubaini kiwango cha madhara kabla ya kutoa taarifa rasmi kwa umma.
Meli ya MV New Mwanza iliyozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Januari 23, 2026, katika Bandari ya Mwanza Kusini imejengwa na mkandarasi kutoka Korea, Gas Entec Ship-Building, kwa kushirikiana na TASHICO kwa gharama ya shilingi bilioni 120.56.
Meli hiyo imetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na imefanya safari sita za majaribio katika ruti ya Mwanza–Bukoba tangu Machi 2025, ambapo matokeo yake yameridhisha na TASAC imeruhusu kuanza rasmi kwa safari.
Meli hiyo yenye ghorofa nne na urefu wa mita 92.6 ndiyo kubwa zaidi katika ukanda wa Maziwa Makuu, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa matatu kwa wakati mmoja imekusudiwa kuwa mkombozi wa kiuchumi na kiusafiri kati ya Mwanza, Bukoba, na nchi jirani za Uganda na Kenya.
Tukio la kuondoka kwa meli katika njia yake linahusishwa na sababu za kiufundi za tabia ya vyombo vikubwa vya majini (ship hydrodynamics na momentum). Meli kubwa kama MV New Mwanza inapokuwa majini inahitaji eneo kubwa la kugeuka (turning radius) na muda mrefu wa kupunguza mwendo.
Wakati hatari ya kugongana na kivuko cha Sengerema ilipojitokeza kwa ghafla, nahodha alilazimika kukata kona au kubadili mwelekeo kwa dharura (evasive maneuver), hatua inayopelekea chombo kikubwa kama hicho kuondoka katika mkondo salama wa maji (navigable channel) na kwenda moja kwa moja kugonga miuamba hiyo ya Bismarck.
Matukio ya namna hii katika Ziwa Victoria mara zote hurejesha kumbukumbu zenye simanzi za ajali kubwa za zamani zilizowahi kutokea ziwani humo. Mwaka 1996, taifa lilipata pigo kubwa baada ya meli ya MV Bukoba kuzama na kuua mamia ya wananchi kutokana na changamoto za uzito kuzidi na uchakavu wa miundombinu. Miaka kadhaa baadaye mwaka 2018, ajali nyingine ya kivuko cha MV Nyerere ilitokea katika Kisiwa cha Ukara na kupoteza maisha ya watu wengi.


Post a Comment