Wadenishi
waahidi kuendelea kusaidia vifaa vya muziki kwa ajili ya kufundishia na
kujifunzia; Tamasha la Bagamoyo lawavuta wengi.
Na Rahel
Pallangyo
TAASISI ya
Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ni miongoni mwa taasisi tatu za Tanzania
ziliteuliwa kuwa vituo vyenye ubora uliotukuka (Centres of Excellence) kwenye
maeneo yake ya msingi.
TaSUBa
iliteuliwa kuwa kituo cha ubora uliotukuka kwenye ufundishaji katika nyanja za
utamaduni na sanaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community
Centre of Excellence in Culture and the Arts).
Malengo
mahsusi ya TaSUBa kuwa kituo cha ubora uliotukuka ni pamoja na kuendesha
mafunzo ya sanaa na utamaduni kwa wasanii wa nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki, kukuza sanaa na utafiti kwenye eneo la utamaduni, kuzishauri nchi
zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki katika maeneo ya uhifadhi, ukuzaji na
maendeleo ya sanaa na utamaduni na kuratibu na kuendesha tamasha la Sanaa na
Utamaduni kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Historia ya TaSUBa
TaSUBa ni
Wakala wa serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Serikali Na.
30 ya mwaka 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, kupitia tangazo
la Serikali Na. 220 la Novemba 2, 2007.
Taasisi hii
inatokana na kilichokuwa Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambacho kilianzishwa mwaka
1981 baada ya kuvunjwa kwa kikundi cha Sanaa za Maonyesho cha Taifa mwaka 1980.
Baada ya
kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni mwaka 1962, kilianzishwa kikundi cha Sanaa za
Maonyesho cha Taifa ambacho kilianza na fani ya ngoma (1963), Sarakasi (1969)
na Tamthilia (1974).
Kazi kubwa
ya Kikundi hiki ilikuwa kufanya maonyesho sehemu mbali mbali nchini ili kukuza
mwamko wa kuupenda na kuutukuza utamaduni wa Watanzania ambao mkoloni
alijitahidi kwa nguvu zake zote kuukandamiza.
Kazi za
kikundi hicho ni kuwahamasisha Watanzania wajivunie utamaduni wao na washiriki
kikamilifu kuufufua, kuukuza na kuulinda.
Makazi ya Kikundi yalikuwa Shariff Shamba- Ilala, Dar es Salaam, mahali
zilipo ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Mtendaji
Mkuu wa TaSUBa, Dk Herbert Makoye wamejipanga kuhakikisha Taasisi hiyo inakuwa kituo cha mafunzo ya Sanaa na
Utamaduni chenye ubora uliotukuka barani Afrika.
Malengo ya TaSUBa
“Kwa sasa
TaSUBa ni kituo bora uliotukuka kwa Afrika Mashariki hivyo tumejiandaa
kuhakikisha tunakuwa bora Afrika nzima na kwa sasa inawezekana kwani serikali
ya Denmark imetupatia vifaa vya kufundishia na kujifunza vyenye thamani ya
milioni 100 na serikali pia imetupatia shilingi milioni 100 tukanunulia vifaa,”
alisema Dk. Makoye.
Pia Dk.
Makoye alisema wamedhamiria kuzalisha wasanii, viongozi wa sanaa na wafanyakazi
katika sekta ya utamaduni sambamba na kuzalisha kazi za sanaa pamoja na huduma
za multimedia.
Dk. Makoye
alisema kwa upande wa wafanyakazi na waalimu wamejipanga kuandaa wakuzaji wa
sanaa, wasanii, waendeshaji na wasimamizi wa shughuli za sanaa kwenye sekta za
umma na binafsi. Kwa sababu sanaa na utamaduni kwa kiasi kikubwa unaanza
kupotea pia wanaandaa watafiti na washauri wa sanaa na utamaduni kwa ngazi ya
taifa na kimataifa.
Kukuza
viwango vya sanaa na moyo wa kupenda mila na desturi za Mtanzania na kukuza
mwamko wa matumizi ya sanaa katika mapambano ya matatizo mbalimbali katika
jamaii.
Shughuli za TaSUBa
Taasisi
inatoa mafunzo katika nyanja za Ngoma, Maigizo, Muziki, Sarakasi, Sanaa za
ufundi, Ufundi wa Majukwaa, Sayansi ya jamii (Uongozi na Utawala wa masuala ya
sanaa, TEHEMA, Ujasiliamali, Haki Miliki, Kiswahili na Kiingereza
Pia katika Ubunifu
na uzalishaji wa picha jongefu, ubunifu na uzalishaji wa muziki na sauti.
Katika
kuhakikisha malengo waliojiwekea yanatimia Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Dk. Makoye
alisema kwa mwaka huu wanatarajia kutumia tamasha la Bagamoyo kujitangaza
kimataifa hasa nchi za Afrika Mashariki na Afrika nzima.
