WANACHAMA SIMBA WABARIKI MABADILIKO
WANACHAMA wa klabu ya Simba jana walipitisha
marekebisho ya katiba yao kupisha mabadiliko ya uendeshaji.
Katika mkutano huo maalumu wa wanachama uliofanyika kwenye bwalo la
maofisa wa Polisi Oysterbay Dar es Salaam, wanachama wamekubaliana klabu
iendeshwe kwa muundo wa hisa.
Mkutano huo ulioendeshwa chini ya rais wa Simba, Evans Aveva
ulihudhuriwa na wanachama 642. Simba ina wanachama zaidi ya 6,000.
Tofauti na ilivyokuwa katika mkutano uliopita ulitawaliwa na vurugu,
wanachama katika mkutano wa jana walikuwa watulivu muda wote na kila mmoja
akisikiliza hoja za mwingine kabla ya kufikia mwafaka.
Wanachama walikubaliana kipengele cha uendeshwaji wa klabu kiwekwe
katika ibara ya 49 ya katiba ya klabu hiyo.
Ibara hiyo ya 49 baada ya
kubadilishwa inasomeka: 49 (a) Mkutano
wa wanachama unaweza kuitishwa kwa mujibu wa Ibara ya 22 na kufanya mabadiliko
ya mfumo wa umiliki au uendeshwaji wa Simba. 49
(b) mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji au umiliki wa Simba hayataathiri
hadhi ya wanachama wote halali wa Simba isipokuwa hadhi hiyo itabadilika
kuendana na mfumo stahiki wa mabadiliko yaliyofanyika.
Uwiano wa thamani ya umiliki wa kila mwanachama katika mfumo mpya
utajadiliwa na Kamati ya Utendaji kutokana na thamani ya klabu na uwekezaji.
Kipengele (c) cha ibara hiyo kinaeleza kuwa mfumo mpya wa mabadiliko ya
uendeshaji au umiliki wa Simba utarithi haki na mali zote pamoja na madeni na
wajibu wowote uliokuwa chini ya Simba kabla ya mabadiliko hayo.
Kipengele (d) na cha mwisho cha Ibara hiyo kinasema mabadiliko ya mfumo
wa umiliki au uendeshaji wa Simba yatabainisha kuacha kutumika kwa katiba hii
na mkutano mkuu chini ya mfumo mpya utapitisha katiba mpya chini ya utaratibu
wa haki na kura za mfumo huo mpya.
Baada ya wanachama kupitisha kipengele hicho, Rais Aveva aliwataka kuwa
watulivu wakati ambao mabadiliko hayo yatapelekwa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na mwisho kwa Msajili wa
Vyama na Klabu za Michezo ili yapitishwe na kuwa Katiba kamili.
Sikba imefanya mkutano huo baada ya mmoja wa wanachama wake na
mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji ‘Mo’ kutaka kununua asilimia 51 ya hisa za
klabu kwa Sh bilioni 20.
mwisho.
No comments:
Post a Comment