Pages

Sunday, September 24, 2017

TAMASHA LA SANAA NA UTAMADUNI LA KIMATAIFA BAGAMOYO LADHAMIRIA KULETA TIJA KWA WASANII WA NDANI NA NJE YA NCHI


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (wapili kulia) akimsikiliza mjasiriamali wa kazi za sanaa kutoka Dar es Salaam Bibi. Magreth Kabonge (kushoto) alipotembelea banda lake kabla ya kufungua Tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi ya TaSUBa. Kulia ni Mtendaji Mkuu Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akiangalia moja ya kazi za sanaa iliyotengenezwa na mbunifu kutoka Arusha Bi. Joyce Lema (kushoto) alipotembelea banda lake kabla ya kufungua Tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi ya TaSUBa.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akionyesha picha yenye mfano wa sura yake iliyochorwa na kalamu ya risasi na mwanafunzi kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Bw. Baraka Jeje (kushoto) alipotembelea banda lake kabla ya kufungua Tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi ya TaSUBa.
Baadhi ya wanafunzi kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) wakiimba wimbo wa taifa wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi hiyo.
Wanafunzi kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) wakicheza ngoma wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi hiyo.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi ya TaSUBa.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (watatu kulia) akishirikiana na Mtendaji Mkuu kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo Dkt. Herbert Makoye (wapili kulia), Katibu Tawala Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Erica Yegelea (watatu kushoto), Mtendaji Mkuu Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Godfrey Mngereza (kulia) na Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Mhe. Shukuru Kawambwa (wapili kushoto) kukata keki kuashiria uzinduzi wa Tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi ya TaSUBa. Picha na: Genofeva Matemu - WHUSM 

 
Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imeagizwa kukaa na kufanya tathmini ya kina kuandaa mpango mkakati mzuri wa namna ya kuliendesha tamasha la Sanaa na Utamaduni ili liweze kuwa na tija zaidi kwa wasanii na Taasisi kwa ujumla.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa tamasha la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa Bagamoyo jana katika Taasisi hiyo mjini Bagomoyo. “Tangu kuanzishwa kwa tamasha hili mwaka 1982, Tamasha limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wasanii na wadau wa sanaa ndani na nje ya nchi na wananchi kwa ujumla hivyo ni vyema Bodi ya ushauri ya TaSUBa ikapanga mikakati yenye tija zaidi kwa maslahi ya wasanii wetu na Taasisi yetu” amesema Mhe. Mwakyembe.

Aidha Mhe. Mwakyembe ameipongeza Bodi, Menejimenti, wafanyakazi na wanachuo wote wa TaSUBa kwa kazi kubwa wanayoiofanya kila mwaka ya kuandaa na kuendesha Tamasha hilo kwa kipindi cha miongo mitatu na nusu mfululizo na kuwataka kutembea kifua mbele kwa rekodi hiyo iliyotukuka ndani na nje ya nchi.

Mhe. Mwakyembe amesema kuwa lengo la Tamasha hilo ni pamoja na kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa mtanzania, kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa TaSUBa wanalitumia kupima kiwango chao cha umahiri katika sanaa kwa mwaka, kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali kutoka sehemu tofauti duniani ili kuonyesha utajiri wao wa sanaa na utamaduni, pamoja na kutengeneza jukwaa ambalo ni kiungo cha kujenga mahusiano ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho ya sanaa na kubadilishana uzoefu na uwezo katika kuendeleza tasnia ya sanaa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbert Makoye amesema kuwa taasisi inajivunia mafanikio makubwa wanayoendelea kuyapata kupitia tamasha hilo kwani kwa sasa tamasha linajumuhisha wasanii wa ndani na nje ya nchi pamoja na wanafunzi waliosoma katika taasisi hiyo miaka ya nyuma na waliopo mafunzoni.

Aidha Dkt. Makoye amewashukuru wakazi wa Bagamoyo kwa ushirikiano ambao wamekua wakiuonyesha katika kushirikiana na Taasisi kuendeleza na kuthamini sanaa na utamaduni wa mtanzania.

Naye Chifu wa Unyanyembe na Mwenyekiti wa Chama cha Machifu Tanzania Mhe. Msagati Fundikira amewapongeza watendaji wa TaSUBa kwa kutoa wataalamu wazuri katika fani ya sanaa na utamaduni kwani kwa ufanya hivyo wamekua wakiendeleza na kudumisha utamaduni wa mtanzania kwa vizazi vya leo.

Tamasha hili la 36 la Sanaa na Utamaduni la kimataifa la Bagamoyo lenye kauli mbiu isemayo “Sanaa na Utamaduni katika kupiga vita madawa ya kulevya” limeshirikisha wasanii kutoka Kenya, Ufaransa, Uingereza, Zimbabwe na Mayyote na kuudhuriwa na mabalozi mbalimbali akiwemo balozi wa Malawi, balozi wa Palestina, balozi wa uholanzi, pamoja na wawakilishi kutoka ubalozi wa Zambia, Saudi Arabia, Msumbiji, Japani, Ujerumani, Marekani, India, Shirikisho la Urusi, Angola na Kenya.

No comments:

Post a Comment