KAMATI ya uendeshaji wa ligi imeteua wajumbe
watatu kuchunguza kiwango cha uchezeshaji cha mwamuzi Israel Nkongo na
kuwasilisha taarifa yake kwa ajili ya hatua zaidi.
Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi
ya Ligi (TPBL) Boniface Wambura alisema kuwa Nkongo alichezesha mchezo dhidi ya
Mbeya City na Kagera na kumalizika kwa sare ya 1-1 licha ya kuwa hakuna timu
iliyolalamika kamati imeamua kufanya hivyo ili ichukue hatua stahiki.
“Kamati hiyo itapitia mkanda wa mechi hiyo na
kuchunguza kiwango cha uchezeshaji cha Nkongo na kuwasilisha taarifa kwa ajili
ya hatua stahili maana baada ya mchezo kumalizika mashabiki walitaka kumpiga
lakini askari waliwadhibiti,” alisema Wambura
Katika mchezo huo Mbeya City imepigwa faini ya
sh. 500,000 kwa kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani katika mechi hiyo
iliyochezwa Januari Mosi, 2018, Mbeya, kitendo ambacho ni kinyume na Kanuni ya
14(14) ya Ligi Kuu na adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49).
Kocha wa Mbeya City, Ramadhani Mwazurimo
amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na kosa la
kuondolewa kwenye benchi na mwamuzi baada ya kumtolea lugha ya kashfa katika
mechi hiyo iliyochezwa Januari 14, 2018 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya.
Pia klabu ya Mbeya City imepigwa faini ya sh.
500,000 kutokana na washabiki wake kuingia uwanjani na kumzonga mwamuzi kwa
madai alikataa kutoa penalti kwa timu hiyo.
Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana
na kukataa wachezaji wake wakaguliwe ndani kwa madai kuwa chumba kimepuliziwa
dawa katika mechi hiyo iliyofanyika Januari 18, 2018 Uwanja wa Majimaji mjini
Songea na wamepewa siku saba kuthibitisha madai yao.
Mtunza Vifaa wa Singida United FC, Mussa Rajab
amefungiwa mwezi mmoja na kupigwa faini ya sh. 300,000 kutokana na kuingia
uwanjani baada ya filimbi ya mapumziko na kumlalamikia mwamuzi wakati wa mchezo
dhidi ya Simba uliochezwa Uwanja wa Taifa Januari 18.
No comments:
Post a Comment