Pages

Thursday, October 20, 2016

LIGI YA WANAWAKE KUANZA NOVEMBA MOSI



 
LIGI ya wanawake ngazi ya Taifa inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba Mosi, ikiwa kwenye makundi mawili yenye timu sita kila moja.
Akizungumza na wandishi wa habari, Afisa wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Alfred Lucas alisema ligi hiyo itachezwa kwa makundi kwa kuzingatia ukanda ili kuzipunguzia gharama timu.
“Timu hizi zitacheza nyumbani na ugenini na washindi watatu kwenye kila kundi watapambanishwa kwenye kituo kimoja ili bingwa apatikane”, alisema Lucas.
Lucas alisema timu zinazounda kundi A ni Mburahati Queens, Evergreen Queens na JKT Queens zote za Dar es Salaam, Mlandizi Queens ya Pwani, Fair Play ya Tanga na Viva Queens ya Mtwara.
Kundi B lina timu za Marsh Academy ya Mwanza, Baobab Queens ya Dodoma, Majengo Women FC ya Singida, Sisters FC ya Kigoma, Kagera Queens ya Kagera na Panama FC ya Iringa.
Viwanja vitakavyotumika  kwa kundi A ni Nang’wanda Sijaona cha Mtwara , Mkwakwani Tanga,  Uhuru na Karume vya Dar es Salaam na kundi B ni CCM Kirumba, Lake Tanganyika, Samora Iringa,  Jamhuri Dodoma na Namfua Singida.
Pia Alfred alisema Mburahati Queens imeweka pingamizi kwa wachezaji Mwanahamisi Omari na Fatuma Bushiri waliosajiliwa na Mlandizi Queen Neema Paul na Mwasiti Juma  waliosajiliwa na Sisters ya Kigoma na Fatuma Hassan ambaye amesajiliwa na JKT Queens
Pingamizi hizi zitasikilizwa Octoba 22 na kamati ya maendeleo ya soka la wanawake kwa kuwaita wachezaji wenyewe kujua wamesajili timu gani .
Alfred alisema timu zinatakiwa kusajili wachezaji wasiozidi saba wa kigeni kutokana na kanuni ya 53 na 54 za ligi na pia mchezaji huyo anatakiwa kupata kibali cha kufanya kazi na uhamisho wake. (ITC)

No comments:

Post a Comment