MAPINDUZI YA SEKTA YA SUKARI: NEEMA KWA VIJANA, AJIRA NA USALAMA WA FEDHA ZA KIGENI





Serikali imebainisha kuwa mkakati wa kuongeza uwekezaji wa ndani na nje (FDI) katika sekta ya sukari mkoani Morogoro si tu suluhisho la uhaba wa bidhaa hiyo, bali ni injini ya kukuza ajira na kuimarisha uchumi wa taifa kuelekea Dira ya 2050.

Akizungumza katika ziara yake mkoani humo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amefafanua maana ya uwekezaji huo katika nyanja tano (5) muhimu.

Akizungumzia fursa za ajira na mustakabali wa vijana alisema uwekezaji wa kampuni kama Agro Tech, Kilombero, na Mkulazi Sugar unafungua milango ya ajira rasmi na zisizo rasmi kwa maelfu ya vijana. Kuanzia wataalamu wa kilimo (Agronomists), wahandisi wa mitambo ya viwandani, hadi vijana wa usafirishaji na biashara ndogondogo, mnyororo huu wa thamani unatoa jukwaa la vijana kujipatia kipato na ujuzi wa kisasa.

Pia alisema kwamba katika masuala ya ustawi wa jamii na maendeleo ya vijijini,kuwepo kwa miradi mikubwa ya sukari katika maeneo ya pembezoni kama Kijiji cha Mkulazi kunachochea ustawi wa jamii kupitia ujenzi wa barabara na upatikanaji wa nishati ya umeme,kupatikana kwa huduma za kijamii kama shule, vituo vya afya vinavyojengwa na wawekezaji kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) na kupatikana kwa soko la wakulima wadogo.

Tanzania ikiwa na mahitaji ya tani 700,000 za sukari kwa mwaka, huku pengo la uzalishaji likiwa bado ni changamoto, Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani kutaondoa utegemezi wa kuagiza sukari nje ya nchi, jambo ambalo mara nyingi husababisha mfumuko wa bei na kuyumba kwa upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu mezani.

Moja ya mafanikio makubwa ya mkakati huu ni kulinda akiba ya fedha za kigeni (Foreign Exchange Reserves). Kwa sasa, taifa hutumia mamilioni ya dola za Marekani kuagiza sukari nje. Kwa kuzalisha sukari ya kutosha ndani ya nchi, fedha hizo zitabaki nchini na kuelekezwa kwenye miradi mingine ya kimkakati kama Reli ya SGR na nishati.

Chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Serikali inalenga kufikisha Pato la Taifa (GDP) kwenye dola trilioni 1, ambapo asilimia 70 itatoka sekta binafsi. Uwekezaji huu wa sukari ni kielelezo cha namna sekta binafsi inavyoweza kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 bora barani Afrika katika uzalishaji wa chakula.

Ziara ya Prof. Mkumbo mkoani Morogoro inatoa picha ya wazi kuwa sekta ya sukari sasa inageuka kuwa "dhahabu nyeupe" itakayohakikisha usalama wa chakula, utulivu wa kiuchumi, na fursa pana kwa kizazi cha sasa na kijacho.


No comments