Pages

Friday, September 8, 2023

TFF yatambulisha nembo ya Championship

 


Na Rahel Pallangyo

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema watalinda haki walizouzia Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa mujibu wa mkataba waliosaini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura, Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa nembo rasmi ya ligi ya Championship ambayo mdhamini wake ni NBC.

"TFF tuna furaha kupata mdhamini mmoja kwenye bidhaa zetu tatu kwa wakati mmoja hivyo nawahakikishia NBC kuwa haki tulizowauzia tutazilinda kwa mujibu wa mikataba tuliyosaini,” alisema Wambura.

Naye Mkurugenzi wa Wateja Binafsi wa NBC, Elibariki Masuke alisema katika mkataba waliosaini Agosti 11 na TFF kipengele cha tatu kinazungumzia udhamini wa ligi ya Championship.

“Leo hii tuko hapa kutimiza sehemu ya jukumu letu la kimkataba na udhamini kuzindua chapa mpya ya Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) na kuipa jina la NBC Championship League kama sehemu ya uzinduzi wa mashindano haya ya soka yanayotarajiwa kuanza hivi karibuni,” alisema.

Agosti 11, mwaka huu jijini Tanga, NBC ilitangaza kuingia makubaliano ya kuongeza muda wa kudhamini Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kipindi cha miaka mitano mingine kuanzia msimu wa mwaka 2023/24 hadi mwaka 2027/2028 na kuongeza Ligi ya Championship na First League.

Mkataba wa awali wa udhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa miaka mitatu ulikuwa wa thamani ya Sh bilioni tisa ambapo utamalizika msimu ujao wa mwaka 2023/2024 na sasa wameingia makubaliano mapya ya mkataba wenye thamani ya Sh bilioni 32.56.

Wakati wakisaini makubaliano hayo NBC kupitia Mkurugenzi Mtendaji, Theobald Sabi, alisema

Ligi ya Championship na First league zote zitapewa majina ya benki hiyo baada ya utaratibu kukamilika.

NBC Championship League inashirikisha timu 16 na inatarajiwa kuanza kesho kwa kuchezwa michezo mitano katika viwanja vya miji tofauti na mingine mitatu itachezwa keshokutwa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment