Pages

Monday, May 29, 2017

Mabeki hawa ni vyuma vya pua England



WACHEZAJI wanaotokea kulipwa fedha nyingi zaidi katika ligi mbalimbali duniani ni viungo, mawinga na washambuliaji.
Hata kwenye ada za uhamisho huwa hao ndio wanalipiwa zaidi tofauti na mabeki na magolikipa. Hata hivyo, hiyo haiondoi umuhimu wa mabeki, wawe wa pembeni au wa kati, kwani ndizo nguzo muhimu za timu na msingi imara wao.
Hebu tuangalie mabeki waliokuwa bora zaidi katika Ligi Kuu ya England (EPL), tukizingatia wastani wa mechi walizocheza na jinsi walivyosaidia timu zao kuondoka na ‘clean sheet’, yaani kutofungwa bao lolote katika mechi. Hawa tunaowakagua leo ni kwamba wamecheza zaidi ya mechi 100 EPL.
 Image result for Ricardo Carvalho
 1. Richardo Carvalho
Huyu alichezea Chelsea mechi 135 na katika michezo hiyo, asilimia 48.9 hawakufungwa hata bao moja, hivyo kwamba kwa karibu kila mechi mbili alizopiga, basi moja wapinzani hawakufurukuta kufunga bao.
 Image result for Tony Adams
 2. Tony Adams 
Mlinzi huyu alipiga mechi 255 akiwa na Arsenal na asilimia ya mechi ambazo hawakufungwa ni 45.1. tunazungumzia mechi 115 pasipo kufungwa bao kwenye EPL na ndiyo tafsiri hasa ya mtu huyu. Je, Arsenal watakaa wapate beki wa kati mzuri kama huyu? Ni kusubiri tu. Ni majuzi mchezaji huyu alitoka kumshambulia Wenger kwamba amembania asiwe kwenye benchi la ufundi hapo Arsenal zaidi ya mara nne kwa madai eti anamuogopa kutokana na umaarufu wake. Lakini ni huyu huyu amepewa Granada wa Hispania, wakashika mkia La Liga na sasa wameshuka daraja.
 Related image
 3. Nemanja Vidic
Amecheza mechi 211 na asilimia 45 yake hakuruhusu bao, akiwa kwenye ulinzi wa kati, imara sana pale akishirikiana na wengine kama Rio Ferdinand. Alikuja kuzongwa na majeraha kabla ya nahodha huyu wa Manchester United kuamua kuhamia Internazionale kabla ya kustaafu mapema 2016. Alikuwa mgumu wa kweli EPL.
 Image result for John Terry
4. John Terry 
John Terry ndio kwanza ameachia ngazi Chelsea, baada ya kuwa amekamilisha mechi nyingi kwenye klabu aliyokuwa nahodha pia. Walikubaliana na uongozi kwamba kiangazi cha mwaka huu ni wakati mwafaka kwake kuondoka. Ni mmoja wa walinzi na viongozi wazuri waliopata kutokea EPL, achilia mbali utovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja. 
 Image result for Daniel Agger
5. Daniel Agger 
Akicheza na Liverpool, Agger alipiga mechi 175, kati ya hizo asilimia 41.7 bao halikutinga kwenye goli lao. Kwa kiasi kikubwa hakuwa akichukuliwa kuwa mchezaji mkubwa, lakini takwimu haziongopi na zinaonesha kwamba yupo juu. Ameshahama kwa sasa. 
 Image result for steve bruce man utd
6. Steve Bruce 
Huyu alicheza sana kabla ya kuja kuwa kocha wa Hull na aliachia ngazi huko mwaka jana hivi baada ya wamiliki wa klabu hiyo ya EPL kukataa kumpa fedha za kununua wachezaji. Matokeo yake timu imeshushwa daraja sasa. Enzi zake alikipiga katika timu tofauti nchini England, akacheza mechi 148 EPL na asilimia 41.2 mambo yalikuwa mazuri kwani hakuachia bao. Alikuwa akifunga pia mabao muhimu na mazuri kwa timu yake. 
 Related image
7. David May 
Huyu alicheza mechi 158 na usafi wa lango lake aliuhimili kwa asilimia 39.9 akiwa na timu za Manchester United na Blackburn Rovers. Hakudumu sana lakini alikuwa na ufanisi wa kutosha. 
 Image result for Gary Pallister
8. Gary Pallister
Alicheza mechi 261 na asilimia ya kutofungwa bao ilisimama katika asilimia 39.8. Yumo katika orodha ndefu ya wachezaji wanaoitwa mashujaa wa Manchester United. Beki huyu wa kati alifanikiwa kutwaa ubingwa wa England misimu minne kati ya sita aliyokuwa na klabu hiyo kongwe. 
 Image result for Paulo Ferreira
9. Paulo Ferreira 
