MAYANJA AFURAHIA SIMBA KUKAA KILELENI HADI 2017
KOCHA msidizi wa
Simba, Jackson Mayanja, amesema amefurahishwa kuona timu hiyo inakwenda kuanza
mwaka mpya wa 2017 ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti ya pointi
nne dhidi ya mahasimu wao Yanga.
Simba juzi iliifunga Ruvu Shooting ya Pwani bao
1-0, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru na kufikisha pointi 44
ikiiacha nyuma Yanga nafasi ya pili ikiwa na pointi 40.
Akizungumza na gazeti hili baada ya mchezo huo
kumalizika, Mayanja raia wa Uganda, alisema kuanza mwaka wakiwa wanaongoza ligi
ni jambo zuri kwani watakachokifanya wakati ligi itakapoendelea ni kuhakikisha
wanaendeleza mikakati yao ya kupata ushindi ili kuendelea kubaki kwenye nafasi
hiyo hadi mwisho wa msimu.
“Nawapongeza wachezaji pamoja na benchi zima la
ufundi unajua ligi imekuwa ngumu sana lakini wachezaji wamekuwa wakipambana
kufa kupona na ndiyo maana leo (juzi) tunaelekea kuuanza mwaka mpya tukiwa
tunaongoza ligi tunajua bado hatujamaliza kazi, lakini hapa tulipofika panatia
matumaini,” alisema Mayanja.
Akizungumzia timu yake kupata ushindi mdogo wa
bao moja katika baadhi ya mechi zao, kocha huyo alisema hiyo inatokana na hali
ya hewa kubadilika na joto kuwa kali kiasi cha kuwapa tabu wachezaji wao wakati
mchezo ukiendelea.
Alisema
kama ingekuwa ni amri yao wangeomba Shirikisho la mpira wa miguu
Tanzania TFF, kutoa dakika kadhaa kwa wachezaji kunywa maji kama ambavyo
zinafanya baadhi ya nchi Ulaya, kutokana na joto kuwa kali lakini anaamini hilo
litakuwa gumu.
Kwa upande wake kocha wa Ruvu Shooting, Malale
Hamsini, alisema mchezo ulikuwa mgumu na sababu iliyowafanya kupoteza mechi
hiyo ni makosa madogo madogo ya wachezaji wake, lakini wanakwenda kujipanga
kuhakikisha wanafanya vizuri mechi zijazo.
No comments:
Post a Comment