Pages

Tuesday, October 10, 2017

MALALAMIKO YA PEPSI YAMEKATALIWA

Malalamiko ya Pepsi dhidi ya Madini kuwa timu hiyo ilimtumia mchezaji Shabani Imamu kwenye mechi yao ya Ligi Daraja la Pili (SDL) iliyochezwa Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa  Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini wakati akiwa na adhabu ya kutumikia kadi nyekundu yamekataliwa.
Kamati imebaini kuwa mchezaji huyo alishatumikia adhabu ya kukosa mechi moja wakati wa mchezo wa SDL kati ya Madini na JKT Oljoro uliochezwa Februari 6 mwaka huu.
Mchezaji huyo alioneshwa kadi ya pili ya njano msimu uliopita kwenye mechi kati ya Madini na AFC iliyofanyika Januari 31 mwaka huu, na kukosa mechi moja iliyofuata kati ya Madini na JKT Oljoro ya Februari 6 mwaka huu, hivyo kuwa halali kwenye mechi ya Pepsi na Madini iliyochezwa Septemba 30 mwaka huu.
Kocha Msaidizi wa Area C United, Omarooh Omari amesimamishwa kukaa kwenye benchi la timu yake wakati akisubiri suala lake la kumpiga kiwiko mchezaji wa Nyanza FC kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.

Alimpiga kiwiko mchezaji wa Nyanza, Rajab Adam alipokuwa akikimbilia mpira uliopita karibu yake. Pia dakika ya 78 alianzisha tena vurugu na Mwamuzi kumtoa kwenye benchi la ufundi lakini aligoma kutoka hadi alipotolewa na askari polisi.
Alifanya vitendo hivyo vya utovu mkubwa wa nidhamu wakati wa mechi kati ya Ligi Daraja la Pili kati ya timu yake na Nyanza iliyochezwa Oktoba 1 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyerere uliopo Mbulu mkoani Manyara.
Uamuzi wa kumsimamisha umefanywa kwa kutumia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Pili.

No comments:

Post a Comment