Pages

Saturday, June 17, 2017

WAHITIMU WA NGOMA ZA UTAMADUNI WAFUNIKA TASUBA











SERIKALI imeipongeza Taasisi ya Tulia Trust kwa kufadhili vijana 20 kutoka Tukuyu, Mbeya elimu ya sanaa katika Taasisi ya Sanaa Bagamoyo (TaSUBa)
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo maalum ya miezi miwili jana, Kaimu Mkurugenzi wa Utamaduni, Leah Kihimbi aliwashukuru vijana hao kwa kukubali kupokea mafunzo hayo.
Kihimbi aliwataka vijana hao kutumia mafunzo hayo kuchochea jamii kupenda utamaduni wetu na kurejea katika misingi ya vyakula, mavazi na sanaa.
“Naamini hamtofanya sanaa Mbeya pekee bali mtapanua wigo katika mikoa mingine hivyo mtakuwa mabalozi wa ngoma za asili hapa nchini,” alisema Kihimbi
Aidha aliwaasa vijana hao wakatumie ujuzi walioupata Bagamoyo kwa wenzao wa Mbeya na kuongeza kuwa mafunzo hayo wayafikishe kwa wanawake ambao hawakushiriki mafunzo.
Naye Kaimu  Mtendaji wa TaSUBa, Gabriel Kiiza alisema mafunzo ya vijana hao yaliyoanza Aprili 18-Juni 16  kwa ushirikiano TaSUBa na Tulia Trust na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano wa Tulia Trust
 “Tunaipongeza Tulia Trust kwa kuwaendeleza vijana ambao walikuwa hawana elimu ya sanaa, hivi sasa watafanya kazi yao kwa weledi zaidi tofauti na ilivyokuwa awali,” alisema Kiiza.
Balozi wa Tulia Trust, Hassan Ngoma alisema vijana 20 waliopata mafunzo Bagamoyo ni zao la Maonesho ya Utamaduni Tulia yaliyofanyika mwaka jana wilayani Tukuyu, hivyo shindano la mwaka huu wanatarajia kuongeza ushindani kwa vijana watakaoshiriki maonesho yanayotarajia kuanza Septemba 21-23.
Ngoma alisema mbali ya kusaidia sanaa, pia Tulia Trust ni waandaaji wa Tulia Marathon na vikundi vya uchumi kwa akina mama.
 “Tumepanga kuendeleza ushirikiano utaendelea kati yao na TaSUBa, wengine waige mfano huo ambao utasaidia sanaa yetu katika anga la Kimataifa,” alisema Ngoma.
Katika hafla hiyo, vijana hao walikabidhiwa vyeti huku wengine wanne kati yao wakichaguliwa kuendelea na masomo ya cheti baada ya kufanya vizuri.       

No comments:

Post a Comment