Viwanda viwili vyafungwa Kibaha kwa uchafuzi wa mazingira



Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas, ametoa amri ya kusitishwa kwa shughuli za uzalishaji katika viwanda viwili vilivyopo Kata ya Misugusugu, kutokana na kosa la kutiririsha maji taka yenye sumu na kinyesi kwenye makazi ya watu.

Viwanda vilivyofungiwa ni Radiant (vinywaji na vipodozi) na Fortune Paper Group Limited. Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa mtaa wa Kalabaka na Saeni kulalamika katika mkutano wa hadhara uliofanyika Shule ya Miomboni, wakibainisha kuwa maji hayo yanawasababishia magonjwa ya ngozi, kuvimba miguu, na kukausha mazao yao kama mahindi na mbogamboga.

Dkt. Nicas, aliyeambatana na jopo la wataalamu wa mazingira, alishuhudia ujenzi holela wa mifereji inayotoa harufu kali. "Tumefikia uamuzi huu baada ya kubaini viwanda hivi vimekaidi maelekezo ya Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zaidi ya mara tatu," alisema Dkt. Nicas.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa, Mrisho Mlela, amesisitiza kuwa uzalishaji hautaanza mpaka hapo mifumo ya kisasa ya kuchuja maji taka na mabwawa ya usalama yatakapojengwa. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Radiant, aliyetambulika kwa jina la Mahesh, amekiri makosa hayo na kuahidi kurekebisha mifumo hiyo ndani ya miezi mitatu.

Hatua ya kukifungia Kiwanda hicho imechukuliwa  Desemba  31 2025 baada ya wananchi kutoa kero hiyo kwenye mkutana wa hadhara  uliofanyika katika Viwanja vya  Shule ya  Miomboni  Kata ya Misugusugu  Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.

Dkt. Nicas baada ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali  za wananchi  aliamuru jopo la wataalam kwenda kuona hali halisi katika eneo linalolalamikiwa na wananchi.Katika eneo hilo Dkt. Nicas  alishuhudia  ujenzi holela wa mfereji unaolalamikiwa. 





Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha   Mrisho Mlela alikiri kuwa hali ambayo ameishuhudia siyo rafiki kwa wanachi na amesisitiza Mkurugenzi wa Kiwanda cha Radiant afuate maelekezo ambayo amepewa mara kadhaa na  Baraza la Uhifadhi wa Mazingira NEMC. Kiwanda hicho kimepewa maonyo mara tatu lakini hakuna utekelezaji.

"Wameonywa mara tatu  na yeye Mahesh  anakubali hilo lakini bado  tu hakuna utekelezaji " alisema  Dkt. Nicas.

Ofisa Mazingira Manispaa ya Kibaha Raheli  Ulaya amekiri kutoa onyo zaidi ya tatu lakini wamiliki hao hawajaonesha kutii.

Diwani wa Kata ya Misugusugu, Ally Simba pamoja na baadhi ya Wenyeviti wa Serikal za Mitaa   wamekiri kuwepo kwa uchafuzi huo wa mazingira na kwamba wamekuwa wakizungumza bila kufanyiwa kazi. 


No comments