DIPLOMASIA NA AFYA YA AKILI: WATANZANIA TUPO TIMAMU PROPAGANDA ZA MITANDAONI ZIKIFELI



Katika hali inayozidi kuthibitisha kuwa Tanzania iko kwenye mstari sahihi wa maendeleo na ustawi wa jamii, ripoti mpya za kimataifa zimeendelea kuipandisha chati nchi yetu na kuumbua propaganda dhaifu zinazopikwa kwenye mitandao ya kijamii na wasiotakia mema taifa. 

Ripoti ya hivi karibuni ya Dunia ya Afya ya Akili ya mwaka 2025 iliyotolewa jijini Washington D.C na taasisi ya Sapien Labs kupitia mradi wa Global Mind Project, imeitaja Tanzania kushika nafasi ya tano duniani kwa kuwa na vijana wenye uimara mkubwa wa afya ya akili. 

Mafanikio haya makubwa yanaonyesha kuwa vijana wa Kitanzania wana utulivu wa ndani na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za maisha kuliko wenzao wa nchi zilizoendelea barani Ulaya, Amerika, na Asia, jambo linalozima kabisa kelele za wapotoshaji wanaojaribu kuonyesha kuwa nchi haina mwelekeo.

Utafiti huo ulioshirikisha zaidi ya watu milioni moja katika nchi 84, umebaini kuwa siri ya mafanikio ya vijana wa Tanzania inatokana na misingi imara ya kitamaduni na malezi. 

Tanzania imeongoza duniani katika kipimo cha imani na mambo ya kiroho, huku ikisifiwa kwa kuwa na wastani mkubwa wa umri wa vijana kuanza kutumia simu za mkononi ikilinganishwa na nchi nyingine. Hali hii ya kuchelewa kujiingiza kwenye ulimwengu wa kidijitali utotoni imewasaidia vijana wetu kulinda uwezo wao wa ufahamu na kudhibiti mihemko, tofauti na mataifa mengine ambapo matumizi ya mapema ya teknolojia yamesababisha kuporomoka kwa mahusiano ya kijamii na afya ya akili. Hii ni dhihirisho tosha kuwa wakati wachache wanatumia mitandao vibaya kuchafua taswira ya nchi, msingi mkuu wa vijana wa Kitanzania uko imara na hauyumbishwi na propaganda hizo.

Sambamba na heshima hiyo ya kiafya, Tanzania imeendelea kupata ushindi mwingine wa kidiplomasia katika nyanja ya haki za binadamu huko Geneva, Uswisi. 

Kamishna Mkuu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (HRC), Volker Turk, ametoa pongezi za wazi kwa Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kurejesha utulivu na kusafisha taswira ya nchi kimataifa. 

Katika kikao cha 61 cha baraza hilo, Kamishna Turk ameitaja hatua ya Tanzania kuunda Tume ya Uchunguzi kufuatia matukio ya Oktoba 29 kama kielelezo cha ukomavu wa uongozi unaojali misingi ya haki na uwajibikaji kwa kufuata taratibu za kimataifa. 

Hatua hii imepokelewa kama jibu la vitendo dhidi ya wale wanaodai kuwa nchi inakiuka misingi ya haki, ikionyesha kuwa serikali iko makini katika kusimamia usalama na haki za raia wake.

Ukweli huu wa kimataifa unadhihirisha kuwa Tanzania tuko bomba na tunaendelea kupaa, huku wasiotakia mema nchi yetu wakibaki na silaha yao pekee ambayo ni uzushi kwenye mitandao ya kijamii. 

Wakati wasambaza propaganda wakijaribu kupotosha umma kwa habari za kufikirika, ripoti za kisayansi na za kidiplomasia duniani zinathibitisha kuwa Tanzania ni nchi ya amani, yenye vijana wenye afya imara ya akili na serikali inayozingatia haki. 

Ni muhimu kwa kila mwananchi kutoingia kwenye mtego wa kufuata upotoshaji wa mitandaoni unaolenga kufadhaisha jamii, bali tujivunie hatua hizi kubwa zinazoifanya dunia iendelee kutuheshimu na kutuamini kama mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kote.

No comments