Pages

Sunday, October 8, 2017

TFF YAWALILIA MWAMUZI TSHIKUNGU NA MCHEZAJI WA ZAMANI MAJHAM

Image result for WALLACE KARIA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya wanafamilia wawili wa soka vilivyotokea Oktoba 5, 2017 kwa nyakati tofauti.

Akizungumza Ofisa habari wa TFF Alfred Lucas alisema Rais wa TFF Wallace Karia amesikitishwa na taarifa aliyekuwa mchezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’,  Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, pamoja na Afrika Mashariki miaka ya 1950 na 1960, Abdul Majham na Mwamuzi wa Daraja la Kwanza Mirambo Tshikungu.

“Hakika nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo hivi. Ni mshtuko mkubwa sana katika familia ya mpira wa miguu hapa Tanzania, natambua pia ni majonzi makubwa kwa familia za marehemu,” alisema Rais Karia.

“Familia, ndugu, jamaa, marafiki, majirani wawe na moyo wa subira baada ya ndugu zetu kutangulia mbele ya haki. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwingi wa Rehema, basi tumuombe awe na msamaha kwa ndugu zetu,” aliongeza.

Abdul Majham aliyefariki dunia huko Visiwani Zanzibar na mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Vikokotoni ya Zanzibar, pia aliwahi kuichezea klabu Bingwa ya kwanza ya Tanzania, Cosmopolitan ya Dar es Salaam.
Kuhusu Tshikungu, alifariki dunia jioni ya Oktoba 5, katika hospitali ya Peramiho Ruvuma ambako alihamishiwa akitokea hospitali ya Ikonda iliyoko Makete mkoa wa Njombe.

Mwenendo wa uchezeshaji wake ulikuwa na tija kwani rekodi zinaonesha hajawahi kufungiwa au kupewa onyo na mchezo wa mwisho kucheza ni kati ya Majimaji ya Songea na Yanga uliofanyika Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma msimu uliopita.
Tshikungu alizikwa jana nyumbani kwake Mbeya na ameacha mke na watoto watatu mmoja kati yao ni wa kiume.



No comments:

Post a Comment