Pages

Saturday, October 15, 2016

ARSENAL NA CHELSEA ZASHINDA HUKU MAN CITY IKILAZIMISHWA SARE



ARSENAL na Chelsea leo zimeibuka na ushindi mtamu wa mabao matatu kila mmoja dhidi ya Swansea na Leicester, huku Manchester City ikilazimishwa sare na Everton na wageni Bournemouth waliopanda daraja msimu huu wakibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Hull.
Ushindi wa Arsenal wa mabao 3-2, umewafanya kujivuta hadi nafasi ya pili ikiwa pointi 19 sawa Man City iliyopo nafasi ya kwanza kwenye msimamo, wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Chelsea imemhakikisha kocha wake, Antonio Conte kuendelea kuwa na tabasamu ya kukinoa kikosi hicho, baada ya kuwafunga mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Leicester City mabao 3-0 katika dimba la Stamford Bridge.
Conte alikuwa akishutumiwa na uvumi uliozagaa kwamba, amekalia kuti kavu baada ya Chelsea kutokuwa na matokeo mazuri tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu.
Lakini matokeo hayo yanamfanya Conte kuwa na tabasamu zuri usoni mwake na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutotimuliwa katika kibarua chake.
Leicester ambayo msimu uliopita iliweka rekodi ya aina yake kwa kutwaa taji la Ligi Kuu ikitoka kupanda daraja, hicho kilikuwa ni kipigo chao cha nne mfululizo kwenye Ligi hiyo.
Katika mchezo huo, Chelsea walianza kuhesabu bao lao la kwanza dakika ya saba baada ya Nemanja Matic kuupindua mpira wa kona uliopigwa na Eden Hazard na Diego Costa akautumbukiza wavuni.
David Luiz alipiga shuti kali la adhabu ndogo ambalo liligonga mlingoti wa goli kabla ya Pedro kuupata mpira na kumpasia Hazard, ambaye alimpiga chenga golikipa, Kasper Schmeichel na kufunga bao la pili dakika ya 33.
Luiz nusuru ajifunge baada ya mpira wake kugonga mlingoti wa goli kipindi cha pili kabla ya Victor Moses kufunga bao la tatu baada ya kupokea pasi kutoka kwa Nathaniel Chalobah ikiwa ni dakika ya 80.
Leicester, ambao ilimuweka Riyad Mahrez benchi kwa mara ya kwanza wakianza mechi katika mechi 36, na hawakuwa na shuti lolote lililolenga goli na walionekana kubanwa zaidi na mashambulizi ya Chelsea.
Leicester wameshinda mechi mbili pekee kati ya nane walizocheza msimu huu kwenye Ligi Kuu na wapo nafasi ya 13 ikiwa na pointi nane, huku Chelsea wakijivuta hadi nafasi ya tano na kufikisha pointi 16.
Katika mechi ya Arsenal ambayo walimaliza wakiwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya Granit Xhaka kutolewa nje kwa kadi nyekundi, mabao yake yalifungwa na Theo Walcott dakika ya 26 na 33, kabla ya Mesut Ozil kufunga bao la tatu dakika ya 57.
Mabao ya Swansea yalifungwa na Gylfi Sigurdsson dakika ya 38 na jingine likawekwa kimiani na González Tomás dakika ya 66.
Wao Man City walilazimika kutoka nyuma kuweza kusawazisha na kumaliza mchezo wa sare ya bao 1-1 dhidi ya Everton, huku mabao kwenye mchezo huo yakifungwa na Romelu Lukaku dakika ya 64 na Nolito dakika ya 72.
Katika mechi nyingine, waliopanda daraja msimu uliopita, Bournemouth iliwafurumusha Hull mabao 6-1, huku Stoke ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Sunderland na West Brom wakailazimisha Tottenham sare ya kufungana bao 1-1.

No comments:

Post a Comment