Pages

Thursday, August 31, 2017

RATIBA YA LIGI KUU KUFUMULIWA YOTE, YAUNDIWA KIKOSI KAZI




SHIRIKISHO  la Soka Tanzania (TFF) limemwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB) likimtaka kuwaajibisha maofisa waliyohusika kupanga ratiba ya Ligi Kuu bila kufuata matukio ya mwaka ya kisoka ya nyumbani na kimataifa.
Akizungumza na wandishi wa habari jana, Kaimu Katibu Mkuu alisema ratiba ya ligi ilitakiwa kukidhi mechi za kimataifa za Taifa Stars kulingana na kalenda ya FIFA, mechi za mashindano za CAF na FIFA, mashindano ya Mapinduzi, mashindano ya Federation (Azam Federetion Cup ) na mashindano mengine ambayo yapo kwenye kalenda ya TFF.
 “Baada ya ligi kuanza na kusimama Rais Wallace Karia ameniagiza kumwandikia Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi kumchukulia hatua za kinidhamu wataalamu wa kupanga ratiba ama kwa uzembe au kwa kutokujua, ”
“Ligi baada ya kuanza na kuchezwa mzunguko mmoja ililazimika kusimama kupisha mchezo wa kirafiki wa kimataifa wa Taifa Stars dhidi ya Botswana hali iliyozua maswali juu ya weledi na utendaji kazi wa TFF,” alisema Kidao
Alisema kati ya mambo ambayo yamekuwa yakisemwa vibaya ni juu ya ratiba ya ligi kuu kupanguliwa na kudai yeye kama kocha na mkufunzi anajua athari gani kitaalamu ambazo timu zinapata achilia mbali kujiandaa kiuchumi.
Alisema Bodi ya ligi ni chombo cha TFF ambacho wamekipa majukumu ya kusimamia ligi ili TFF ijikite kwenye maendeleo  ya soka kwani wanaamini wasingeweza kusimamia ligi na wakati huo huo wajikite kwenye maendeleo.
Pia Kidao alisema kwa kutambua umuhimu wa kuwa na ratiba ambayo ligi inachezwa mwanzo mwisho bila kubadilishwa kwa nchi za wenzetu wanavyofanya ameunda kikosi kazi cha watu wanne ambao kitaipitia ratiba yote na kuipanga na kuiwasilisha Septemba 2.
“TFF hairidhishwi na ratiba iliyopo kwani ina mapungufu mengi, hivyo nimeunda kikosi kazi cha wataalamu wanne kuifanyia kazi na tunaamini baada ya marekebisho hayo haitabadilika tena mpaka msimu uishe labda litokee  kwa jambo ambalo lipo nje ya uwezo mwanadamu kama mvua,” alisema Kidao.
Kidao alisema baada ya udhaifu huu kutokea ratiba ya ligi haitatoka bila kusainiwa na Katibu Mkuu wa TFF ili kulinda heshima ya taasisi hiyo kwani pia ratiba iliyotoka kuna timu zinamaliza mechi nne ugenini jambo ambalo halina ushindani sawa.
Mtandao huu ulimtafuta Mtendaji wa Bodi ya Ligi, (TPLB) Boniface Wambura kujua ni hatua gani alizochukua juu ya watendaji wa bodi hiyo ambao wanalalamikiwa na kudai hajapata barua kutoka TFF akipata ataeleza hatua alizochukua.
Pia nilitaka kujua kama anaridhika na ratiba iliyotoka bila kuzingatia kalenda ya FIFA na kusema upangaji wa ratiba siyo kazi ya professionalism.
Baada ya ligi kuu kuanzia Agosti 26 kuanza ligi ilisimama baada ya kuchezwa mzunguko mmoja hali iliyozua maswali huku tuhuma zingine zikitupwa kwa uongozi mpya wa TFF ambao uliingia madaraka mapema Agosti.
Kwa miaka kadhaa TPLB ambayo ndiyo waandaji wa ratiba za ligi zote imekuwa ikilalamikiwa kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara na kugeuka kero miongoni mwa wadau wa soka nchini.

No comments:

Post a Comment