Pages

Wednesday, October 19, 2016

NAPE MGENI RASMI TAMASHA LA NANI ZAIDI LITAKALOFANYIKA MOROGORO DESEMBA 25





WAZIRI wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la uchangiaji wa damu litakalofanyika Disemba 25 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Tamasha hilo limeratibiwa na kampuni ya Tegemeo Arts Group Tanzania, (TAGT)  litawapambanisha wasanii nguli wa muziki wa Taarab Mwanahawa Ally, Khadija Kopa pamoja na Hadija Yusuph ili kujua nani mwenye uwezo wa kukonga nyoyo za mashabiki wa mahadhi ya Pwani watakaohudhuria katika tamasha hilo.
Mratibu wa tamasha hilo Hamis Abdallah 'Kajumulo' amesema kuwa mbali na uchangiaji wa damu pia kutakuwa na zoezi la upimaji wa afya kwa hiyari na sehemu ya mapato ikitumika kuchangia wanafunzi 100 kutoka mikoa mbali mbali nchini vifaa vya elimu kama sare, vitabu na viatu.
"Sehemu ya mapato tutachangia wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu hasa vijijini ili kuinua sekta ya elimu nchini kwa ajili ya kusaidia jitihada za Rais wetu John Magufuli," alisema Kajumulo.
Kwa upande wake Khadija Kopa ambaye ni miongoni mwa washindani kwenye tamasha hilo alisema amehamasika kushiriki tamasha hilo ili kuwasaidia watu wenye matatizo ya damu hasa wanawake huku akijigamba kuwapoteza wanaoshindana naye hivyo wakae vizuri kwavile amejipanga kuwapoteza.

"Nitawaonyesha kwa kwanini mimi naitwa Malkia wa Mipasho nchini, nitawafunika vibaya Mwanahawa na mdogo wangu Hadija lazima niwaambie ukweli ili wajiandae," alitamba Khadija Kopa.

Wasanii hao watasindikizwa na Msondo Ngoma, Sikinde, Jahazi Modern Taarab, Ogopa Kopa Classic Band, The East African Melody pamoja na Five Stars Modern Taarab.

Wengine ni Afande Sele, 20%, Samir, Wali Nazi, Wakali wa Mchiriku TAGT Music, Wakali wa Singeli, Mtanga, Bambo na Kiwewe.

No comments:

Post a Comment