Huyu ni beki wa pembeni wa Chelsea aliyewachezea mechi 141 na kuwa na 39.7% ya kutoruhusu mabao kwenye mechi zote hizo. Amekuwa hapati sifa anazostahili, hata hivyo, lakini ukweli ni kwamba ametwaa mataji 13 katika miaka yake tisa aliyokaa England. 
 Image result for Sami Hyypia
10. Sami Hyypia
Wengi watakuwa wanamkumbuka mlinzi huyu mrefu na aliyetumia vyema umbo lake akiwa kiongozi wa Liverpool kwa muda mrefu. Alicheza mechi 318 na akazuia mabao kwa asilimia 38.4 ya mechi zote hizo. Alikuwa moyo wa ukuta wa The Reds. 
11. Jamie Carragher
Mtu huyu ambaye kwa sasa ni mchambuzi yakinifu wa mechi, amecheza mechi nyingi – 508 katika miaka 17 aliyokaa Liverpool na asilimia yake ya uokozi ni 38.4. Anastahili sifa kwa muda mrefu aliokaa hapo na kutoka katika mechi 195 bila lango lake kutikiswa na mpira. Ndiye anaongoza kwa mechi nyingi kiasi hicho.
12. Per Mertesacker 
Mjerumani huyu mrefu na nahodha wa Arsenal amekuwa pia kwenye Timu ya Taifa ya Ujerumani. Bado anadunda na ni tegemeo kwa Arsenal akiwa mzima, lakini msimu wote huu amekuwa nje ya dimba kutokana na kuumia wakati wa maandalizi ya msimu.
Ni mtu mwenye nidhamu ndani na nje ya uwanja ambapo kabla ya unahodha alikuwa mkuu wa nidhamu chini ya Arsene Wenger, akikusanya faini kwa wachezaji waliofanya makosa yoyote ndani na nje ya dimba, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kazini. 
13. Ashley Cole
Ashley Cole amepata kutajwa kuwa mmoja wa mabeki wazurti zaidi wa kushoto, akiwa amecheza mechi 385 na akazuia mabao katika mechi asilimia 38.2. amezigawanywa kwa Arsenal na baadaye Chelsea, pamoja na utata unaoyazunguka maisha yake ndani na nje ya dimba.
 14. William Gallas
Huyu alikuwa kiongozi hapo Arsenal, akicheza mechi 321 lakini pia akizigawa kwa kuwa Chelsea na Tottenham Hotspur na kuwa na asilimia 38 ya kutoruhusu mabao. Alikuwa akivaa namba 10, alijiamini na kupata mafanikio mchanganyiko.
 15. Laurent Koscielny 
Mfaransa mwingine huyu aliyecheza mechi nyingi akiwa na Arsenal. Beki wa kati wa kimataifa wa Ufaransa ambaye amekaimu unahodha Arsenal muda mwingi. Wapo wachache wanaohoji uimara wake lakini ni mmoja wa mabeki wazuri wa kati na hata alitakiwa na Barcelona. 
16. Rio Ferdinand 
Huyu ni beki mrefu wa kati aliyecheza mechi 504 na katika hizo alifanikiwa kwa asilimia 37.5 kwenda bila kufungwa bao. Kwa muda wote amekuwa tegemeo kwa klabu alizokuwa – Manchester United lakini pia kabla ya hapo Leeds na West Ham, akaja kumaliza bila mafanikio na Queen Park Rangers (QPR) akashuka nao daraja, akasema na kustaafu.
 17. Denis Irwin
Huyu ni mtu aliyekuwa na mechi 308 na asilimia ya mafanikio bila bao kufungwa langoni mwake ni 37.5. huyu ndiye mchezaji pekee ambaye kocha mahiri Alex Ferguson alisema kwamba hapana wasiwasi angemweka wkenye kikosi chake cha ‘Best 11’ cha wakati wote, akisema alikuwa akifanya kosa moja tu katika kipindi cha miaka 10.
18. Lee Dixon 
Dixon alicheza mechi 305 na katika hizo hakuruhusu bao kwenye asilimia 37.4 yake. Alikuwa mchezaji aliyepewa nafasi mara nyingi katika ukocha wa Arsene Wenger hapo Arsenal, katika kipindi kile cha mwanzo cha mafanikio makubwa. 
19. Gary Neville 
Huyu ni mlinzi aliyepata mafanikio makubwa Old Trafford, akicheza mechi 400 na kufanikisha ‘clean sheet’ kwa kiwango cha 37%. Siku hizi mafanikio hayo yanasahaulika kutokana na jinsi alivyofanya vibaya kama kocha. 
20. Vincent Kompany 
Huyu ni nahodha wa Manchester City ambaye hana uhakika wa kuwapo kikosini msimu ujao chini ya Pep Guardiola msimu ujao. Company, Mbelgiji na beki wa kati mwenye nguvu alikuwa akileta tofauti kubwa sana kwa Man City akiwapo na kutokuwapo; majeraha yanamsonga na kwa hakika atakuwa akielekea mwisho wa soka ya ushindani katika ngazi ya juu kwenye klabu kubwa England.

No comments:

Post a Comment