NDEGE yake
ilitua muda mfupi tu baada ya kumalizika kwa mechi za Ligi Kuu ya England
(ECL), lengo likiwa kupimwa na kukubali maslahi binafsi na Manchester City ili
msimu ujao akipige Etihad.
Si yeye wala
kocha Pep Guardiola waliopenda kupoteza muda juu ya jambo hilo, wote
wakionekana kuwa makini na kutaka wamalizane mapema ili lisitokee jingine na
kuvuruga mipango – kila mmoja akionekana kuwa na hamu.
Wakati
Guardiola amechukua hatua ya haraka kwenye kuanza usajili, mchezaji mwenyewe, Bernardo
Mota Veiga de Carvalho Silva kutoka Ureno alitaka ahakikishe kwamba ima faima
anajiunga na matajiri hao wa Manchester akitoka Monaco, Ufaransa.
Jina
lililozoeleka zaidi ni Bernardo Silva na si kwamba yanatumika yote kwenye
mlolongo huo hapo juu, akiwa ni Mreno aliyezaliwa Agosti 10, 1994 na amekuwa
akifurahia Ligue 1 – Ligi Kuu ya Ufaransa na Timu ya Taifa ya Ureno akicheza
eneo la kiungo.
Na leo ndiyo
siku rasmi ambayo atachukuliwa kwamba ameanza mkataba wake, kwani ndipo Chama
cha Soka (FA) kimefungua rasmi dirisha hili kubwa la usajili la msimu wa
kiangazi, litakaloona mbwembwe kwa wenye fedha na kukimbilia makombo kwa wasio
na kisu kikali.
Naam, Man
City wameachana na pauni milioni 43.5 kwa ajili ya kifaa hiki katika ada ya
uhamisho. Silva atakayeungana na Silva (David) mwingine hapo Etihad, hajaanza
kusikika leo kwani alikuwa kwenye kikosi cha U-19 cha Timu ya Taifa ya Ureno
kwenye michuano ya Uefa 2013.
Ni yeye
aliyetia mchango sana wakasonga hadi nusu fainali na haikushangaza pale
alipotajwa kuwa moja kati ya watu 10 wenye umri mdogo wenye kipaji kikubwa
katika Ulaya kwenye soka.
Hakuchaguliwa
na marafiki zake, bali wana habari kutoka nchi mbalimbali za Ulaya, kama
England, Ufaransa, Italia, Ujerumani, Hispania na kwingineko, ikiwamo Ureno.
Alianza
kuchezea kikosi ha wakubwa cha Ureno Machi 31, 2015 walipokipiga dhidi ya Cape
Verde katika mechi ya kirafiki na mguu wake ulihusika kwenye moja ya mabao
matano waliyoshinda dhidi ya Ujerumani (U-21) kwenye Uefa.
Watu wanajua
kutoa majina – na hutofautiana baina ya mtu mmoja na mwingine, ambapo kinda
huyu wa Man U anayekwenda kukutana na akina Gabriel Jesus, anaitwa bazooka,
yaani kwamba ni aina ya mchezaji anayweza kujitanua anavyopenda uwanjani,
akiwapelekesha wachezaji wa timu pinzani.
Ni mtu
aliyekuwa akiishi kwenye nyumba iliyobana sana kwenye maflati hapo jijini Monaco,
ambapo alianza maisha akiwa na hali ya chini, akiosha vyombo hotelini kujipatia
chochote cha kupeleka kinywani.
Anaelezwa na
walimu wake kwamba ni mchezaji mwenye ufundi mkubwa na maono ya kimichezo
anapokuwa uwanjani, akicheza kana kwamba mpira umeshikiliwa kwa gundi mguuni
pake, ambapo kuupoteza ni ngumu sana.
Asifikiri
kwamba yaliyokuwa Monaco ndiyo yapo humu kwenye EPL, maana kule kwanza kuna uwezekano
mkubwa wa kutolipa kodi, lakini pia mtindo wa maisha ni wa kujirusha sana,
kukiwamo macasino mengi na utajiri wa aina hyake.
Hata hivyo,
yote niliyotaja hapo juu hayamhusu yeye moja kwa moja, bali alikuwa akiona kwa
wengine huko Monaco. Hajiingizi kwenye hayo, bali alitumia fedha zake kwa
uangalifu, akiwa na chumba kilichobana sana cha kulala na jiko dogo.
Hakuwa
amenunua hata mashine ya kuosha vyombo, hivyo alikuwa akiosha mwenyewe kwa
mikono yake na vivyo hivyo kwa kufua nguo zake na kuzianika kwenye balkoni kwa
ajili ya kuzikausha.
Ni kweli
alikokaa aliangaliana na bahari, mandhari nzuri isipokuwa kwa udogo wa eneo
lake si hivyo. Kwa pauni 30,000 kwa wiki alizokuwa akilipwa hapo Monaco,
angeweza kuzitumia kuchukua nyumba kubwa tu kwenye viunga vya jiji.
Manchester
kule hataiona bahari tofauti na Monaco na haijaeleweka atatafuta nyumba ya aina
gani, kwa sababu moja ya sifa zake ni mtu asiyetaka kutumia kiasi kikubwa cha
fedha kwa mambo yake mwenyewe. Hajichori tatuu wala kununua saa au magari ya
kifahari.
Akiwa na
umri wa miaka 22 amejijengea nidhamu fulani anayotaka ahakikishe kuishikilia na
anaondoka wakati Monaco waliokosa ubingwa mara kadhaa wakiuchukua kwa
kuwashinda mahasimu wao – Paris Saint-Germain (PSG).
Wanamsema
kuwa ni aina ya mtu anayeona vitu kabla ya wengine wote – kutafuta vyumba,
kupokea mpira, kugawa pasi, kukimbia na mpira na kisha kutafuta eneo zuri
kwa ajili ya kupokea tena mpira na kufungwa – utampenda. Si rahisi kumwona
uwanjani eti akiwa amekaa; muda wote anasongea na kukimbia.
“Mnamzungumzia
Bernardo Silva? Achana na hilo jina, mwito bazooka, anasambaa kwa kujitanua
lakini pia anaushikilia mpira mguuni pake kana kwamba kuna gundi. Ningeweza
kulipa fedha kwa ajili ya kumtazama akicheza nakuambia,” anasema Benjamin
Mendy, beki wa kushoto wa Monaco baada ya timu yao kutwaa ubingwa kwa mara ya
kwanza katika kipindi cha miaka 17.
Mchezaji
mwenzake mwingine (wa zamani sasa), Jemerson, ambaye ni beki wa kati, anasema
Silva ana uchawi wa aina yake na kwamba ni kama vile ametoka sayari nyingine.
Anasema hufanya vitu visivyo vya kawaida kwenye mazoezi sana na kwenye mechi.
Anamalizia kwa kicheko, na anapoulizwa kulikoni, anasema ni kutokana na jinsi
masikio ya Silva yalivyo kiajabu.
No comments:
Post a Comment