Watanzania Milioni Sita Wananufaika na Uchumi wa Buluu



Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Reuben Kwagilwa, amebainisha kuwa Watanzania takriban milioni sita wananufaika na Uchumi wa Buluu kupitia sekta ya uvuvi, ambayo inachangia asilimia 2.2 katika pato la taifa. 

Ameyasema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Nadra Ghulam Rashid, aliyetaka kujua mikakati ya pamoja ya Serikali mbili za Muungano katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu, ambapo alifafanua kuwa serikali zote mbili zinashirikiana kikamilifu kutekeleza Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2024 na Sera ya Uchumi wa Buluu ya Zanzibar ya mwaka 2022 kupitia mikakati ya utekelezaji ya mwaka 2024 hadi 2034 na mwaka 2022 hadi 2027.

Katika kuimarisha usimamizi na ushirikiano huo, Mhe. Kwagilwa alieleza kuwa serikali zimekuwa zikiandaa kwa pamoja Mwongozo wa Uchumi wa Buluu, kufanya uainishaji wa maeneo ya kipaumbele, kuandaa Mpango wa Matumizi Endelevu ya Maeneo ya Maji, pamoja na kuratibu mikataba, itifaki na maazimio ya kikanda na kimataifa. 

Alisisitiza kuwa hatua hizo za ushirikiano zinalenga kuimarisha uratibu na kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa mtazamo wa pamoja kwa kuzingatia majukumu ya kila upande wa Muungano, huku akiongeza kuwa kupitia mifuko mbalimbali, serikali inawasaidia wanawake wakiwa katika vikundi au mmoja mmoja, sanjari na kuwepo kwa mradi wa mabadiliko ya tabianchi wenye thamani ya dola milioni 150 zinazotekelezwa katika halmashauri 65 nchini, zikiwemo 11 kutoka Zanzibar.

Kufuatia ukuaji thabiti wa sekta hiyo, Tanzania imeendelea kupiga hatua kubwa kimataifa na inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi utakaofanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026, ambapo pamoja na mambo mengine utajadili masuala ya utunzaji na uendelezaji wa Bahari ya Hindi huku serikali zote mbili zikiendelea kuratibu maandalizi na ushiriki kwa pamoja.

 Aidha, akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Magomeni, Mhe. Imamu Vuai, kuhusu mikakati ya kuwawezesha vijana, Mhe. Kwagilwa alieleza kuwa serikali imeweka utaratibu maalum wa kufungua fursa na kuwawezesha vijana wa pande zote za Muungano kupitia rasilimali fedha ili washiriki kikamilifu katika miradi ya uvuvi na kilimo inayotokana na Uchumi wa Buluu.

No comments