UONGOZI wa Simba umesema kitendo cha mshambuliaji Denis Kibu kutokuwepo kambini hakiathiri mipango yao ila watamchukulia hatua za kinidhamu kwa kosa hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally Morogoro leo walipokwenda kuzindua jezi mpya
za msimu ujao.
Kibu aliongezewa mkataba wa miaka miwili utakaomalizika
Juni 2026 na kulipwa stahiki zake za kimkataba jambo ambalo hata meneja wake Carlos Mastermind amekiri mchezaji huyo
haidai Simba.
Ahmed alisema kutokuwepo kwa Kibu hakuathiri programu za Kocha
Mkuu Fadlu Davis kwa sababu wamefanya usajili kulingana na mahitaji ya timu.
“Kibu hadi sasa hajaungana na timu nchini Misri. Tulimuongeza
mkataba wa miaka miwili na amesaini kuitumikia Simba, tumemlipa fedha zote na
mahitaji yote aliyohitaji. Amelipwa kama kondakta, fedha alikabidhiwa mkononi
na kuondoka, hatuna deni na mchezaji bali Simba inamdai utumishi wake,” alisema
Ahmed.
Pia alisema baada ya kumaliza ligi alienda Marekani lakini
walimpa taarifa ya kambi, kupima afya na safari ya Misri, baadaye alisema hati
ya kusafiria imejaa.
“Kweli alirudi na kufuatilia hati yake lakini hakutokea
ofisini kwa ajili ya safari, alipotafutwa apeleke hati yake akasema ameenda
Kigoma, baada ya hapo zikaanza danadana za hapa na pale, tutaendelea kumtafuta
lakini jana tulisikia ameenda nje ya nchi,” alisema Ahmed.
Tetesi zinasema Kibu amevutiwa na Yanga na anaweza
kutambulishwa Siku ya Wananchi itakayofanyika Agosti 4 Uwanja wa Benjamin
Mkapa, Dar es Salaam.
Endapo atasajiliwa Yanga haitakuwa ajabu kwani meneja wake Carlos pamoja na
kukiri Simba kumlipa stahili zote alidai Yanga ndio waliotoa dau kubwa.
Hata hivyo Carlos anasema mchezaji
huyo amepata mwaliko wa moja ya klabu nchini Norway.
“Ni kweli Kibu hajajiunga na timu Misri kwa sasa yupo
Ulaya, ninachojua hawadai Simba wamemalizana na suala la kwanini hajajiunga na
wenzake nchini Misri, Simba wana uwezo wa kujibu hilo,” alisema Carlos.
No comments:
Post a Comment