Pages

Friday, February 9, 2018

YANGA DHIDI YA MAJIMAJI, AZAM FC DHIDI YA KMC KOMBE LA FA

YANGA itasafiri hadi Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya mchezo wa hatua ya 16 bora ya mashindano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) kucheza na wenyeji, Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji.
Katika hatua ya 32, Yanga waliponea chupuchupu kuondolewa baada ya kusawazisha bao dakika ya mwisho kwa penalti ya Obrey Chirwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kupata sare ya 1-1 na Ihefu ya daraja la pili kabla ya kwenda kusonga mbele kwa penalti pia.
Katika droo iliyopangwa jana mubashara katika Kituo cha runinga cha Azam kilichopo Tabata, Dar es Salaam, mechi za hatua ya 16 bora zitachezwa kati ya Februari 22 na 25.
Azam FC watacheza na KMC ya Kinondoni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Stand United itaikaribisha Dodoma FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga na Buseresere itaialika Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Kahama.
Mechi nyingine JKT Tanzania watakuwa wenyeji Ndanda FC Uwanja wa Mbweni, Dar es Salaam, Kiluvya United itacheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Filbert Bayi, Kibaha, Pwani.

Singida United itaikaribisha Polisi Tanzania katika Uwanja wa Namfua na Njombe Mji itacheza na Mbao FC Uwanja wa Saba Saba, Njombe. 
Bingwa wa mashindano ataiwakilisha nchi katika mashindano ya kombe la shirikisho barani Afrika na hadi sasa kombe hili halina mwenyewe baada ya bingwa mtetezi Simba kuondolewa katika hatua ya 64.

No comments:

Post a Comment