URITHI WA KARDINALI PENGO: NI WITO WA KUREJEA KWENYE MAADILI, UKWELI NA UMOJA WA KITAIFA



KATIKA kipindi hiki ambacho ulimwengu wa kidijitali umetawaliwa na kasi ya habari zisizothibitishwa, kifo na mazishi ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo yameacha ujumbe mzito kwa taifa. 

Ni ujumbe unaowataka Watanzania kuachana na utamaduni wa kuishi kwa "kuhisi na kudhani" kupitia mitandao ya kijamii, na badala yake kurejea kwenye misingi ya kweli ya maadili, uzalendo na mshikamano wa dhati.

Akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya mazishi iliyofanyika Pugu, Dar es Salaam, Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ametoa onyo kali dhidi ya ugonjwa wa ubaguzi na uhasama wa kisiasa. 

Dkt. Nchimbi ameuita ugomvi wa kivyama kuwa ni "ujinga," akisisitiza kuwa nchi ni moja na hakuna sababu ya wananchi kugawanyika. Kauli hii ni dokezo tosha kwa watumiaji wa mitandao wanaotumia majukwaa hayo kupandikiza mbegu za chuki, badala ya kujenga hoja za kuliunganisha taifa.

Kwa upande wake, Jaji Mstaafu Joseph Warioba amegusia pengo kubwa lililoachwa katika nyanja ya uadilifu. Amesema Kardinali Pengo alikuwa sauti ya kinabii iliyokemea kuporomoka kwa maadili bila uoga. Katika zama hizi ambapo "kiki" na umaarufu wa dharura vimechukua nafasi ya utu, hotuba ya Warioba inatukumbusha kuwa urithi wa kweli haujengwi kwa idadi ya wafuasi wa mtandaoni, bali kwa uaminifu na msimamo usiotetereka katika kutetea haki na usawa kwa wote.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thadeus Ruwa’ichi, ameeleza kuwa maisha ya Pengo ya miaka 55 ya upadri hayakuwa ya "kubahatisha." Huu ni ujumbe mahususi kwa jamii ya sasa inayotafuta njia za mkato kufikia mafanikio. Ruwa’ichi amesisitiza kuwa utumishi wa Pengo ulijengwa katika kujitoa na kujisadaka, jambo linalotofautiana na maisha ya kudhania yanayohubiriwa na baadhi ya watu kwenye mitandao, ambao hueneza taswira ya mafanikio yasiyo na jasho wala uadilifu.

Aidha, ushiriki wa viongozi wa kidini kutoka nchi jirani za DRC na Rwanda ni uthibitisho wa nguvu ya mshikamano inayovuka mipaka. Hii inatupa somo kuwa amani tunayoifurahia Tanzania ni tunda la jitihada za viongozi kama Pengo walioamini katika mazungumzo na maridhiano. Ni wito kwa kila Mtanzania kutotumia simu yake mkononi kama silaha ya kubomoa amani hiyo, bali kama chombo cha kuhubiri umoja na upendo miongoni mwa watu wa imani na itikadi tofauti.

Kwa kuhitimisha, safari ya mwisho ya Kardinali Pengo iwe chachu ya mabadiliko ya fikra. Taifa linahitaji watu wanaosimama kwenye ukweli, wanaofanya kazi kwa uaminifu bila "kutegea," na wanaoweka mbele maslahi ya nchi badala ya hisia potofu za mitandaoni. Huu ndio mshikamano na amani aliyokuwa akisisitiza Pengo; misingi ambayo ni lazima iendelezwe ili kulinda heshima na utulivu wa Tanzania kwa vizazi vijavyo.

No comments