NJIA aliyopitia
imemfikisha katika ‘utukufu’ aliotaka kuwafikisha Manchester United, lakini
bado Jose Mourinho ana mengi ya kujifunza na kufanyia kazi.
Alionesha
mkato wa tamaa kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) ngwe ya mwisho kiasi kwamba
alifika mahali na kusema hawakuwa wakitaka kucheza mechi hizo tena, bali
kujielekeza kwenye ligi ndogo – Europa League.
Alishaona
kwamba hawana ubavu wa kuwapiku Arsenal, Liverpool wala Manchester City katika
kuwania nafasi ya tatu na ya nne ili kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya
(UCL), ambayo ni ndoto kubwa ya klabu na wachezaji wengi hapa Ulaya.
Ni kwa
sababu hiyo, bila wengi kujua awali, Mourinho alijiongoza kwenye Ligi ya
Europa, akafanikiwa kupenya robo, nusu na hatimaye fainali, akakunja kidole na
kusema hapo hapo, huku akimwaga makinda kwenye mechi za EPL.
Kweli
amefanikiwa kuwapa ubingwa wa Europa Manchester United – kwa kuwafunga Ajax 2-0
– walau akamalizia msimu wake wa kwanza hapo kwa kutwaa kombe, tofauti na klabu
hasimu – Manchester City wanaofundishwa na Pep Guardiola aliyekuwa pia kwenye
msimu wake wa kwanza.
Sasa Man U
wameungana na mabingwa wa England, Chelsea ambao chini ya Antonio Conte, naye
kwenye msimu wake wa kwanza wametwaa kombe hilo wakati Tottenham Hotspur
wamekuwa wakali zaidi chini ya Mauricio Pochettino na kushika nafasi ya pili,
akijijengea matumaini ya kuwa kwenye ushindani mkubwa zaidi mwakani na
akifikiria pia kutwaa ubingwa.
Wakati
wachezaji wa Man U wakishangilia kutwaa kombe hilo Jumatano, Mourinho alikuwa
akitembea akiwa na bendera nyekundu, akapitiliza mbele ya kikosi chake na
kujaribu kwenda kupandikiza kamlingoti ka bendera hiyo uwanjani lakini kutokana
na ugumu wa dimba mlingoti ukapinda.
Alijaribu
zaidi lakini akashindwa, ikawa kama alivyojaribu kupata kufuzu kupitia EPL
akashindwa akajielekeza ligi hiyo ndogo; hapo alisogelea kibango kilichokuwa
hapo kikiwa kimeandikwa ‘Stockholm Final 2017’. Hili lilikuwa hakika
fumbo baada ya kashikashi zote kwenye ligi, kukaa nafasi ya saba muda mwingi,
wakapanda ya sita kisha ya tano, wakapata majeruhi kabla ya kurudi chini nafasi
ya sita walikomalizia.
Haikuishia
hapo, Paul Pogba akafiwa na baba yake na kukosa mechi kadhaa, huku Zlatan
Ibrahimovic aliyekuwa na uchu wa kuwa kwenye nne bora akiumia vibaya goti na
hadi fainali hiyo inafanyika alikuwa akitembelea magongo, basi Man U wakawa
wazito na wakagongwa na Arsenal waliokatisha muda wao mrefu wa kutofungwa mechi
EPL.
Baada ya
madhila yote hayo, hatimaye wamemaliza msimu kwa kikombe hicho kidogo, lakini
maana yake kubwa ni kule kufuzu kwa UCL, ambapo msimu ujao watakuwa wakiwacheka
wapinzani wao kama Arsenal ambao wamemaliza katika nafasi ya tano – juu yao,
lakini wamekwama UCL na wanakwenda Europa huku Man U wakienda UCL.
Ni
mbinu tu na ujanja lakini vina mwisho. Lazima Mourinho ahakikishe anajijenga
vyema na kikosi chake, maana ukiangalia tangu mwanzo wa msimu, akiwa na
wachezaji wazuri, mahiri, ghali kwenye kila eneo kuanzia golikipa, hawakufanya
vyema, wakafungwa kisha wakaendekeza sare nyingi.
Ukiachilia
mbali kombe hilo na kufuzu kwao, kuna maswali mengi kuliko majibu juu ya kipi
kikosi hicho kilifanya kwenye EPL; kulikoni mkusanyiko wa kikosi aghali jinsi
hiyo ushindwe kufanya mambo kiasi cha kuzidiwa kwenye nafasi na hao niliowataja
awali.
Je, Mourinho
anaishiwa mbinu za kufundisha na kuishia kuegesha basi ili kuona kwamba
wanakwenda sare nyingi vile? Kwenye fainali ile dhidi ya vijana wadogo kabisa
wa Ajax, United walikuwa ndicho kikosi ghali zaidi kupata kucheza kwenye
fainali ya Europa, lakini shangaa kwamba Marouane Fellaini eti ndiye
alichezeshwa kama mshambuliaji pekee.
Kama ni kiu,
basi Mourinho alikuwa nayo ya kupata kikombe msimu huu, na moyo wake haukutulia
hadi alipojihakikishia kwamba amepata hicho; bao la kwanza lilipofungwa
hakushangilia, akijidai kwamba ama hakuona au alikuwa na mawazo mengine.
Lakini
lilipofungwa lile la pili, alisimama na kushangilia na mwonekano wa tangu hapo
uliashiria kitu kimoja – gemu ilikuwa imeisha na ushindi ni wake. Hata kitendo
chake cha kulibusu kombe kabla halijakabidhiwa kwa nahodha Wayne Rooney na
kisha kujidai kutoroka nalo ilikuwa ni ishara tosha kabisa jinsi
lilivyomaanisha makubwa kwake.
Naam, katika
majenzi mapya ya klabu hiyo ambayo haijapata kuwa juu tangu kuondoka kwa kocha
mkongwe Alex Ferguson, ilikuwa muhimu kushinda – kufuzu kwa UCL, lakini njia
aliyopitia kwa sasa inaweza kupuuzwa, japokuwa msimu ujao ataangaliwa kwa jicho
yakinifu zaidi.
Mourinho
alipingwa na wengi kwa njia aliyopitia, lakini akawaambia wapinzani hao wa ndani
na nje ya klabu watulie kimya na Jumatano hii aliwaonesha kwa nini
alikuwa akifanya hayo – anaenda UCL na wakubwa zao kimsimamo – Arsenal,
wanakwenda kwenye ligi ndogo na ngumu, inayohusisha mechi nyingi na safari za
mbali, michosho kwa wachezaji na pengine kuumia, ikizingatiwa Arsenal wamekuwa
na kikosi cha wachezaji wanaoumia hovyo hovyo.
No comments:
Post a Comment