Pages

Tuesday, August 29, 2017

MBAO YAPATA UDHAMINI WA SHILINGI MILIONI 140


Mwenyekiti wa Mbao FC (kulia) Solly Zephania Njashi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya GF Trucks & Equpments Imran Karmali (katikati) wakionesha  mkataba baada ya kusaini kuidhamini Mbao kwa mwaka mmoja katika hafla iliyofanyika Dar es Salaam. Kushoto ni Ofisa Masoko wa GF Trucks, Kulwa Bundala (Picha na Rahel Pallangyo)





MBAO FC ya Mwanza imeingia mkataba wa udhamini wa mwaka mmoja na kampuni ya GF Trucks & Equpments wenye thamani ya sh. milioni 140.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Ofisa Masoko wa kampuni hiyo, Kulwa Bundala alisema katika mkataba huo Mbao itapata basi lenye  thamani ya sh. milioni 70 pamoja na fedha taslimu sh. milioni 70.
“Tumeingia mkataba wa mwaka mmoja na Mbao kwa sababu tumeona jitihada zao katika mchezo wa soka na tunasaini mkataba  wenye thamani ya shilingi milioni 140 na ndani ya mkataba huo tunawapatia basi lenye thamani ya shilingi milioni 70 na milioni 70 nyingine tutawakabidhi fedha taslimu,”.
Pia Bundala aliipongeza Mbao FC kwa kuanza ligi vizuri kwani waliifunga Kagera Sugar katika mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu ikiwa ni msimu wake wa pili tangu ipande ligi kuu lakini imeweza kufanya vizuri.
Naye Mwenyekiti wa klabu hiyo Solly Zephania Njashi aliishukuru  kampuni ya GF kwa kuingia nao mkataba nakusema basi litawasaidia katika safari mbalimbali kipindi hiki cha ligi.
“Tunawashukuru GF kwa udhamini wao wa fedha pamoja na basi kwani itasaidia kwenye klabu yetu katika safari za mikoani za ligi kuu,” alisema Solly.
Huo ni udhamini baada ya mwaka jana kupata udhamini wa Hawaii Products Supplies, watengenezaji wa maziwa ya Cowbell wenye thamani ya sh. milioni 50 kwa msimu. 
Katika msimu uliopita Mbao ni washindi wa pili wa Azam Sports Federation Cup.

No comments:

Post a Comment