JUMANNE
jioni watu walikuwa wamejikusanya katika makundi madogo na wengine makubwa hapa
Kaskazini mwa London, wakijadili uamuzi wa Arsene Wenger kusaini mkataba mpya
wa miaka miwili kubaki klabuni hapa.
Amechukua
uamuzi huo, ikiwa ni kipindi kifupi kabisa tangu kuwatandika Chelsea 2-1 na
kutwaa Kombe la FA, lakini ikiwa pia si muda mwingi tangu kwa mara ya kwanza
katika miongo miwili wamalize Ligi kuu ya England (EPL) nje ya nne bora za juu.
Hii
inamaanisha nini? Kwa mara ya kwanza Arsenal hawashiriki msimu ujao kwenye Ligi
ya Mabingwa Ulaya (UCL), kwa mara ya kwanza wamemaliza kwenye nafasi ya tano,
kwa mara ya kwanza shinikizo kubwa limekuwa kwa Mfaransa huyo kuondoka.
Lakini kwa
mara nyingine tena ameonesha yeye ndiye ndiye ‘sterling’ hapo Emirates na
atakwenda kwa zaidi ya miaka 22 mfululizo, akiwa pia mtoa uamuzi wa kipi
kifanyike.
Alikutana na mmiliki wa Arsenal, Mmarekani
Stan Kroenke Jumatatu, akakubali ofa aliyokuwa amewekewa mezani kitambo sasa.
Baada ya
kumalizana wawili hao, kilichofuata ni kupeleka tu uamuzi huo kwa wajumbe wa
Bodi ya Wakurugenzi wa Arsenal waliokuwa wakikutana juzi Jumanne kwa kikao cha
kawaida cha mwaka, ikiwa pamoja na mambo mengine ilikuwa kuona mwelekeo wa
klabu hiyo.
Baada ya
kumaliza Ligi Kuu wakiwa pointi 18 nyuma ya mabingwa wapya Chelsea, huku vijana
wa Stamford Bridge wanaofundishwa na Antonio Conte wakiwa kwenye kiwango cha
juu, walitabiriwa kuchukua pia Kombe la FA, lakini kama walivyofanya kwa Manchester
United kwenye mechi ya EPL, Arsenal waliwanyamazisha Chelsea kwa mabao mawili
tena.
Wenger
ameweka historia ya kuwa kocha mwenye mafanikio zaidi katika rekodi za Kombe la
FA, kwani amelitwaa mara nne kati ya saba ambazo Arsenal wamelichukua, lakini
pia amewapa ubingwa wa England mara tatu.
Ni wazi
anaamini kwamba alitakiwa aheshimiwe zaidi na washabiki, lakini pia wamiliki na
viongozi kuweka zaidi imani kwake.
Iwapo
Arsenal wangefungwa na Chelsea, tena wakafungwa kwa idadi kubwa kabisa ya mabao
kama wengi walivyotarajia, basi kungekuwa na giza kubwa klabuni, giza ambalo
huenda ingekuwa vigumu hata kwa washabiki wanaomuunga mkono kuendelea kusimama
naye.
Badala yake,
tafsiri inayokuja kwa ushindi wa Arsenal dhidi ya Chelsea ni kwamba bado Wenger
ana uwezo wa kushinda mechi kubwa – gemu ngumu na anaweza kutoa majibu kwa
maswali magumu.
Moja ya
mbinu mpya alizokuja nazo kwenye mechi za mwisho, ni zile alizoziua alipoingia
Arsenal 1996 – matumizi ya beki tatu. Amerejea kule na kusema kwamba hata katika
umri wake mkubwa, bado anaweza kukumbatia mageuzi.
Bila shaka
kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Arsenal, ingetokea ubishani basi
angewaonesha Kombe la FA na kuwaeleza kwamba ndio ushahidi wa wazi kwamba bado
ana uwezo wa kufanya mambo Emirates dhidi ya klabu kubwa.
Sasa kama
Wenger ameshaamua kubaki, anatakiwa kuharakisha masuala ya wachezaji wake
nyota, Alexis Sanchez na Mesut Ozil yanamalizwa kwa njia chanya kwa klabu.
Tunasikia jinsi Manchester City na Bayern Munich wanavyomuwania Sanchez huku Ozil
akidaiwa kupigwa jicho na Besiktas wa Uturuki.
Pale Wembley
dhidi ya cheslea, wawili hao walicheza vyema, wakawa kwenye viwango vizuri na
kuonesha uzalendo mkubwa kwa klabu, hivyo ni juu ya Arsenal sasa kuonesha nguvu
na kuamua kuwabakisha Emirates.
Wenger
akishawatuliza hao, inabidi awageukie Waingereza Alex Oxlade-Chamberlain na
Theo Walcott, ambao hapana ubishi kwamba wana vipaji sana, lakini hawajaonesha
kazi ya ufanisi kwa uendelevu sana.
Kabla ya
kuukubali mkataba mpya, Wenger alisikika akisema kwamba Washika Bunduki wa
London wanahitaji mchezaji mmoja au wawili tu wapya wenye kiwango cha juu
kabisa, lakini lazima wawe timamu kiakili na kimwili, ili kuepuka kuanguka
anguko kubwa kama lile lililoanza Machi mwaka huu na kuwagharimu nafasi ‘yao’
UCL.
No comments:
Post a Comment