Pages

Sunday, September 24, 2017

MTIBWA YAJIIMARISHA KILELENI, SINGIDA UNITED YAISHUSHA SIMBA



MTIBWA Sugar imeendelea kukaa kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara licha ya leo kutoka sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting kwenye mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mabatini, Pwani.
Kwa matokeo hayo Mtibwa Sugar wamefikisha pointi 10 baada ya kucheza michezo minne na kushinda michezo mitatu huku nafasi ya pili Singida United ikiwa na pointi tisa.
Ruvu Shooting walitanguliaji kufunga bao dakika ya kwanza likifungwa na Zuberi Dabi lakini dakika ya 25 mshambuliaji Stahimili Mbonde aliisawazishiwa Mtibwa Sugar.
Katika dimba la Jamhuri Dodoma Singida United waliweza kuutumia vema uwanja wa nyumbani kwa kuifunga Kagera Sugar bao 1-0, lililofungwa na Tafadzwa Kutinyu kwa penalti dakika ya 89.
Huu ni mchezo wa nne kwa Kagera Sugar, kikosi kinachonolewa na kocha kijana mzawa Mecky Maxime kikipoteza.
Stand United ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga  iliifunga Mbeya City mabao  2-1, mabao ya Stand yalifungwa na Kisatya Sahan dakika ya 53  na la pili lilifungwa na Ally Ally dakika 62 na bao pekee la Mbeya City lilifungwa na Mohamed Samatta dakika ya 57
Baada ya kumalizika kwa mzunguko wa nne ligi inatarajiwa kuendelea tena Septemba 30 ambapo kutachezwa michezo saba na mchezo mmoja utachezwa Oktoba Mosi.
Baada ya hapo timu ya Taifa ya soka itaingia kambini kwa ajili ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Malawi unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 7 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment