WAKATI Azam
FC, wakiwa safarini Ruvuma kucheza na Majimaji kwenye mchezo wa Ligi Kuu
Tanzania Bara, habari njema kwao wamepangwa kuazia hatua ya kwanza kwenye kombe
la Shirikisho barani Afrika.
Azam FC
itaanza kucheza nyumbani na mshindi kati
ya Opara United ya Botswana na Mbabane
Swallows ya Swaziland wakati KVZ ya Zanzibar itaanzia hatua ya awali nyumbani
kwa kucheza na Messager Ngozi ya Burundi.
Mashindano yaliyopita Azam FC iliandika
rekodi ya kuwa timu pekee ya Afrika Mashariki kuanzia raundi ya kwanza kwenye
michuano hiyo na hata kwa wale walishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, zingine
zote za ukanda huo zilianzia raundi ya awali.Azam FC kwenye raundi ya kwanza ilikutana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini na kuitoa kwa jumla ya mabao 7-3, ikiwafunga ugenini mabao 3-0 na kuwapa kipigo kingine cha nyumbani 4-3.
Raundi ya pili mabingwa hao wakakutana na vigogo wa Tunisia, Esperance na kujikuta ikifa kiume kwa kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2.
CAF msimu huu imebadilisha mfumo wa mashindano hayo, ambapo imepanua wigo kwa timu zitakazoingia hatua ya makundi kutoka nane hadi 16, kila michuano itahusisha makundi manne yenye timu nne kila moja.
Mfumo huo unamaanisha kuwa timu 32 zitakazocheza raundi ya kwanza inayofuata baada ya ile ya awali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, zile 16 bora zitakazoshinda zitaingia moja kwa moja katika hatua ya mwisho ya mtoano (play off).
Katika hatua hiyo zitakutanishwa na timu nyingine 16 zilizotolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na wale 16 bora watakaopenya hapo watafuzu moja kwa moja kwenye hatua ya makundi, itakayoanza kuchezwa Mei mwakani.
Pia CAF imepandisha zawadi kwa washindi wa Kombe la Shirikisho, wakati bingwa akivuna Dola za Kimarekani Milioni 1.25 (sawa na zaidi ya Bilioni 2.72 za Kitanzania), mshindi wa pili atajizolea Dola za Kimarekani 625,000 (sawa na zaidi ya Sh. Bilioni 1.36).
Timu zitakazoingia nusu fainali kila mmoja itajizolea Dola za Kimarekani 450,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 979.96), zilizoingia robo fainali nazo zitazoa Dola za Kimarekani 350,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 762.19) huku zile zitakazoshika nafasi ya tatu na nne kwenye makundi zikiambulia Dola za Kimarekani 275,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 598.86).
No comments:
Post a Comment