BMT YAMWAGA SH BILIONI 5.8: MAGEUZI MAKUBWA YA MICHEZO TANZANIA
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kuinua sekta ya michezo nchini kwa kuimarisha uwezeshaji wa timu za taifa na wanamichezo binafsi.
Katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2023 hadi kufikia Januari 2026, Baraza limetumia jumla ya Sh 5,829,403,959 kugharamia ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.
Mchanganuo huo unaonyesha kuwa Sh 810,175,635 zilitumika mwaka 2023/2024, huku kiasi kikubwa cha Sh 3,803,566,185 kikitumika mwaka 2024/2025, na kufikia Januari ya mwaka wa fedha 2025/2026, tayari Sh 1,215,662,139 zimeshakabidhiwa kwa wadau wa michezo.
Katibu Mtendaji wa BMT, Bi. Neema Msitha, amebainisha kuwa uwekezaji huo umetoa matunda makubwa katika soka la kimataifa, ambapo timu ya Taifa Stars iliwezeshwa kushiriki mashindano ya CHAN (Agosti 2025) yaliyofanyika nchini Tanzania, Kenya, na Uganda, pamoja na kufika hatua ya 16 bora katika fainali za AFCON nchini Morocco mwezi Desemba 2025.
Aidha, timu ya wanawake ya Twiga Stars ilishiriki mashindano ya WAFCON nchini Morocco Julai 2025, huku timu ya soka ya watu wenye ulemavu (Amputee Football) ikiiwakilisha nchi nchini Burundi mwezi Septemba 2025 katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati.
Mbali na soka, uwezeshaji huo umegusa michezo mingine mingi ikiwemo Netiboli, Pooltable, Kuogelea, Gofu, Wavu, Judo, na michezo ya Paralimpiki.
Mafanikio makubwa yalionekana katika mchezo wa riadha ambapo Alphonce Simbu alitwaa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Dunia nchini Japan mwezi Septemba 2025, baada ya kufanya vizuri nchini China mwezi Novemba 2023.
Katika mchezo wa ngumi, bondia Grace Mwakamela aliweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kutwaa medali ya fedha kwenye mashindano ya Afrika nchini Cameroon mwaka 2023, huku Yusuf Changalawe akitwaa fedha katika mchujo wa Olimpiki barani Afrika mwezi Aprili 2024.
Hatua hii ya BMT inaonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuhakikisha wanamichezo wa Tanzania wanapata vifaa, maandalizi, na ushiriki wa uhakika kwenye majukwaa ya kimataifa.
Kupitia uwezeshaji wa klabu kama Singida Black Stars na timu mbalimbali za taifa, Tanzania sasa inazidi kujidhibiti kama kitovu cha vipaji na ushindani barani Afrika, ikikuza diplomasia ya michezo na kutoa ajira kwa vijana kupitia tasnia hiyo.
Post a Comment