Pages

Wednesday, May 24, 2017

SERENGETI BOYS YAWASILI, MWAKYEMBE AIPOKEA, ASEMA WASIKATE TAMAA.









WAZIRI wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk.Harisson Mwakyembe amewataka wachezaji wa timu ya Taifa ya Wachezaji wa chini ya miaka 17, Serengeti kutokata tamaa badala yake kujipanga kuitumikia timu ya U-20.
Dk. Mwakyembe alisema hayo baada ya kuipokea timu hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere iliporejea kutokea nchini Gabon ilipokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika la U-17.
Timu hiyo ambayo imetolewa ikiwa inashikiria nafasi ya pili baada ya kufungwa 1-0 na Niger na hivyo kulazimika kuyaaga mashindano hayo kwa kanuni ya head to head
Mwakyembe alisema Serengeti imewakilisha vema nchi kwa kushiriki kwao kwenye michuano hiyo kwa kuwa mara ya mwisho kwa nchi kuingia hatua hiyo ni miaka 37 iliyopita.
Alisema, watanzania wanatambua kazi ngumu ambayo timu hiyo imefanya na hasa kwa kushinda baadhi ya michezo yake ikiwa ni pamoja na kutoa sare dhidi ya Mali ambao ni mabingwa watetezi.
"Nyie ni washindi kwa kuwa asiekubali kushindwa sio mshindani na nyie ni washindi kwa kuwa mlichokifanya sio cha kawaida, na hata hao Niger wameshinda ni kama wamebahatisha tu Wizara ipo nanyi na tutawaendeleza".
Aliongeza" nilikuwa bungeni Dodoma, na nimemuomba ruhusa Mheshimiwa Spika ili aniruhusu nije kuungana na nyinyi na sasa tusilie ila tujipange".
Aliuomba uongozi wa timu hiyo kuipeleka mkoani Dodoma kwa ajilia ya mchezo wa kirafiki na wabunge ikiwa ni sehemu ya kuwaonesha uwezo wao kisoka.
Aliongeza, huku wachezaji hao wakianza kambi kwa ajili ya kuiwakilisha Ngorongoro tayari maandalizi ya kuiinua itakayokuwa Serengeti yameanza.
Kwa upande wake Mkuu wa msafara, Ayoub Nyenzi alishindwa kuvumilia na kujikuta akiangusha kilio wakati akizungumzia michuano hiyo ilivyokuwa chini Gabon.
Wachezaji waliwasili majira ya saa nane unusu na baada ya kuwasili ilienda moja kwa moja kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya kuwapokea ndani ya Uwanja huo.
Walikabidhiwa maua huku Waziri Mwakyembe akiwa na jukumu la kuwapokea katika lango la kuelekea kwenye eneo hilo na alisikika akiwafariji wachezaji hao.
Nje ya eneo la Uwanja kulikuwapo na wazazi, ndugu na jamaa wa wachezaji hao walioenda kuwasalimia kabla ya wachezaji hao hawajapanda basi lao kuelekea kambini.

No comments:

Post a Comment