Pages

Tuesday, September 12, 2023

DK NDUMBARO AZINDUA BODI MBILI, AZIPA JUKUMU LA KUONGEZA MAPATO

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro akizungumza kwenye hafla ya kuzindua bodi za COSOSTA na Bodi ya Filamu

Naibu Waziri Hamis Mwinjuma

Katibu Mkuu Said Yakubu

Waziri Dk Ndumbaro, Naibu Hamisi Mwinjuma, Katibu Mkuu, Said Yakub na wajumbe wa bodi za COSOSTA na Bodi ya Filamu


Na Rahel Pallangyo

Wajumbe ya Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOSTA) na Bodi ya Filamu Tanzania wametakiwa kuhakikisha sekta ya sanaa inatoa ajira za kutosha na wananchi wanafaidi matunda ya kazi zao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro wakati akizindua bodi za taasisi hizo  Dar es Salaam leo 

“Wizara hii ina dhamana kubwa na watekelezaji wa kazi zake ni taasisi zinazosimamiwa na Bodi, kazi yenu ni kuhakikisha taasisi mnazozisimamia zinakua kiuchumi ili kukuza Pato la Taifa na uchumi wa wadau wa sekta yetu ya Sanaa ambayo imekua kwa asilimia 19 ”amesisitiza Waziri Dkt. Ndumbaro.

Awali akimkaribisha Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Damas Ndumbaro kuzindua Bodi hizo, Naibu Waziri, Hamis Mwinjuma amewahimiza wajumbe wa bodi hizo kutekeleza wajibu wao ili kuleta uhalisia na utofauti wa utendaji wa kazi wa taasisi hizo kabla ya uteuzi na baada ya kuingia madarakani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesisitiza kuwa sekta ya Sanaa nchini imekuwa na Tanzania ni ya pili Afrika ambapo inazalisha filamu 2000 kwa mwaka sawa na wastani filamu sita kwa siku.

Ameongeza kuwa Sekta hiyo imefanikiwa kuzalisha wingi wa filamu na kuwahimiza wajumbe hao kushirikiana na taasisi wanazoziongoza ili kujikita kuzalisha kazi bora ambazo zitakuwa chanzo adhimu cha mapato kwa wasanii na taifa kwa ujumla.

Aidha, Yakubu amezitaka Bodi hizo kuhakikisha Taasisi zinaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka nje ya nchi kupitia kazi za Sanaa ambazo zinazooneshwa katika nje ya mipaka ya Tanzania na kuongeza ushirikiano na Taasisi zenye majukumu yanayofanana nayo.

Wakizungumza kuhusu uzinduzi wa Bodi hizo,  Mwenyekiti wa Bodi ya Hakimiliki Tanzania (COSOSTA)  Victor Tesha na Mwenyekiti wa Bodi ya Filamu Dk. Mona Mwakalinga wamesema watahakikisha linakuwepo jukwaa ndani la kuonesha na kusambaza kazi za Sanaa ndani na nje ya nchi kama ilivyo majukwaa mengine na kusisitiza watasimia kuongeza  ubora katika filamu za Tanzania ili zipate soko kubwa zaidi duniani.

No comments:

Post a Comment