Dk. Makoye
alisema tamasha la Bagamoyo linatarajiwa kufanyika Septemba 23-30 mwaka huu
kwenye viwanja vya Taasisi hiyo huku likipambwa na vyakula vya aina mbalimbali
vya asili, ngoma za asili, nguo za asili na vitu vingine vya asili ya hapa
Tanzania.
“Tunatarajia
kutumia Tamasha la Bagamoyo kuitangaza TaSUBa kwenye nchi za Afrika Mashiriki
kwani kwenye nchi za Ulaya tunafahamika na watu wanakuja kusoma hapa,” alisema
Dk. Makoye.
Pia Makoye
alisema tayari nchi za Denmark, Norway na China zimeshathibitisha kushiriki
tamasha la mwaka huu ambalo ni la 35 tangu kuanza mwaka 1991.
Aidha Dk.
Makoye alisema lengo la kujitangaza kwenye nchi za Afrika Mashariki ni
kuwavutiwa kuja kusoma na kujifunza utamaduni kwenye taasisi hiyo ambayo ni
kituo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Nayo serikali
ya Denmark katika kuhakikisha TSUBa inatoa mafunzo kwa vitendo imetoa msaada wa
vifaa vya kufundishia na kujifunzia muziki yenye thamani ya shilingi milioni
100.
Balozi wa
Denmark, Einar Jensen wakati akikabidhi vifaa hivyo alisema Tanzania na Denmark
wana ushirikiano wa miaka 50 sasa na wamekuwa wakishirikiana katika kuendeleza
utamaduni na Sanaa katika jamii za watanzania na kuahidi kuendelea kusaidia.
“Muziki ni
njia mojawapo ya kusaidia kufikisha ujumbe na huwezi kufanya hivyo bila kutumia
vifaa ndio maana Denmark tumeona umuhimu wa kusaidia nyanja hii,” alisema
Jensen.
Dk.
Makoye, alisema msaada wa vifaa hivyo vya Wadenish utasaidia kuboresha
mafunzo ya muziki yanayotolewa na TaSuBa na kuahidi kuvitunza na kuvilinda ili
viweze kutimiza lengo la kununuliwa kwake.
“Vifaa hivi
vimekuja wakati muafaka kwa sababu Taasisi ipo kwenye harakati za kuimarisha
programu zake ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili ili vijana wengi wa Kitanzania
ili wapate fursa ya mafunzo,” alisema Dk. Makoye.
Pia Dk.
Makoye alisema vifaa hivyo vitasaidia eneo la upigaji wa muziki kuondoa
malalamiko yanaelekezwa kwa wasanii wengi wa muziki kuwa hawana uwezo wa kutumia
au kupiga vyombo vya muziki wanapokuwa wanatumbuiza.
Aidha Dk.
Makoye alisema Denmark imekuwa ikisaidia TaSUBa katika kuimarisha taaluma kwani
mwaka 2016 ilitoa msaada wa vyombo vya muziki pamoja na komputa na makabati ya
kutunzia vifaa hivyo vya muziki.
Mwaka 1994
ubalozi wa Denmark uligharamia uendeshaji wa Sanaa shirikishi kwa kushirikiana
na TaSUBa kwenye jamii za wilaya ya Bagamoyo na udhamini wa uchapishaji
wa kitabu cha Sanaa na maendeleo kilichoandikwa na Juma Bakari na Ghonche
Materego ambao walikuwa wafanyakazi wa taasisi hiyo.
TaSUBa
inatoa kozi ya Astashahada mwaka mmoja,
katika masomo ya yafuatazo:
Katika Sanaa
za Maonyesho na Sanaa za Ufundi, katika Teknolojia na Ubunifu wa Sauti na
Muziki, katika Uzalishaji wa Filamu na Vipindi vya Television.
Pia Stashahada
miaka miwili kwenye masomo yafuatazo:
Katika Sanaa
za Maonyesho na Sanaa za Ufundi, katika Teknolojia na Ubunifu wa Sauti na
Muziki na katika Uzalishaji wa Filamu na Vipindi vya Television
Pia TaSUBa
inatoa kozi fupi fupi ambazo zinaandaliwa kulingana na mahitaji maalum ya
walengwa ambazo zinafundishwa kwenye maeneo yote ya taaluma zinazotolewa na
TaSUBa
ambazo ni
Utunzi muziki, uimbaji, upigaji wa ala mbalimbali za muziki, teknolojia ya
muziki na ngoma.
Uigizaji wa
michezo ya kuigiza na filamu, uandishi wa miswada ya michezo ya kuigiza na
filamu, uongozaji wa michezo ya kuigiza na filamu, ubunifu wa malebo, ufundi wa
jukwaa, sarakasi, uchoraji, graphic design, uhariri wa filamu na upigaji wa
filamu.
Dk. Makoye
anawaalika watu, makampuni na taasisi zinazohusu sanaa na utamaduni kujiunga na
TaSUBa ili wapate mafunzo katika kozi ambazo watachagua wenyewe na kuacha
kufanya kazi bila kusoma kwa kisingizio cha uzoefu.
No comments:
Post a Comment