Benki ya Dunia Paa Moja na Serikali ya Rais Samia



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake nchini, Bw. Nathan Belete, ambaye alifika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumuaga kufuatia hitimisho la utumishi wake hapa nchini. 

Katika ziara hiyo, Bw. Belete alitumia fursa hiyo kumtambulisha mrithi wa nafasi yake, Bw. Firas Raad, ambaye tayari ameanza rasmi majukumu yake mapya nchini. 

Katika hatua iliyoonyesha imani kubwa kwa nchi, kiongozi huyo anayeondoka ameipongeza kwa dhati Tanzania kwa usimamizi thabiti na wa ufanisi wa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, akibainisha kuwa taifa hili limekuwa miongoni mwa nchi za kupigiwa mfano barani Afrika kwa utekelezaji mzuri wa miradi hiyo kutokana na nidhamu kubwa ya matumizi ya rasilimali na msukumo wa serikali katika kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Bw. Belete alikwenda mbali zaidi na kusisitiza kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya Tanzania zimekuwa zikitumika vizuri na kuleta tija inayoonekana, huku akibainisha kuwa katika kipindi chake cha uongozi, ushirikiano kati ya pande hizo mbili umeimarika kwa kiwango kikubwa katika sekta za kimkakati kama vile elimu, afya, nishati, maji, hifadhi ya jamii, miundombinu, na mageuzi ya kisera, sambamba na miradi inayotekelezwa visiwani Zanzibar. 









Kwa upande wake, Rais Samia alimshukuru sana Bw. Belete kwa ushirikiano mkubwa alioutoa tangu alipoanza majukumu yake nchini mwezi Novemba 2022, akieleza kuwa mchango wake umekuwa chachu ya kuimarisha uhusiano wa serikali na taasisi hiyo kubwa ya kifedha duniani na kusukuma mbele ajenda za maendeleo, huku akimpongeza pia kwa kupata nafasi mpya ya kikanda barani Afrika na kumtakia mafanikio mema.

Akifafanua kuhusu mustakabali wa ushirikiano huo, Rais Samia alieleza kuwa Tanzania imeshirikiana na Benki ya Dunia katika utekelezaji wa programu na miradi 18 inayogusa sekta mbalimbali nchini ikiwemo usafirishaji, nishati, maji, na ustahimilivu wa tabianchi, ambayo imesaidia kuboresha maisha ya Watanzania huku serikali ikiweka msisitizo kwenye vipaumbele vinavyoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

 Mkuu huyo wa nchi alitaja maeneo ya kipaumbele ya kikanda kuwa ni pamoja na miundombinu ya reli ya SGR inayoelekea nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, nishati safi ya kupikia, kilimo, na usalama wa chakula. 

Katika kuhitimisha mazungumzo hayo, Rais Samia alimkaribisha rasmi Mkurugenzi Mkazi mpya, Bw. Firas Raad, na kumhakikishia ushirikiano thabiti wa serikali, huku Bw. Raad akionyesha kuvutiwa na mwenendo mzuri wa maendeleo, utulivu wa uchumi, na fursa za ukuaji zinazozalisha ajira na kupunguza umaskini nchini Tanzania.

No comments