Pages

Tuesday, October 10, 2017

KOCHA TOTO AFRICANS AZUIWA KUKAA BENCHI

Kocha wa Toto Africans, Almasi Moshi amezuiwa kukaa kwenye benchi la timu yake kutokana na kutokidhi matakwa ya Kanuni ya 72(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu benchi la ufundi.
Kwa mujibu wa Kanuni hiyo, Kocha Mkuu wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza anatakiwa kuwa na Leseni ya chini kuanzia Daraja C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). 

Klabu ya Mvuvumwa FC imepigwa faini ya sh 100,000 (laki moja) kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) ikiwa na maofisa wawili tu badala ya wanne wakati wa mechi namba 5 ya Kundi A la Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Kiluvya United iliyochezwa Septemba 22 mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo, na kitendo chao cha kuwa pungufu kwenye pre match meeting ni kukiuka Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza. 

Nayo Toto Africans imepigwa faini ya sh 100,000 (laki moja) kwa kuhudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) ikiwa na maofisa watatu badala ya wanne wakati wa mechi namba 10 ya Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Transit Camp FC iliyochezwa Septemba 29 mwaka huu katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza. 

Adhabu dhidi ya klabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo, na kitendo chao cha kuwa pungufu kwenye pre match meeting ni kukiuka Kanuni ya 14(2b) ya Ligi Daraja la Kwanza.

JKT Oljoro imepigwa faini ya s 100,000 (laki moja) kwa timu hiyo kufika uwanjani ikiwa imechelewa kinyume na Kanuni ya 14(9) ya Ligi Daraja la Kwanza. Ilifanya kosa hilo kwenye mechi namba 5 ya Kundi la Ligi Daraja la Kwanza katika mechi dhidi ya Pamba iliyofanyika Septemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Mchezaji Hussein Nyamandulu wa Transit Camp amesimamishwa kucheza wakati akisubiri suala lake la kufanya vurugu kwenye benchi la Toto African kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF.

Nyamandulu aliyekuwa amevaa jezi namba 10 alifanya vurugu hizo baada ya mechi dhidi ya Toto Africans iliyofanyika Septemba 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kumalizika. Mchezaji huyo amesimamishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza.

Timu ya Polisi Dar imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi (pre match meeting) wakati wa mechi yao namba 7 dhidi ya KMC iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu Chamazi Complex, Dar es Salaam.
Kitendo hicho ni kinyume na Kanuni 14(2) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo, na adhabu dhidi yao imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichopita ilipitia taarifa mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2017/2018 zinazoendelea hivi sasa.
Dodoma FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na timu hiyo kuonesha vitendo vinavyoashiria ushirikina kwa kumwaga vitu kwenye mlango wa kuingilia uwanjani, na pia golikipa namba pili aliweka kitu golini.
Timu hiyo ilifanya vitendo hivyo kabla ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Biashara United Mara iliyochezwa Septemba 23 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.Adhabu yao ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
Mwamuzi Youngman Malagila ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi wa Ligi Daraja la Kwanza kutokana na kuchezesha chini ya kiwango mechi kati ya Rhino Rangers FC na JKT Oljoro FC ya Arusha iliyofanyika Septemba 30, 2017 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Uamuzi dhidi ya Mwamuzi huyo umezingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Hivyo, amerejeshwa kwenye Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa hatua zingine.
Nao waamuzi Steven Patrick (Mwamuzi wa Kati) na Msaidizi wake Adrian Kalisa wameondolewa kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza kutokana na kuchezesha chini ya kiwango mechi kati ya Pamba na Biashara United Mara iliyofanyika Oktoba 2, 2017 katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Uamuzi dhidi ya Mwamuzi huyo umezingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi. Alama walizopata waamuzi hao kwenye mechi namba 12 haziwaruhusu kuchezesha Ligi hiyo.

No comments:

Post a Comment