Pages

Saturday, August 26, 2017

YANGA KUSHUKA UWANJANI KESHO MATOLA AAPA KUFA NAYO






MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara Yanga kesho wanaingia uwanjani kuwakabili Lipuli FC ya Iringa katika mchezo wa wao wa kwanza wa ligi hiyo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.
Yanga itaendelea kuwakosa nyota wake Obrey Chirwa na Pius Buswita kutokana na kesi tofauti, ambapo Buswita amesimamishwa mwaka mmoja baada ya kubainika kusaini mara mbili Simba na Yanga.
Chirwa licha ya kuwa ni majeruhi lakini pia, alisimamishwa na Kamati ya Usimamizi ya Uendeshaji Bodi ya ligi ile ya masaa 72 ya msimu uliopita baada ya kumpiga mwamuzi Ludovic Charles katika mchezo wa kumaliza msimu dhidi ya Mbao FC hivyo, anasubiri suala lake kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Yanga imekuwa haitabiriki katika mechi zake za mwanzo kuna wakati huanza vibaya na wakati mwingine huanza vyema. Lakini mara nyingi imekuwa ikifanya vizuri katika mechi za nyumbani.
Lipuli  ni timu iliyopanda msimu huu na ina kocha mzoefu wa ligi Seleman Matola ambaye anaifahamu Yanga  vizuri. Hautakuwa ni mchezo rahisi kwa kila mmoja ingawa Yanga inaweza ikapewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na aina ya kikosi ilichosajili msimu huu.
Baadhi ya nyota wa Yanga waliong’ara katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba JUmatano, Ibrahim Ajib, Donald Ngoma, Gadiel Michael, Thaban Kamusoko na Papy Kabamba Tshishimbi wanatarajiwa kuendeleza makali yao iwapo watapangwa.
Lakini sio mchezo wa kudharau hasa Lipuli FC kwani wanajua wanakutana na timu ya aina gani hivyo, watacheza kwa juhudi kujionyesha kuwa hata wao ni bora.
Kocha wa Yanga George Lwandamina alisema maandalizi yanakwenda vizuri na wamejipanga kuhakikisha pointi tatu zinabakia kwao.
Alisema kinachotakiwa kwa wachezaji wake ni kujituma na kuanza vyema michuano hiyo.
Kocha Selemani Matola alisema Yanga ni timu kubwa na nzuri hivyo anaamini mchezo utakuwa mgumu kwani mapungufu ya Yanga na mazuri ameyaona katika mchezo wa Ngao ya Jamii
Alisema wamefanya maandalizi ya kutosha watahakikisha wanapambana na kupata pointi tatu ugenini

No comments:

Post a Comment