Pages

Wednesday, September 13, 2017

TANZANITE YAONDOKA NA MATUMAINI KIBAO







NAHODHA wa timu ya Taifa ya soka ya Wasichana (U-20) ‘Tanzanite’  Wema Richard amewaahidi Watanzania kurudi na ushindi katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Dunia dhidi ya Nigeria unaotarajiwa kuchezwa Abuja Jumamosi.
Hayo aliyasema leo wakati akikabidhiwa bendera ya Taifa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Yusuph Singo katika Ukumbi wa Mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Karume, Dar es Salaam.
Wema alisema kikosi chao ambacho kipo chini ya kocha Sebastian Nkoma kimepata maandalizi ya muda mrefu japo hawakupata mechi ya kirafiki ya kimataifa lakini wamejiandaa kupambana ili warudi na ushindi.
“Kocha amemaliza kazi yake kilichobaki na sisi wachezaji kuonesha kwa vitendo kile tulichofundishwa na sisi tupo tayari kwa kazi na kauli mbiu yetu ni ‘kazi kazi,” alisema Wema.
Akizungumza kabla ya kukabidhi bendera Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Dk. Yusuph Singo aliwaambia wachezaji hao Watanzania wanapenda mpira hivyo wanategemea ushindi.
“Timu yenu ni nzuri japo sijabahatika kuwaona mkicheza kama Tanzanite ila baadhi nimewaona mkicheza kama Makongo, Mlandizi na timu nyingine lakini naamini mtakwenda kufanya vizuri,” alisema Dk. Singo.
Pia Singo aliwaambia wako sokoni hivyo wakacheze kwa kuonesha vipaji vyao kwani wanaweza kupata timu za kucheza au kufanya majaribio kama ilivyokuwa kwa Serengeti boys.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao alikiri timu hiyo kukosa michezo wa kirafiki wa kimataifa lakini akasema TFF imejitahidi kuwalipa wachezaji hao posho zote kuanzia walipoanza kambi.
“Kama TFF tumetimiza wajibu kwa kuwalipa posho zote mnazodai na hata posho za nje mkuu wa msafara atakabidhiwa kwani zipo tayari na nyie wachezaji pamoja na benchi la ufundi mnakwenda kutimiza wajibu,” alisema Kidao

No comments:

Post a Comment