Pages

Wednesday, July 17, 2024

Aisha Masaka aula England




MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Aisha Masaka amesajiliwa na klabu ya 
Brighton & Hove Albion FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake England.

Katika taarifa iliyotolewa na klabu hiyo yenye makazi yake Crawley, United Kingdom imemsajili Aisha Masaka kutoka BK Hacken kwa masharti ambayo hayajawekwa wazi, kwa kuzingatia taratibu za kawaida za udhibiti.

“Tunayofuraha kutangaza kumsajili mshambuliaji Aisha Masaka kutoka BK Hacken kwa masharti ambayo hayajawekwa wazi, kulingana na taratibu za kawaida,” alisema  Zoe Johnson, Mkurugenzi Mkuu wa soka la wanawake na wasichana, na kuongeza, "Tuna furaha kumkaribisha Aisha, Brighton.

"Ameshindana kwa kiwango cha juu nchini Uswisi akiiwakilisha Hacken kwenye Ligi ya Mabingwa (UEFA).

"Yeye ni mshambuliaji ambaye anatawala mpira na mfungaji wa asili. Tunatazamia kumkaribisha Albion kabla ya msimu mpya.”

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 alijiunga na Hacken mwaka 2022 akitokea Yanga Princess  na pia amewahi kuichezea Alliance FC ya Mwanza.

Katika misimu miwili aliyokaa Hacken, aliwasaidia kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi ya Uswisi na walifika robo fainali ya UEFA msimu uliopita kabla ya kushindwa na PSG.

Katika kipindi chake cha Ligi Kuu ya Tanzania, alishinda mfungaji bora katika kampeni za 2020/21 baada ya kuifungia Yanga Princess mabao 35 katika mechi 20.

Katika ngazi ya kimataifa ameichezea Tanzania mechi 15, akifunga mabao tisa tangu alipoanza kucheza mwaka 2021.

Kwenye michuano ya Kombe la COSAFA ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 alikuwa kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa na yeye kumaliza mfungaji bora.

Pia ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha Tanzania kilichofuzu kucheza michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wanawake (AFCON 2024) itakayofanyika Morocco mwakani baada ya kusogezwa mbele.

Masaka anakuwa mchezaji wa kwanza kwa wanawake kucheza Ligi Kuu England lakini wa pili akitanguliwa na Mbwana Samatta aliyecheza Aston Villa mwaka 2020.

Wachezaji wengine wa Twiga Stars wanaocheza nje na klabu zao kwenye mabano ni Clara Luvanga (Al Nassr- Saudia), Enekia Kasonga (Flames-Saudia), Julietha Singano (Juavares - Mexico), Opah Clement (Beskitas - Uturuki), Diana Msewa (Amed Spor - Uturuki) na wengine wanaocheza nchi za Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment