Pages

Thursday, August 31, 2017

CHIRWA NA KASEKE HURU, MSUVA APEWA ONYO

Image result for OBREY CHIRWA

WACHEZAJI Obrey Chirwa wa Yanga na Deus Kaseke wa Singida United wameachiwa huru na Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la mpira miguu Tanzania (TFF) baada ya kufungiwa kutocheza michezo ya kimashindano ya ndani ya nchi kwa tuhuma za kufanya vurugu katika mchezo wa mwisho ya Ligi Kuu msimu uliopita dhidi ya Mbao FC.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Mei 21 mwaka huu wachezaji hao ambao walikuwa wakichezea Yanga ilidaiwa kumwangusha mwamuzi wa mchezo huo Charles Ludovic kutoka Tabora kutokana na kutoridhishwa na maamuzi.
Akizungumza leo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya nidhamu ya TFF, Peter Hellar alisema wamepitia picha mjongeo (video) mnato, taarifa ya mwamuzi na Kamishna na kujiridhisha kuwa wachezaji hao hawakufanya kosa bali Simon Msuva ndiye aliyemsukuma Ludovic na kuandikiwa barua ya onyo.
“Kamati ya nidhamu ya TFF imekutana jana (juzi) kusikiliza shauri la wachezaji Deus Kaseke, Obrey Chirwa na Simon Msuva. Chirwa na Kaseke walikuwepo na kuhojiwa lakini Msuva hakuwepo,”
“Kupitia picha mjongeo (video) kamati imejiridhisha kuwa Chirwa na Kaseke hawakufanya kosa ila Msuva licha ya kutokufika mbele ya kamati amepatikana na hatia na ameandikiwa barua ya onyo,” alisema Hellar.
Pia Hellar alisema kwa mujibu wa kanuni za ibara ya 49 kifungu kidogo cha tisa ambayo adhabu yake ni kufungiwa si chini ya mechi tatu imeamua kutoa onyo kwa sababu kamati ya saa 72 ilitoa adhabu kabla ya kamati ya nidhamu ambayo ndio yenye mamlaka ya kutoa adhabu.
Aidha Hellar alisema kwa kutambua kuwa wachezaji hao walianza kutumikia adhabu kabla ya kamati ya nidhamu kusikiliza shauri hilo na Yanga ilikuwa kwenye mashindano imeamua kumwandikia Msuva barua ya onyo
Tayari Kaseke na Chirwa wamekosa mchezo wa kwanza wa ligi huku Msuva akisajiliwa na timu ya Difaa Al Jadida ambayo inashiriki ligi kuu ya Morocco.
Shauri hilo liliwasilishwa kwa kamati hiyo mnamo Mei 30 na Kamati ya uendashaji wa Ligi kwa hatua za kinidhamu.

No comments:

Post a Comment